Sunday, May 6, 2018

WAKULIMA WA KAHAWA RUVUMA WAISHUKIA BODI YA KAHAWA


Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

BAADHI ya Wakulima wanaozalisha zao la kahawa katika Wilaya ya Songea, Mbinga na Nyasa Mkoani Ruvuma wameitaka Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kuwawezesha kujisajili kwenye mfumo wa utoaji wa taarifa za masoko ya dunia, ili mauzo ya kahawa yao yaendane na soko hilo.

Pia walisema kuwa ili waweze kuuza kahawa yao moja kwa moja mnadani bila kupitia kwa mtu binafsi ni muhimu waingizwe kwenye mfumo huo ili watambue soko la dunia lipoje.

Walisema hayo kwa nyakati tofauti Mkoani humo wakati walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini.


Walisema kuwa kwa kufanya hivyo kutawafanya wakulima wa kahawa kuepukana na wafanyabiashara wajanja ambao huwatapeli fedha zao kupitia mauzo ya kahawa yao mnadani.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya kahawa Tanzania, Primus Kimaryo alipohojiwa alisema kuwa bodi hiyo inao uwezo wa kusimamia hilo na wakulima wataweza kuingizwa kwenye mfumo wa kupata taarifa za soko la dunia kwa wakati.

Alisema kuwa namna ya kuweza kujisajili na mfumo huo ni gharama ya dola za Kimarekani 1,000 na kwamba kupitia kwenye vyama vyao vya ushirika wataweza kuanza kuwasajili kuanzia mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

“Masoko yatakapofunguliwa na minada ya kahawa kuanza ndipo bodi inatarajia kuanza kazi hii ya kusajili wakulima mfumo wa utoaji taarifa za masoko ya dunia ili mauzo ya kahawa zao ziendane na soko hilo”, alisema Kimaryo. 

Vilevile Meneja wa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Wilayani Mbinga (MCCCO), Jonas Mbunda amenukuliwa na vyombo vya habari akiiomba Serikali kuweka sera itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa kwa wakulima pamoja na uhamasishaji unywaji wa kahawa ya ndani ya nchi.

Alisema Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba inatafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kuwafanya wakulima hao waweze kuuza kahawa yao kwa bei nzuri.

Mbunda alifafanua kuwa endapo itasimamia mambo hayo kikamilifu maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa Mkoani Ruvuma katika Wilaya hizo yatakuwa juu na hatimaye kuweza kufikia malengo husika.

Alibainisha kuwa MCCCO mkakati walionao hivi sasa katika kujiongezea mapato ni kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake ili kuweza kupata kiasi kikubwa cha kahawa kinachozidi asilimia 60 ambazo wanazipata hivi sasa.

Kadhalika mkakati mwingine walionao aliongeza kuwa watajenga kiwanda kidogo cha kusindika kahawa ya kunywa ambayo huyeyuka mara moja pamoja na kuendelea na biashara ya ununuzi wa kahawa bora.

“Kiwanda hiki cha kukoboa kahawa hapa Mbinga kinao uwezo wa kukoboa tani 12 za kahawa kwa saa na tani 30,000 katika msimu kwa mwaka, lakini tukiangalia kwenye orodha ya mapokezi wakati kiwanda kimeanza 1989 hadi sasa 2018,

“Hakuna uwezo wa kupokea kahawa zaidi ya tani 10,000 tumekuwa tukipokea tani 5,000 hadi 10,000 maana yake ni kwamba kinafanya kazi chini ya uwezo wake kutokana na uzalishaji wa kahawa hapa Mbinga kuwa kidogo”, alisema Mbunda.

Meneja huyo alisema kuwa hali ya uchumi wa kiwanda hicho kutoka mwaka 2012 hadi 2017 kinaendeshwa kwa faida na kwamba hakijawahi kupata hasara katika kipindi hicho cha miaka mitano na kwamba kimekuwa kikilipa kodi zote za Serikali na kimeweza kupata hati tuzo ya kuwa mlipa kodi mkubwa katika ngazi ya Wilaya kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.

Pamoja na mambo mengine Kiwanda cha kukoboa kahawa Wilayani Mbinga kinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 43 na asilimia 57 kutoka kwenye vyama vya ushirika vinavyolima zao la kahawa hapa nchini.

No comments: