Damian Kapinga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa kata ya Ruanda mara baada ya kukabidhiwa baiskeli maalum ya kutembelea. |
Mbinga.
CHAMA Cha Walemavu Tanzania (CHAWATA) tawi la Mbinga mkoa wa
Ruvuma, kimetoa msaada wa baiskeli maalum ya kutembelea mlemavu Damian Kapinga
(22) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili, shule ya sekondari Ruanda
wilayani humo yenye thamani ya shilingi milioni moja.
Akikabidhi msaada huo shuleni hapo mbele ya Mkuu wa shule
Stephano Ndomba na Diwani wa viti maalum tarafa ya Namswea Immaculatha Mapunda,
Mwenyekiti wa chama hicho wilayani hapa Martin Mbawala alisema kuwa baiskeli
hiyo ya kutembelea mtoto huyo imepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na
chama, kutoka kwa wasamaria wema.
Mbawala alisema kuwa chama kimefanya jitihada ya kutafuta
baiskeli hiyo kutokana na taabu alizokuwa akizipata mtoto huyo kutambaa kwa
mikono na magoti wakati wa kwenda shule kuhudhuria masomo yake, hivyo kiliona
kuna kila sababu ya kumtafutia chombo hicho ili kumrahisishia asiendelee kupata
adha hiyo.
“Nakukabidhi baiskeli hii iweze kukusaidia na kukurahisishia
uweze kutembea na kuhudhuria masomo yako vizuri, nawaomba viongozi wa kata hii
ya Ruanda muendelee kumtunza mtoto huyu kama walivyo wenzake ambao hawana
matatizo ya ulemavu”, alisisitiza Mbawala.