Na Julius Konala,
Songea.
WANACHAMA wa chama cha akiba na mikopo Mahanje SACCOS katika
Halmashauri ya Madaba wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya ukaguzi
wa vyama hivyo COASCO mkoani hapa kwa madai kuwa wameshindwa kutoa taarifa ya
ukaguzi wa chama hicho tangu mwaka 2014.
Malalamiko hayo yalitolewa jana na wanachama hao kwenye
mkutano mkuu wa 19 wa chama hicho, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
Tumaini uliopo mjini hapa, ambapo walidai kuwa hali hiyo inasababisha chama
chao kushindwa kupata mikopo na kufanya shughuli zao mbalimbali za kimaendeleo.
Akichangia hoja katika mkutano huo mshauri wa chama hicho,
Nathan Malangalila alisema kuwa vyama vingi vya ushirika wa akiba na mikopo
vimekufa kwa sababu ya kukosa usimamizi wenye uongozi makini pamoja na
kushindwa kutoa ripoti mbalimbali za ukaguzi.
Malangalila alisema kuwa pamoja na chama chao kutoa fedha kwa
ajili ya kufanyia ukaguzi husika, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika ambapo maofisa
wa COASCO mkoani humo wameonekana wakipokea fedha hizo bila ya kufanya kazi na
kupelekea usumbufu kwa wanachama wa Mahanje SACCOS.
“Viongozi wa COASCO wamekuwa wasumbufu kwa kuwa kila
wanapoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo mara wanasema ipo Dodoma mara ipo Madaba,
wakati sio kweli hivi tunaiomba halmashauri ya Madaba kwa kushirikiana na Ofisa
ushirika wa halmashauri hii kufuatilia jambo hili na tuweze kupata majibu
sahihi”, alisisitiza Malangalila.
Naye Meneja wa Mahanje SACCOS, Kassim Masengo akizungumza
katika mkutano huo alisema kuwa inashangaza kuona chama kinatoa gharama kwa
ajili ya ukaguzi lakini maofisa waliopewa dhamana wamekuwa wazembe katika
kukitembelea chama hicho kwa ajili ya kutoa ripoti za kaguzi zinazofanyika.
Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa chama hicho walisema
kuwa kuna kila sababu ya kuwakataa wakaguzi wa COASCO kwa ajili ya kuifanyia
ukaguzi ushirika wao kuytokana na kuonesha dhahiri kwamba wameshindwa kufanya kazi
hiyo na badala yake watafutwe watu wengine watakaoweza kufanya ukaguzi katika
chama hicho.
No comments:
Post a Comment