Wednesday, January 31, 2018

RAIS MAGUFULI AWATAKA UHAMIAJI KUENDELEA KUSHUGHULIKIA WAHAMIAJI HARAMU



Na Mwandishi wetu,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ameitaka idara ya Uhamiaji hapa nchini kuendelea kushughulikia wahamiaji haramu pasipo kumwogopa mtu yeyote yule.

Dokta Magufuli alitoa agizo hilo leo wakati alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa hati ya kusafiria ya Kielektroniki jijini Dar es Salaam, huku akiipongeza Wizara ya mambo ya ndani kwa utendaji mzuri wa kazi.

Alisema kuwa Wizara hiyo anaipongeza kwa sababu Waziri mwenye dhamana na Wizara hiyo wakati anamteua alimpeleka pale akimwambia kwamba kuna changamoto nyingi na kwa kiasi kikubwa sasa zimetatuliwa.

SERIKALI YATOA GHARAMA MPYA HATI YA KUSAFIRIA



WAZIRI wa Mambo ya ndani ya nchi, Dokta Mwigulu Nchemba amesema kwamba gharama mpya ya hati ya kusafiria ya Kielektroniki itakuwa ni shilingi 150,000.

Hayo yalisemwa leo na Dokta Nchemba wakati wa uzinduzi wa hati hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo imezinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli.

Vilevile Dokta Nchemba alisema kuwa hati hizo za kusafiria (Pasipoti) zitakuwa na ukurasa zaidi ya mmoja na mwonekano mpya.

Monday, January 29, 2018

JAFO APIGA MARUFUKU UJENZI WA MADARASA YA UDONGO AU TEMBE

Seleman Jafo.
Na Lilian Lundo,
Maelezo Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Seleman Jafo amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halamshauri zote nchini, kuhakikisha kwamba wanajenga madarasa yenye ubora na viwango vinavyokubalika ili kuondokana na tatizo la baadhi ya Wilaya kuwa na majengo ya udongo au tembe.

Jafo alitoa agizo hilo leo mjini Dodoma alipokuwa akifungua mafunzo ya uongozi ya siku tano kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi toka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara yanayoendelea kufanyika katika ukumbi wa Hazina Mkoani humo.

“Sitaki kuona madarasa ya udongo, tembe na watoto kusomea nje hakikisheni matumizi ya mapato ya ndani yanagusa na kujibu matatizo ya wananchi”, alisisitiza Jafo.

BREAKING NEWS: AFISA MISITU HALMASHAURI MJI WA MBINGA AFUKUZWA KAZI

Baraza la Madiwani Halmashauri Mji wa Mbinga, likiwa limeketi juzi kwenye kikao chake cha robo ya pili katika ukumbi wa Jumba la Maendeleo mjini hapa.


Na Kassian Nyandindi,        
Mbinga.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma limemfukuza kazi aliyekuwa Kaimu Afisa misitu wa Halmashauri hiyo, David Hyera kwa kile walichoeleza kuwa baada ya kupatikana na hatia ya kutosimamia na kutekeleza majukumu yake ya kazi za utumishi wa umma ipasavyo.

Akizungumza katika kikao cha Baraza hilo cha robo ya pili kilichoketi juzi mjini hapa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kipwele Ndunguru alisema kuwa hatua ya kumfukuza kazi mtumishi huyo pia inatokana na kushindwa kusimamia mapato ya fedha za mradi wa uvunaji wa msitu.

Ndunguru aliutaja msitu huo kuwa ni wa Mbambi ambao ni wa Halmashauri ya Mji huo na kwamba baada ya Hyera kushindwa kutekeleza kikamilifu majukumu aliyopewa alisababisha kutokea kwa wizi wa mbao na upotevu wa mamilioni ya fedha za mradi huo.

VIWAVI JESHI WAHARIBIFU WA MAZAO WADHIBITIWA SONGEA



Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

WADUDU aina ya viwavi jeshi (Fally arm worms) ambao wameingia katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, tangu mwezi Mei mwaka jana mpaka sasa wamefanya uharibifu mkubwa wa mazao na wataalam husika wamefanikiwa kuwadhibiti kwa asilimia 95.

Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Manispaa hiyo, Zawadi Nguaro alisema kuwa viwavi hao wana uwezo wa kushambulia aina 80 ya mazao yakiwemo mahindi, miwa na mtama na kwamba tangu walipoingia katika Manispaa hiyo walianza kwa kushambulia nyasi.

Alisema kuwa wadudu hao waligundulika mwishoni mwa mwezi Desemba 2017 wakiwa wameshambulia Hekta zaidi ya 1,000 za mahindi, ambapo wadudu hao hutoboa majani ya mahindi na kuchana kama kamba na kwamba wana uwezo wa kushambulia kwa kasi kubwa iwapo hawadhibitiwi haraka.

JAJI MKUU AZINDUA KITUO CHA MAFUNZO NA HABARI ZA MAHAKAMA



Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam. 

JAJI Mkuu, Profesa Ibrahim Juma amezindua kituo cha mafunzo na habari za Mahakama ili kuwajengea uwezo watumishi.
Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Akizindua kituo hicho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Januari 29 mwaka huu, Profesa Juma alisema malengo ya kufanya hivyo ni kuhakikisha haki inawafikia wananchi kwa wakati na kwa urahisi zaidi.

Profesa Juma alisema kituo hicho kimejengwa kwa kushirikiana na Benki ya Dunia.

Jaji Mkuu alifafanua kuwa wanawajengea uwezo watumishi wa Mahakama kwa sababu kuna mambo mengine hawakusoma wakiwa chuoni.

Saturday, January 27, 2018

SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI TUNDURU KULIMA KOROSHO

Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kubangua korosho cha Korosho Afrika Limited kilicopo Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, wakimsikiliza juzi Mkuu a Wilaya hiyo, Juma Homera (hayupo pichani) alipokwenda kwa ajili ya kusikiliza kero zao mbalimbali.


Na Muhidin Amri,          
Tunduru.

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Juma Homera ametoa agizo kwa shule zote za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuhakikisha wanalima ekari tatu za zao la korosho ikiwa hapo baadaye wakati wa mavuno ndiyo sehemu ya chanzo kikuu cha mapato.

Aidha alisisitiza kuwa endapo watazingatia hilo shule hizo zitakuwa na uwezo wa kujipatia fedha na kujitegemea kutoa hata chakula shuleni kwa wanafunzi wao na kufanya mambo mengine ya kimaendeleo.

Homera alikemea pia tabia ya baadhi ya wananchi kwenda kuchukua miche kwenye vitalu ambako imeeoteshwa na kuwauzia wengine kwa lengo la kujipatia fedha ambapo kwa atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

MADABA WAJIVUNIA MAFANIKIO UZALISHAJI MICHE YA KOROSHO



Na Kassian Nyandindi,
Madaba.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, katika msimu wa mwaka huu inatarajia kupanda miche ya zao la Korosho 55,020 sawa na ekari 1,965 ya zao hilo ikiwa ni mkakati uliojiwekea Halmashauri hiyo katika kuongeza vyanzo vyake vya mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.  

Shafi Mpenda ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba alisema kuwa pamoja na jitihada hizo Serikali kuu kupitia Bodi ya korosho Tanzania, imekuwa ikisaidia kuendeleza zao hilo kwa kuleta mbegu bora, miche iliyobebeshwa, vifaa vya kitalu, viuatilifu na kufanya mafunzo kwa wakulima wa zao hilo.

Mpenda alieleza kuwa tayari miche hiyo wamekwisha anza kusambaza kwa wakulima katika vijiji mbalimbali hasa vile vyenye hali ya hewa inayostawi vizuri korosho ikiwemo kijiji cha Mbangamawe, Ifinga, Ngadinda, Gumbiro, Lutukila, Mtyangimbole, Magingo, Kipingo na Mahanje.

SONGEA WANAFUNZI WASIORIPOTI SHULENI KUSAKWA NYUMBA HADI NYUMBA


Na Albano Midelo,       
Songea.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Palolet Mgema amesema kwamba Oparesheni ya kuwasaka wanafunzi wa madarasa ya awali, msingi na sekondari ambao hawajaripoti shule Wilayani humo itafanyika nyumba hadi nyumba kuanzia sasa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaripoti shuleni.
Palolet Mgema.

Alisema uchunguzi umebaini kuwa bado kuna idadi kubwa ya wanafunzi waliotakiwa kwenda shuleni, lakini bado wapo mitaani wakati Serikali inatoa elimu bure kuanzia msingi na sekondari kuhakikisha watoto wote wanapata elimu.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi wa madarasa ya awali waliopo shuleni hivi sasa ni asilimia 68 tu ya walioandikishwa ambao ni 4,395 kati ya wanafunzi 9,485 waliotarajiwa kuanza elimu ya awali mwaka huu.

WANAFUNZI NANDEMBO TUNDURU KUONDOKANA NA KERO UPUNGUFU WA MABWENI YA KULALA

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Homera, upande wa kulia akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa kike kidato cha sita shule ya Sekondari Nandembo Wilayani humo  alipokuwa katika ziara ya kukagua ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika shule hiyo.


Na Muhidin Amri,            
Tunduru.

WANAFUNZI wanaosoma kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Nandembo kata ya Nandembo Halmashauri Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, hivi sasa wataweza kuondokana na kero ya mahali pa kulala baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 160 kwa wakati mmoja.

Mary Ndunguru ambaye ni Mkuu wa shule hiyo alisema kuwa ujenzi wa mabweni hayo hadi kukamilika kwake zimetumika shilingi milioni 150 kwa kutumia mfumo wa Force Account ambapo mafundi wadogo ndiyo wanaotumika kufanya kazi hiyo badala ya kutumia Wakandarasi wakubwa.

Alisema kuwa ili kuweza kutosheleza mahitaji husika kila bweni litatumiwa na watoto 50 lakini baada ya bweni moja kuungua moto mwaka jana hivi sasa wanabweni moja tu na wanafunzi wengine hulazimika kuishi kwenye hosteli za Kanisa Katoliki Nandembo kwa gharama za wazazi wao.

UGONJWA WA NGURUWE WASUMBUA SONGEA


Na Albano Midelo,      
Songea.

UGONJWA hatari wa homa ya nguruwe umeingia katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambapo hadi sasa zaidi ya nguruwe 100 wamekufa.

Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Rozina Chuwa amesema kuwa katika kipindi cha wiki mbili, vimetokea vifo hivyo 100 vya nguruwe na kwamba hadi kufikia Jumapili iliyopita nguruwe 48 walikuwa wamekufa kutokana na ugonjwa huo.

Chuwa alisema kuwa ugonjwa huo unaenezwa virusi aina ya ‘African Swine Fever Virus’ na kwamba hauna kinga na unaenea kwa kasi kubwa katika Manispaa hiyo yenye jumla ya nguruwe 4,581 ambapo ametaja maeneo ambayo yanaongoza kuathirika na ugonjwa huo ni Lizaboni ambako nguruwe zaidi ya 100 wamekufa.

Thursday, January 25, 2018

DC TUNDURU APIGA MARUFUKU WATENDAJI WA SERIKALI KUCHANGISHA WANAFUNZI MICHANGO MBALIMBALI

Na Muhidin Amri,         
Tunduru.

MKUU wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Juma Homera amepiga marufuku Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Wilayani humo kuendelea kuwachangisha Wazazi michango mbalimbali kupitia wanafunzi wanaosoma katika shule za Serikali.

Aidha Homera amewaonya Walimu hao kwamba watakaobainika kuendelea na utaratibu wa michango hiyo, watachukuliwa hatua kali ikiwemo muhusika kufukuzwa kazi kuanzia Mkuu wa shule na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri husika.

Hayo yalisemwa na Mkuu huyo wa Wilaya wakati alipokuwa akizungumza na Maafisa tarafa, Wakuu wa shule za Sekondari, Waratibu elimu kata, Watendaji kata na Watendaji wa vijiji katika ukumbi wa Klasta ya Walimu tarafa ya Mlingoti mjini hapa.

Wednesday, January 24, 2018

RAIS MAGUFULI AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI JAJI MKUU WA TANZANIA

Rais Dokta John Pombe Magufuli.


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Jaji Mkuu wa Tanzania, Ibrahim Juma kutokana na kifo cha Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Robert Kisanga.

Jaji Kisanga alifariki dunia jana Jumanne Januari 23 mwaka huu katika Hospitali ya Regency Jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa leo Januari 24 mwaka huu imemnukuu Dokta Magufuli akisema kuwa Jaji Kisanga atakumbukwa kwa mchango wake alioutoa kwa Taifa hili wakati wote wa utumishi wake.

MWALIMU MBARONI KWA TUHUMA YA KUMPA MIMBA MWANAFUNZI MLEMAVU



Na Mwandishi wetu,
Kilwa.

MWALIMU mmoja wa shule ya wanafunzi wenye ulemavu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi, amefikishwa kwenye vyombo vya sheria kwa tuhuma ya kufanya mapenzi na mwanafunzi mwenye ulemavu na kumsababishia ujauzito.
Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai.

Akizungumza katika kongamano la Wadau wa elimu lililoandaliwa na shirika la TCRS, Mkuu wa Wilaya Kilwa, Christopher Ngubiagai alisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa na mwalimu huyo sio cha kukifumbia macho huku mwanafunzi aliyefanyiwa hivyo akiwa amekatisha kuendelea na masomo yake.

Ngubiagai alieleza kuwa Wilaya hiyo imekuwa akiathirika na tatizo la mimba za utotoni na utoro kwa wanafunzi mashuleni na husababisha watoto hao kufanya vibaya katika mitihani ya Kimkoa na Kitaifa.

WANANCHI TUNDURU WAVAMIA SHAMBA LA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA



Na Mwandishi wetu,            
Tunduru.

BAADHI ya Wananchi kutoka vijiji mbalimbali Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, wamevamia shamba la Chama Kikuu cha Ushirika (TAMCU) kilichopo Wilayani humo kijiji cha Mtetesi, lenye ukubwa wa ekari 3,150 na kuanza kufanya shughuli mbalimbali za kilimo cha zao la korosho.

Mbali na kilimo hicho Waandishi wa habari wameshuhudia wavamizi hao maeneo mengine ya ardhi katika shamba hilo wakikata miti iliyohifadhiwa na Chama hicho huku wengine wakichoma mkaa jambo ambalo linatishia kutokea kwa uharibifu mkubwa wa mazingira.

Pia watu hao wameanza kupanda minazi, miembe, mahindi, mbaazi na matunda mbalimbali huku wakiendesha shughuli za ufugaji katika shamba hilo.

Kufuatia uvamizi huo, Wajumbe wa bodi ya TAMCU wamelazimika kutembelea shamba hilo na kuwakuta wananchi wakiwa wamegawana  maeneo na baadhi yao kuweka makazi ya kudumu  kwa kujenga nyumba za matofali na bati.

WAKULIMA TUNDURU WAISHUKURU SERIKALI UGAWAJI MICHE BURE YA KOROSHO

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera upande wa kushoto akijifunza namna ya uandaaji wa miche bora ya korosho kwa njia ya kuotesha kutoka kwa mkulima wa zao la korosho ambaye hakutaka kutaja jina lake.


Na Muhidin Amri,                
Tunduru.

WAKULIMA wanaozalisha zao la korosho Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma wameipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Dokta John Pombe Magufuli, kwa uamuzi wake wa kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha na  kuimarisha zao hilo kwa kuzalisha  miche ambayo inatolewa bure kwa wananchi.

Walisema kuwa hatua hiyo itahamasisha wananachi wengi kuanza kulima zao hilo na kuweza kujikwamua na umaskini kwa kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati katika kuwasaidia wakulima.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza na mwandishi wetu walisema kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani imeonesha ni jinsi gani inavyowajali wananchi wake hasa kwa kuondoa baadhi ya kero za muda mrefu ambazo zilikuwa zikiwakatisha tama wakulima na kurahisisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo.

DC TUNDURU AIOMBA WIZARA YA MAJI KUSAIDIA UTEKELEZAJI MIUNDOMBINU YA MAJI


Na Kassian Nyandindi,      
Tunduru.
 
SERIKALI Wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, imeiomba Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuangalia uwezekano wa kuipatia Wilaya hiyo fedha shilingi milioni 300 ambazo iliomba, kwa ajili ya kusaidia kuharakisha utekelezaji wa ujenzi miundombinu ya maji katika mji wa Tunduru.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake juu ya maendeleo mbalimbali ya ujenzi wa miradi ya maji katika mji huo.

Homera alifafanua kuwa maombi hayo yalitokana na Mamlaka ya maji mjini hapa kuelemewa na ubovu wa miundombinu yake hali ambayo husababisha wananchi kutumia maji yasiyokuwa safi na salama.

Tuesday, January 23, 2018

RAIS DOKTA MAGUFULI AMTUMBUA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA BUTIAMA



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli leo Januari 23 mwaka huu ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Butiama Mkoani Mara, Solomon Ngiliule kutokana na ubadhirifu wa fedha za umma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Seleman Jafo ametangaza maamuzi hayo leo ikiwa zimepita siku tatu toka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotoa maagizo kwa Kaimu Katibu tawala wa Mkoa huo, Raphael Nyanda kutuma timu ya wakaguzi kwenda kufanya ukaguzi maalum katika Ofisi ya Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Butiama.

SHIRIKA LA UMEME TANESCO MKOANI RUVUMA LABEBESHWA LAWAMA MADABA


Na Muhidin Amri,       
Madaba.

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani Ruvuma, limeagizwa kufanya jitihada ya kupeleka nishati hiyo haraka katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo, ili watumishi waliopo huko waweze kutekeleza majukumu yao ya kutoa huduma bora kwa wananchi ipasavyo.

Aidha imeelezwa kuwa umeme huo utasaidia kupunguza gharama kubwa ya uendeshaji wa Ofisi kutokana na kutumia mafuta mengi kwa ajili ya kuendeshea Jenereta pale watumishi hao wanapofanya kazi husika.

Palolet Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alitoa agizo hilo juzi ambapo alisema kuwa anataka kuona TANESCO wanapeleka umeme haraka ili kuweza kunusuru hali hiyo isiendelee kuwepo.

CHANJO SARATANI KUTOLEWA BURE JAMII YATAKIWA KUPAMBANA NA UGONJWA HUO




Na Mwandishi wetu,

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kwamba kuanzia mwezi Aprili mwaka huu itaanza kutoa bure chanjo dhidi ya kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi (Human Papillon Virus) kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 14.

Aidha hatua hiyo inatokana na takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2012 kuonyesha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na  wagonjwa wapya wa saratani ya mlango wa kizazi 51 kwa kila wanawake 100,000 huku vifo vikiwa 38 kwa kila wanawake 100,000, ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki. 

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Dokta Faustine Ndugulile alisema hayo jana alipokuwa akizindua kampeni ya uchunguzi wa mabadiliko ya awali ya saratani hiyo na ya matiti, uliofanyika katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma.

Monday, January 22, 2018

WAKALA WA MAJENGO RUVUMA LAWAMANI UJENZI WA OFISI MADABA


Na Muhidin Amri,   
Madaba.

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoani Ruvuma, ametakiwa kumaliza ujenzi wa majengo ya Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani humo kwa wakati uliopangwa, ili kuweza kuwafanya watumishi waweze kupata sehemu nzuri ya kufanya kazi zao pale wanapowahudumia wananchi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.

TBA wameonywa pia wasitumie muda mwingi kukaa Ofisini badala ya kufanya kazi husika.

Palolet Mgema ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea alisema hayo juzi wakati alipokuwa amefanya ziara yake ya kushitukiza, kwa lengo la kukagua ujenzi huo.

Kadhalika Mkuu huyo wa Wilaya alisikitishwa kazi ya ujenzi ikiwa inasuasua huku kukiwa na idadi ndogo ya vibarua na mafundi.

MADABA WAZINDUA MPANGO MAALUM KILIMO CHA ZAO LA KOROSHO

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Palolet Mgema akizungumza na baadhi ya Wananchi wa kijiji cha Mbangamawe kata ya Gumbiro Halmashauri ya Wilaya ya Madaba wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji zao la korosho katika halmashauri ya Madaba.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Shafi Mpenda wa pili kushoto akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Songea, Palolet Mgema miche bora ya korosho iliyooteshwa katika vitalu kijiji cha Magingo Madaba siku ya mpango wa uzinduzi upandaji wa zao la korosho ambapo jumla ya miche 55,000 imesambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali Wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda upande wa kushoto akisaidiwa kupanda mche wa korosho na Mratibu wa zao la korosho, Paschal Umbu wakati wa uzinduzi wa mpango wa upandaji zao hilo uliofanyika katika kijiji cha Mbangamawe Madaba.


Na Kassian Nyandindi,       
Madaba.

MKUU wa Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma, Palolet Mgema ameongoza Wakulima wa kijiji cha Mbangamawe kata ya Gumbiro katika Halmashauri ya Wilaya Madaba Mkoani humo, kuzindua mpango maalum wa kilimo cha zao la korosho kwa kugawa na kupanda miche zaidi ya 55,020 ya zao hilo.

Akizindua mpango huo Mgema aliwataka Wakulima wa Madaba kuendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika mkakati wa kufufua zao la korosho na mazao mengine makuu ya biashara kama vile pamba, chai, tumbaku na kahawa.

Alifafanua kuwa Serikali imeamua kuimarisha zao la korosho hapa nchini baada ya kuonekana limekuwa ni zao ambalo lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo ya mtu mmoja mmoja.

Friday, January 19, 2018

DOKTA MAGUFULI ASIMAMISHA USAJILI WA MELI HAPA NCHINI

Dokta John Pombe Magufuli.


Na Mwandishi wetu,

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli ametoa agizo la kusitishwa kwa usajili wa meli mpya hapa nchini, kufuatia taarifa za kukamatwa kwa dawa za kulevya na bidhaa nyingine zinazopingwa kimataifa katika meli hizo ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania na sasa zimefikia tano.

Dokta Magufuli ametoa agizo hilo jana kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar, Balozi Ali Abeid Karume.

Kadhalika amemtaka Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo na kuhakikisha jina la Tanzania halichafuliwi ndani na nje ya nchi.

BREAKING NEWS: WAZAZI KIPIKA WAKUSANYIKA NA KUDAI WAPEWE FEDHA ZAO WALIZOCHANGISHWA KWA AJILI YA CHAKULA CHA WATOTO SHULENI


Baadhi ya Wazazi wakiwa wamekusanyika leo katika eneo la shule ya msingi Kipika Halmashauri Mji wa Mbinga wakishinikiza kupewa fedha zao, walizochangishwa kwa ajili ya chakula kwa watoto wao wanaosoma shuleni hapo.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KUFUATIA tamko la Rais Dokta John Pombe Magufuli la kusitisha michango kwa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini, baadhi ya Wakazi wanaoishi katika mtaa wa Matarawe Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma wamekusanyika katika eneo la viwanja vya shule ya msingi Kipika, iliyopo mjini hapa na kudai warudishiwe michango yao ya fedha walizochangishwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Tukio hilo limetokea leo Januari 19 mwaka huu majira ya asubuhi ambapo wakazi hao ambao ni wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo, walikusanyika katika eneo hilo baada ya Diwani wao wa kata hiyo Leonard Mshunju kuitisha mkutano wa dharula ili kuweza kujua hatma ya michango ya fedha, mahindi na maharagwe ambayo walichangishwa kwa ajili ya chakula cha watoto wanaosoma shuleni hapo.

Mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo, wakichangia hoja kwa nyakati tofauti wazazi hao walisema kuwa wao hawawezi kupingana na tamko lililotolewa na Rais Dokta Magufuli kwani wakati wanachangishwa michango hiyo baadhi yao walikuwa wakipewa vitisho huku wengine watoto wao wakikosa nafasi ya kuandikishwa kuanza shule darasa la awali kutokana na kukosa mchango husika.

SERIKALI YATOA TAHADHARI KUHUSU UGONJWA HATARI WA CHIKUNGUNYA

Ummy Mwalimu.


SERIKALI hapa nchini kupitia Wizara yake ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa tahadhari kuhusu ugonjwa wa Chikungunya ambao umeripotiwa na vyombo vya habari kutokea Mombasa nchini Kenya.

Waziri wa Wizara hiyo, Ummy Mwalimu ametoa taarifa yake leo Januari 19 mwaka huu akisema kuwa mpaka sasa Shirika la Afya Duniani (WHO) bado halijatoa taarifa rasmi lakini Serikali hapa nchini inatoa tahadhari kuzingatia muingiliano mkubwa wa watu baina ya nchi hizi mbili Kenya na Tanzania.

Kwa ujumla Wizara ya afya imefafanua kuwa ugonjwa wa Chikungunya unasababishwa na kirusi ambacho kinaenezwa na mbu aina ya Aedes na kusema ugonjwa huo si mgeni nchini Tanzania kwani ulishawahi kutokea.

Taarifa zaidi hii hapa;

PROFESA NDALICHAKO AWASHUSHIA RUNGU MUHAS MKUU WA KITENGO ASIMAMISHWA KAZI


Na Mwandishi wetu,

UWEPO wa madai ya harufu ya ufisadi ambao unadaiwa kufanyika katika kitengo cha Manunuzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) kumefanya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuagiza ufanyike uchunguzi ili kuweza kuwabaini wahusika na hatimaye wachukuliwe hatua za kisheria.

Profesa Joyce Ndalichako.
Wakati hilo likiendelea kutekelezwa pia Waziri huyo ameagiza kusimamishwa kazi kwa Mkuu anayehusika na kitengo hicho, pamoja na kuchunguzwa kwa wale wote wengine watakaohusika katika sakata hilo.

Hatua hiyo iliyochukuliwa na Profesa Ndalichako ilitokea juzi alipofanya ziara yake ya kushtukiza katika taasisi hiyo, kwa lengo la kujionea na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo.

Kadhalika uwepo wa ziara hiyo ulitokana na kubaini pia matumizi mabaya ya fedha za umma, ndipo ilimlazimu Waziri kufanya hivyo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua na kukomesha hali hiyo isiweze kujirudia tena.

Thursday, January 18, 2018

SERIKALI YATENGA BILIONI 1 KUENDELEA NA KAZI YA UJENZI MRADI MKUBWA WA MAJI MJI WA MBINGA

Picha hii ikionyesha baadhi ya maeneo mbalimbali ya Mji wa Mbinga.


Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Serikali katika mwaka huu wa fedha kupitia Wizara ya maji na umwagiliaji, imetenga jumla ya shilingi Bilioni 1 kwa ajili ya kuendelea na kazi ya kutekeleza sehemu ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.

Aidha mradi huo ni ule ambao kwa ajili ya kutekeleza uendelezaji wa vyanzo vinne vya maji, kutoka katika kijiji cha Tukuzi na ulazaji wa bomba kuu la uzalishaji maji kwa ajili ya kuweza kulisha Wakazi wanaoishi katika Mji huo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) Patrick Ndunguru, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya hali ya utoaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mbinga kwa Waandishi wa habari.

NAIBU WAZIRI WA UJENZI AMTAKA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI DARAJA MTO RUHUHU NYASA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kukifanyia ukarabati kivuko cha MV Ruhuhu kinachotoa huduma kati ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe ili kiweze kuendelea kutoa huduma kipindi chote wakati ujenzi wa daraja hilo unaendelea kufanyika.

Muonekano wa daraja la mto Ruhuhu linalojengwa Wilayani Nyasa na Mkandarasi wa Kampuni ya Lukolo kwa gharama ya shilingi bilioni 6, daraja hilo litaunganisha Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe.


Na Kassian Nyandindi,       
Nyasa.

NAIBU Waziri wa ujenzi, Elias Kwandikwa amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la mto Ruhuhu Wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kwamba anamaliza ujenzi wa daraja hilo kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Kwandikwa alitoa agizo hilo alipokuwa Wilayani humo akikagua ujenzi wa daraja hilo ambapo ameusisitiza Uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Makao makuu, kuhakikisha kwamba utaratibu wa zoezi zima la ununuzi wa vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo unaenda sambamba na makadirio ya muda wa mradi ili kufanya kazi hiyo ikamilike kwa muda uliopangwa.

“Nafikiri sasa jipangeni vizuri ili masika yanapokwisha mhakikishe mnafanya kazi kwa bidii ya hali ya juu, nataka kufikia mwezi Juni mwaka huu daraja liwe limekamilika, pia TANROADS Makao makuu hakikisheni mchakato wa manunuzi ya vyuma vya daraja hili mnauanza mapema ili kuweza kukamilisha mapema”, alisisitiza.

RC IRINGA ATEKELEZA AGIZO LA RAIS MAGUFULI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.


Na Mwandishi wetu,   
Iringa.

SIKU moja baada ya Rais Dokta John Pombe Magufuli, kupigilia msumari wa mwisho juu ya suala la michango kwa wanafunzi mashuleni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewataka walimu wakuu wa shule zote Mkoani humo kuandika barua kueleza aina ya michango iliyopo shuleni kwao na sababu za uwepo wake.

Masenza ameonya mwalimu ambaye atatoa taarifa za uongo katika barua yake hatua kali zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo ya kuondolewa katika nafasi yake ya kazi.

“Kwenye waraka ambao kila mtu anao unazungumzia elimu bila malipo, tayari Serikali ilishaelekeza namna ya kuendesha elimu bila malipo, waraka namba 3 wa mwaka 2016 ambao unazungumzia elimu bila malipo na waraka wa elimu namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango mbalimbali wanayopaswa kutoa wazazi kupitia kamati na bodi za shule,

SIMBA YAMTANGAZA RASMI KOCHA MPYA

Pierre Lechantre.


KLABU ya Simba leo imemtangaza rasmi Mfaransa Pierre Lechantre, kuwa Kocha mpya atakayekinoa kikosi hicho, ambacho kilikuwa hakina mwalimu baada ya kumfukuza aliyekuwa kocha wake, Joseph Omog mwishoni mwa mwaka jana.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Klabu hiyo, Haji Manara imeeleza kuwa kocha huyo ataanza kazi mara moja na atasaidiwa na kocha msaidizi wa sasa Masoud Djuma.

Masoud ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo, na kwamba Mfaransa huyo atashuhudia mchezo wa Simba SC dhidi ya Singida United leo Januari 18 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.

SERIKALI YASITISHA UUZAJI WA MALI ZA CHAMA CHA USHIRIKA KILIMANJARO WABADHIRIFU KUCHUKULIWA HATUA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Na Mwandishi wetu,             
Tarime.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira kusitisha uuzwaji wa mali za Chama cha Ushirika cha Kilimanjaro (KNCU).

Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati alipokuwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, uliofanyika kwenye uwanja wa Serengeti Wilayani Tarime Mkoani hapa.

Hatua hiyo imekuja baada ya KNCU kutangaza kuuza shamba lake kwa ajili ya kuiwezesha benki yake ya KCBL kutimiza sharti la mtaji la Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Wednesday, January 17, 2018

JUHUDI LITUMBANDYOSI MBINGA KUANZISHA DUKA LA PEMBEJEO ZA KILIMO CHA KOROSHO

Baadhi ya wanachama wa kikundi cha Juhudi, kilichopo katika kijiji cha Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi wakiwa kwenye kitalu cha miche bora ya mikorosho ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, kwa kushirikiana na wanakikundi hao wamezalisha miche hiyo kwa ajili ya kuwagawia bure wakulima wa korosho katika kata hiyo ili waweze kuipanda kwenye mashamba yao katika msimu wa mwaka huu.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WANACHAMA wa kikundi cha Juhudi waliopo katika kijiji cha Litumbandyosi kata ya Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, ambao wanajishughulisha na kilimo cha zao la korosho wanatarajia kuanzisha duka la pembejeo la zao hilo ili waweze kupata pembejeo kwa urahisi.

Mhasibu wa kikundi hicho, Athanas Nyimbo aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa kuanzisha kwa duka hilo wanatarajia kuanza na mtaji wa shilingi milioni mbili, fedha ambazo watapewa na Serikali kutokana na mgawo wa asilimia 30 baada ya kazi waliyofanya ya uzalishaji wa miche bora ya korosho ambayo itaanza kusambazwa kwa wakulima wa kijiji hicho.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa duka hilo itakuwa ni msaada mkubwa kwao katika kijiji hicho na maeneo mengine ya jirani na kata ya Litumbandyosi, kwani hivi sasa wamekuwa wakilazimika kufuata huduma ya pembejeo za korosho umbali mrefu Wilayani Tunduru.

HALMASHAURI MJI WA MBINGA WATAKIWA KUPANDA MITI RAFIKI YA MAJI



Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wametakiwa kuendelea kupanda miti rafiki ya maji kwa wingi hasa kipindi hiki ambacho ni cha mvua za masika katika maeneo yenye vyanzo vya maji, ili kuweza kuondokana na tatizo la upungufu wa maji katika kipindi cha kiangazi.

