Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
NAIBU Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jaffo amesema kuwa ameshangazwa kupata
taarifa kwamba baadhi ya hospitali za serikali hapa nchini hazina dawa, wakati
serikali imekuwa ikituma fedha kila mwezi kwa ajili ya kununua vifaa tiba na
madawa ya kutibu wagonjwa.
Suleiman Jaffo. |
Aidha kufuatia hali hiyo ametoa onyo kali kwa Waganga wakuu
wa mikoa na wilaya kwamba endapo atasikia au kupata taarifa kuwa hospitali hizo
hazina madawa, wajiandae kuwajibishwa na kutolea maelezo fedha hizo za kununulia
dawa baada ya kuzipokea wamezitumia kwa shughuli gani.
“Sitegemei kusikia hata dawa aina ya Panadol hakuna, serikali
imekuwa ikileta fedha kwenye mahospitali yetu kupitia mfuko wa Busket fund
lakini taarifa nilizonazo kumekuwa na mchezo mchafu wa kutumia fedha za mfuko
huu, watu kulipana posho wakati wananchi wanateseka”, alisema Jaffo.
Hayo yalisemwa na Waziri huyo jana alipokuwa katika ziara
yake ya kikazi akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji wa Mbinga na
wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo
uliopo mjini hapa.
Jaffo alifafanua kuwa hategemei kusikia mchezo huo wa
kuchezea fedha za mfuko huo kwa matumizi ambayo hayaendani na maelekezo husika
yaliyotolewa na serikali, hivyo amewaagiza Wakurugenzi wa halmashauri hapa
nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo na wananchi
waweze kupata dawa pale wanapokwenda kutibiwa katika hospitali za serikali.
Pamoja na mambo mengine aliongeza kuwa kila baada ya miezi
mitatu hospitali ya mji wa Mbinga imekuwa ikipokea zaidi ya shilingi milioni
100 kwa ajili ya kununulia dawa na kwamba kwa upande wa hospitali ya wilaya ya
Mbinga, nayo imekuwa ikipokea shilingi milioni 254 kwa ajili ya kununua dawa hizo
za kutibu wagonjwa kutoka katika mfuko huo wa Busket fund.
No comments:
Post a Comment