|
Msanii wa filamu nchini, Senga upande wa kulia akiwa na msanii mwenzake katika picha ya pamoja, Gidion Kabrother. |
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.
CHARLES Kanumba ambaye ni baba wa aliyekuwa nguli wa
filamu hapa nchini, Marahemu Steven Kanumba amefunguka akisema kuwa alimtemea
mate msanii Gidion Simon maarufu kwa jina la Kabrother, ili aweze kufanikiwa
katika kazi zake za uigizaji wa filamu kama alivyokuwa mwanae Kanumba.
Alisema aliamua kufanya hivyo, ili ikiwezekana amrithi
mwanae huyo ambaye alikuwa ni rafiki yake kipenzi akishirikiana na mwanae, katika
kazi za uigizaji wa filamu kwa muda mrefu.
“Nilimtemea mate huyu mtoto, kwa sababu katika kazi
zake alikuwa mtu wa karibu sana na mwanangu wakishinda hapa nyumbani, hivyo
niliona nifanye hivi niweze kumpatia baraka na Mungu akimbariki aweze kuonyesha
maajabu kama mwenzake”, alisema.
Alifafanua kuwa, Kabrother wakati anaanza kazi zake za
uigizaji alikuwa akijifunza kupata ujuzi wa fani hiyo, kutoka kwa marehemu
Kanumba.
Hayo yalisemwa na Baba Kanumba, wakati alipokuwa
akizungumza na mtandao huu kwa njia ya simu ambapo aliongeza pia kwa kuwataka
waigizaji wa filamu hapa nchini, kuwa na ushirikiano katika kazi zao ili waweze
kusonga mbele katika tasnia yao ya sanaa na maigizo ya aina mbalimbali.
“Namsifu Kabrother kwa juhudi anazozifanya, ameanza
kazi hii kwa muda mrefu mpaka hapa alipofikia katika kukuza kipaji chake”,
alisema Baba Kanumba.