Saturday, December 24, 2016

VIFO VYA WATOTO WADOGO MBINGA VYAPUNGUA

Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa vifo vitokanavyo na watoto waliochini ya umri wa miaka mitano katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, vimepungua kwa kiasi kikubwa ambapo katika kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu ni watoto wa nne tu, ndio waliofariki dunia sawa na watoto wawili kwa kila walipokuwa watoto 100,000.

Mary Ngonyani ambaye ni Mratibu wa kitengo cha huduma ya afya, uzazi na mtoto wilayani humo alisema pia kwa ujumla vifo vya watoto hao husababishwa hasa na wale wanaozaliwa kabla ya kutimiza umri wa kuzaliwa (njiti) na magonjwa mengine ya akina mama pale anapokuwa mjamzito.

Alifafanua kuwa upungufu wa vifo hivyo unatokana na jitihada zinazofanywa na wataalamu wa kitengo hicho kuendelea kupambana na kudhibiti tatizo hilo ili lisiweze kuendelea kuwepo au kujitokeza, kwa kufikisha elimu husika katika jamii hususan kwa akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya.


Ngonyani alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake ambapo aliongeza pia, wameweza kudhibiti vifo vya wazazi katika kipindi hicho na havijaweza kutokea.

Vilevile alieleza kuwa akina mama wajawazito wanaokuwa chini ya uangalizi wao huwasisitiza kuhudhuria kliniki mara kwa mara ili waweze kupima afya zao, kwa kuangalia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), chanjo na magonjwa ya malaria ambayo husababisha vifo visivyokuwa vya lazima.

“Kwa ujumla mahudhurio ya akina mama hawa ni mazuri lakini wengi wao wamekuwa wakichelewa kuwahi kuhudhuria kliniki na kwamba katika utekelezaji wa miezi ya Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, ni asilimia 39 tu ndio wamekuwa wakihudhuria huku asilimia 70 wakipewa dawa za kuzuia ugonjwa wa malaria”, alisema Ngonyani.

Alifafanua kuwa katika kipindi hicho waliohudhuria walikuwa ni 8,247 sawa na asilimia 97.1 wamefaulu kuwapima pia Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kwamba kati ya hao waliogundulika kuwa na maambukizi mapya ya ugonjwa huo ni 154 ambao nao ni sawa na asilimia 1.9 ambapo wanapatiwa dawa ili kuweza kulinda afya zao na mtoto aliyekuwa tumboni aweze kuzaliwa akiwa salama.


Pamoja na mambo mengine alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ili kuweza kuwafikia walengwa na kutoa huduma husika ipasavyo ni ukosefu wa gari la kuwafikia walengwa vijijini na kufanyia shughuli katika kitengo hicho cha mama na mtoto.

No comments: