Na Dustan Ndunguru,
Geita.
WACHIMBAJI wadogo wa madini katika migodi ya Kakola na
Nyakagwe wilaya ya Kahama na Geita mkoani Geita, wamesema kuwa uamuzi aliochukua
Rais Dkt. John Magufuli wa kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza Makontena yenye
mchanga wenye madini ulikuwa ni wa busara kutokana na ukweli kwamba mchanga huo
uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, ulikuwa wenye madini jambo ambalo
lilikuwa likisababisha nchi kukosa mapato yake.
Dkt. John Magufuli. |
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi
wachimbaji wadogo, Robert Nyamaigolo na Golod Makinga walisema kuwa kila Mtanzania
ambaye ana uzalendo wa kweli anapaswa kupongeza jitihada hizo zilizofanywa na
Dkt. Magufuli baada ya kumaliza kazi hiyo na kuchukua hatua.
Nyamaigolo alisema uzoefu unaonesha kuwa miaka mingi tume za
kuchunguza masuala mbalimbali zilizokuwa zikiundwa zilikuwa hazitoi majibu
yenye kuzaa matunda na baadaye wananchi walikuwa wakikosa imani na serikali
yao.
“Rais Magufuli ameunda tume ya kuchunguza tatizo hili, mara
ilipobainika kulikuwa na uzembe kwa watendaji husika ambao wameufanya mara moja
amechukua hatua ya kuwawajibisha, ni jambo ambalo anapaswa kupongezwa hasa kwa
Watanzania ambao ni wazalendo na wenye uchungu na rasilimali za nchi yao”,
alisema Nyamaigolo.