|
Gaudence Kayombo, Mbunge wa Mbinga Mashariki ambaye analalamikiwa na wapiga kura wake kwamba anatetea hakuna wizi wa kahawa uliofanyika kwa wakulima wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, jambo ambalo wanamshangaa na kumtaka afute kauli yake huku wakiiomba serikali iingilie kati ili waliohusika na hujuma hiyo wachukuliwe hatua za kisheria. |
Na Kassian
Nyandindi,
WAKULIMA wanaozalisha zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma wamesema wanamshangaa Mbunge wao wa Jimbo la Mbinga Mashariki, Gaudence
Kayombo kwamba hakuna mkulima anayelalamika juu ya wizi wa fedha baada ya
kahawa yao kuuzwa mnadani Moshi, hivyo wamemtaka afute kauli hiyo na
kushughulikia matatizo ya wananchi wa jimbo hilo, na sio kukaa kupinga
malalamiko yanayotolewa na wananchi wake huku akijua fika kufanya hivyo ni kuendelea
kuitesa jamii.
Kwa nyakati tofauti walisema wamekosa imani naye baada ya Mbunge
huyo hivi karibuni kusikika kwenye vyombo vya habari, TV na Magazeti akikanusha
na kusema wakulima hao wamenufaika na mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) na hakuna aliyeibiwa fedha, ambapo ni muda mrefu sasa umepita pamoja
na kufikishiwa malalamiko hayo mezani kwake juu ya wizi waliofanyiwa wakulima hao
lakini hakuna hatua aliyochukua huku wakiongeza kuwa, huenda anamaslahi yake
binafsi ndio maana amekuwa akitumia muda mwingi kutetea jambo hilo.
Walifafanua kuwa umefika wakati sasa, kiongozi aliyechaguliwa
na wananchi kuacha tabia ya kutetea watendaji wa serikali ambao ni wezi
wakiwaibia wakulima wanyonge na endapo ataendelea kufanya hivyo, ni sawa na
kuwatesa wapiga kura wake na kuwanyima fursa za kimaendeleo kwa faida ya kizazi
cha sasa na baadaye.
“Huyu Mbunge sisi tunamshangaa sana, anafikia hatua
anadanganya watu kupitia vyombo vya habari kwamba hakuna mkulima anayelalamika
katika jimbo lake ameibiwa fedha baada ya kahawa kuuzwa mnadani yeye anawezaje
kuthibitisha hili, hivyo asubiri mwarobaini wake ataupata uchaguzi mkuu ujao”,
walisema.
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa,
Mbunge Kayombo amefikia hatua ya kutoa kauli hizo baada ya Mkurugenzi wake,
Hussein Ngaga na viongozi wa vyama vya ushirika, kulalamikiwa na wakulima wa kahawa wilayani Mbinga kupitia vyombo
vya habari kuwa wanadaiwa kuwaibia shilingi milioni 783,399,412 katika sehemu ya
kahawa zao ambazo waliuza huko mnadani Moshi.
Wakulima hao ni wale ambao walikopeshwa fedha shilingi
bilioni 2 na shirika hilo la NSSF kupitia vyama vyao vya ushirika (AMCOS) vilivyopo
wilyani humo, ambapo lengo la shirika lilikuwa ni kutoa mikopo yenye gharama
nafuu kwa wakulima wadogo wadogo ambao wamejiunga kisheria katika vikundi,
hatimaye waweze kujikwamua kiuchumi na waondokane na umasikini.
Malalamiko haya yanafuatia pia, Mkurugenzi huyo kuingilia kati
na kupangia matumizi ya fedha juu ya mkopo huo ambao wakulima walikopeshwa,
jambo ambalo mpaka sasa amekuwa hataki kutoa hata mwenendo wa fomu ya mauzo ya
kahawa zao (Account Sale) ili wakulima waweze kujua hatma ya kahawa yao jinsi gani
ilivyouzwa huko mnadani.
“Tumekuwa tukinyimwa hata mwenendo wa matumizi ya fedha zetu tulizokopeshwa
na NSSF ambazo ziliingizwa katika akaunti zetu za vyama vya ushirika (Bank
Statement) ili tuweze kujua zimetumikaje, kwa sababu wakati wa manunuzi ya
kahawa mkurugenzi huyu alikuwa akitupangia matumizi tunakwenda kuchukua fedha
benki mpaka ruhusa itoke kwake na kiasi anachotaka yeye, sasa tunahoji hivi
kweli hizi ndizo taratibu na sheria za vyama vya ushirika zinavyosema?”,
walihoji.
Pamoja na mambo mengine, wakulima wanaolalamikia juu ya hali
hiyo wanatoka katika vyama vinne vya ushirika ambavyo ni Mahilo, Ngaka, Ngima
na Pilikano ambapo hata viongozi wao wa ushirika nao wanalalamikiwa kwamba wameshirikiana
na Mkurugenzi Ngaga kwa namna moja au nyingine kuhujumu fedha hizo za wakulima
wa kahawa, huku wakiiomba serikali kuingilia kati ili haki zao ziweze kupatikana.
KAYOMBO ARUSHIWA KOMBORA
Wakulima hao ambao walionekana kuendelea kujawa na jazba,
waliibua jipya huku wakiendelea kumrushia kombora Mbunge wao Kayombo wakisema kuwa,
mnamo mwezi Agosti mwaka 2012 alianzisha umoja wa wakulima wa kahawa
unaofahamika kwa jina maarufu la; Mbinga Umoja Coffee Association, ambao
ulilenga wakulima wa kahawa wilayani humo waweze kufanya biashara ya kuuza
kahawa yao kwa bei nzuri nchi za nje.