Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
IMEELEZWA kuwa tokea nchi hii ipate Uhuru, Rais wa awanu ya
tano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amekuwa wa kwanza
kuvunja rekodi katika ulipaji wa madeni mbalimbali ndani ya nchi, ambapo zaidi
ya shilingi bilioni 970 ameweza kulipa kwa wakandarasi na wadeni wengine ambao walikuwa wakiidai
serikali.
Suleiman Jaffo ambaye ni Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) alisema hayo jana alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma huku akiongeza kuwa,
nchi hii ilifikia mahali pabaya kwa sababu ya madeni hayo na watu wachache kuwa
wabinafsi wakitaka kujilimbikizia mali nyingi.
Alifafanua kuwa ufanisi huo wa ulipaji wa madeni umetokana na
serikali kuwa imara katika ukusanyaji wa mapato yake, ambapo imekuwa ikikusanya
shilingi bilioni 800 kila mwezi.
Hivyo aliwataka watendaji wa serikali ambao walikuwa
wakifanya kazi kwa mazoea muda wao umepita na wanapaswa kubadilika ili waweze
kuendana na kasi ya awamu ya tano, ambayo ina malengo ya kusimamia na
kutekeleza ipasavyo maendeleo ya wananchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na
baadaye.
“Watumishi wengi walizoea stahili ya uongozi uliopita hivi sasa
tunapaswa kubadilika kwenda na wakati kwa sababu Watanzania wanataka mabadiliko,
ndio maana wakati mwingine mnaona maamuzi magumu yamekuwa yakifanyika kwa lengo
la kuwafikishia maendeleo wananchi wetu”, alisema.
Pia amewataka Wakurugenzi watendaji katika halmashauri za
wilaya hapa nchini, kuketi na wakuu wao wa idara na kupanga malengo yenye
kuleta tija kwa maendeleo ya wananchi na kwamba, kwa mkuu wa idara ambaye
ataonekana kutotekeleza majukumu yake ya kazi ipasavyo achukuliwe hatua ikiwemo
kuondolewa katika cheo chake.
Aliongeza kuwa ikiwa wamepewa dhamana na serikali za mitaa watumishi
wanapaswa kuzungumza lugha moja na sio viongozi kugawanyika, jambo ambalo
linaweza kuwafanya wagombane na kuendeleza mifarakano isiyokuwa ya lazima ambayo
inarudisha nyumba maendeleo ya wananchi.
Vilevile akizungumzia juu ya madai mbalimbali ya watumishi
alisema kuwa serikali imechukua hatua kwa kuandaa kikosi kazi, ambacho kinafanya
uhakiki wa madeni hayo ikiwemo kuondoa wimbi la watumishi hewa.
Hata hivyo alieleza kuwa kila mwezi shilingi bilioni 25
zilikuwa zinaenda kwa watu hewa na kwamba zoezi hilo la uhakiki litakapokamilika
watumishi wote wanaoidai serikali watalipwa stahiki zao.
No comments:
Post a Comment