Ni moja kati ya sehemu ya jengo la kituo cha afya Mjimwema Songea. |
Na Gideon Mwakanosya,
Songea.
BARAZA la
Madiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma limeridhia
na kupitisha ombi la kukipandisha hadhi kituo cha afya Mjimwema na kuwa
hospitali ya halmashauri ya Manispaa hiyo.
Ombi hilo liliwasilishwa katika baraza hilo ili hatua
nyingine ngazi za juu ziweze kuendelea na kuthibitishwa kuwa hospitali kamili.
Aidha kupandishwa huko na kuwa hospitali ni agizo lililotolewa
Januari 11 mwaka huu na Waziri wa afya, ustawi wa jamii, jinsia, watoto na
wazee Ummy Mwalimu alipotembelea kituo hicho.
Waziri Mwalimu aliagiza hayo kwa kuutaka uongozi husika wa
Manispaa hiyo kuwasilisha katika Wizara yake ombi hilo ili liweze kufanyiwa
kazi kwa mujibu wa taratibu husika na hatimaye kufikia maamuzi ya mwisho ya
kituo cha afya Mjimwema kuwa hospitali ya wilaya katika Manispaa hiyo.
Kwa mujibu wa kikao kilichoketi hivi karibuni kwenye ukumbi
wa Manispaa ya Songea mjini hapa kikiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo, Abdul
Mshaweji kilipokea taarifa hiyo na kuidhinisha upandishaji hadhi wa kituo
hicho.
Meya huyo alifafanua kuwa lengo la kuwa hospitali ya wilaya
ni kuweza kuboresha huduma mbalimbali za afya ambazo hazipatikani kwenye kituo
cha afya na sababu za msingi kuomba kuwa hospitali ni kuiwezesha halmashauri ya
Manispaa ya Songea kuwa na hospitali ya wilaya ambayo itaweza kuhudumia
wananchi wengi hasa wale wanaotoka katika maeneo ya pembezoni.
Kwa ujumla kituo cha afya Mjimwema kilianzishwa Aprili 8
mwaka 2002 ambapo kinahudumia wakazi zaidi ya 31,091 kati ya hao 1,213 ni
watoto chini ya mwaka mmoja na kwamba 5,845 ni watoto chini ya miaka mitano
huku 1,275 ni akina mama wajawazito.
Kituo cha afya Mjimwema kina jumla ya majengo nane yakiwemo
jengo la wagonjwa wa nje, wodi ya watoto na wanawake, wodi ya wazazi na huduma
za kujifungua, jengo la kutolea huduma za afya ya uzazi na mtoto na wodi ya
wanaume, jengo la utawala, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba mbili za watumishi
na jengo la upasuaji.
Mshaweji alieleza kuwa kituo hicho cha afya kina jumla ya
watumishi 110 wa kada mbalimbali na kwamba kinatoa huduma mbalimbali za afya
lakini hivi sasa huduma ambazo hazitolewi katika kituo hicho cha afya ni pamoja
na huduma ya upasuaji licha ya kwamba jengo husika limekamilika lakini vifaa
bado havitoshelezi kwa ajili ya mahitaji husika.
No comments:
Post a Comment