Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
KATIKA kuhakikisha kwamba ugonjwa hatari wa malaria
unaendelea kudhibitiwa, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma katika
kipindi cha mwezi Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu, imesambaza
vyandarua 42,174 kwa watoto wa shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani
humo.
Aidha hali ya maambukizi ya ugonjwa huo katika wilaya hiyo
imepungua kwa asilimia 24 kutokana na wataalamu wa afya kuendelea kuhimiza
wananchi kuweka mazingira yao wanayoishi katika hali ya usafi wakati wote ili
kuepukana na mazalia ya mbu wanaobeba vimelea vya ugonjwa huo.
Kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mbinga, Sarah
Komba alisema hayo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini
kwake juu ya halmashauri yake ilivyojiwekea mikakati ya kupambana na ugonjwa
huo kwa lengo la kupunguza maambukizi na vifo visivyokuwa vya lazima
vitokanavyo na malaria.
Komba alisema kuwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba
mwaka jana wagonjwa wa nje 53,671 waliweza kupatiwa matibabu ambao walionekana
kuwa na vimelea vya ugonjwa huo.
“Katika kufanikisha hili tumekuwa tukihamasisha kufanya usafi
wa mazingira ili kuweza kupunguza mazalia ya mbu na kutoa elimu ya afya kupitia
mikutano mbalimbali katika vituo vya kutolea huduma”, alisema.
Hata hivyo changamoto kubwa wanayokabiliana nayo hivi sasa ni
upungufu wa watumishi 253 ambapo waliopo ni 184 huku mahitaji halisi yakiwa ni
437 ambapo wanaiomba serikali, iendelee kukabiliana na hali hiyo kwa kuajiri
watumishi wengine ili kuweza kufikia malengo husika katika sekta hiyo ya afya.
No comments:
Post a Comment