Mwito huo umetolewa jana na Meneja wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MBIUWASA) katika Mji huo, Patrick Ndunguru wakati wa zoezi ambalo mamlaka hiyo inaendelea nalo la upandaji miti kuzunguka vyanzo mbalimbali vya maji ndani ya mji huo.

“Mkakati tulionao wa mamlaka hii ni kurudisha uoto wa asili katika vyanzo vya maji ambavyo vimeanza kupotea kutokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli zao ikiwemo kilimo”, alisema.

TBA YAENDELEA NA UJENZI WA OFISI YA DC NA DED NYASA


Na Muhidin Amri,     
Nyasa.

WAKALA wa majengo Tanzania (TBA) kupitia kikosi chake cha ujenzi Mkoani Ruvuma, ameanza kazi ya ujenzi wa miradi minne ya majengo ya Serikali Wilayani Nyasa Mkoani humo ambayo miradi hiyo inagharimiwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa huo pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.

Meneja wa TBA Mkoani hapa, Mhandisi Edwin Mnunduma alifafanua kuwa miradi yote minne inatekelezwa kwa kutumia rasilimali zilizopo Serikalini kupitia wataalamu waliopo katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya na Wakala wa majengo TBA.

Aidha alisema kuwa kikosi cha ujenzi huo kinajenga majengo yake kwa kutumia njia ya kubuni na kujenga kwa pamoja ili kuweza kutekeleza miradi ya Serikali kwa gharama nafuu.

Tuesday, January 16, 2018

YANGA YALAMBA DILI LA BILIONI MBILI



MABINGWA watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara Yanga, leo wamesaini mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya michezo, Macron wenye thamani ya shilingi bilioni mbili.

Katika mkataba huo uliosainiwa kwenye makao makuu ya klabu hiyo, Yanga itatoa haki zote za utengenezaji na usambazaji wa jezi zao huku pia nembo ya kampuni ya Macron, itaanza kuonekana kwenye jezi za Yanga SC.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amewaonya wote wanaouza jezi za klabu hiyo bila kuwepo kwa makubaliano watawachukulia hatua za kisheria kwa sababu sasa yupo mwenye haki ya kufanya hivyo. 

WANACHAMA BIMA YA AFYA WALALAMIKIA KUBAGULIWA



Na Mwandishi wetu,

BAADHI ya Wananchi ambao wamejiunga na mfuko wa Bima ya afya katika Halmashauri ya Busokelo Wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya wamelalamikia wauguzi kwenye vituo vya afya katika halmashauri hiyo, kuwabagua wagojwa wanaokwenda kutibiwa wakiwa na kadi za bima ya afya na kutoa kipaumbele kwa wagonjwa wanaolipa fedha taslimu hali ambayo wamedai kuwa inakwamisha jitihada za Serikali kuhamasisha wananchi kujiunga na bima za fya nchini.

Wananchi hao wametoa malalamiko yao mbele ya Mbunge wa jimbo la Busokelo, Atupele Fred Mwakibete wakati walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara baada ya Mbunge huyo kufika katika kijiji cha Matamba kwa lengo la kukagua ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.

Akizungumza na wananchi hao, Mwakibete ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko hayo huku akiwahimiza wananchi hao kuungana pamoja kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa la zahanati hiyo ambalo kutokana na ubora wake linaweza kubadilishwa na kuwa kituo cha afya.

CHIKAMBO AWAPA SOMO WANAWAKE RUVUMA


Na Muhidin Amri,         
Songea.

MBUNGE wa Viti maalum Mkoa wa Ruvuma, Sikuzan Chikambo amewataka wanawake wa mkoa huo kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili waweze kujiletea maendeleo katika familia zao na kuweza kuondokana na umaskini.

Aidha Chikambo amewakumbusha wanawake hao kutumia fedha wanazopata kuanzisha vikundi vya ujasiriamali na kutumia kwa ajili ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa nyumba bora za kuishi na kupeleka watoto wao shule.

Mbunge huyo alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na wanachama wa Jumuiya  ya Wanawake ya Chama cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Songea  Mkoani hapa na kusisitiza kuwa wanawake hao wanao mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

DED MADABA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KWENDA KUWEKEZA MADABA


Na Muhidin Amri,           
Madaba.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, Shafi Mpenda amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza katika maeneo mbalimbali Wilayani humo, kufuatia Halmashauri hiyo kutajwa kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa nyingi zinazofaa kwa shughuli za uwekezaji hapa nchini.

Mpenda alitoa wito huo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na fursa  rafiki zilizopo huko ambazo bado hazijafanyiwa kazi licha ya Wilaya ya Madaba kutajwa kuwa ni sehemu nzuri kwa shughuli za uwekezaji.

Alisema kuwa Halmashauri hiyo bado kuna rasilimali nyingi ikiwemo ardhi nzuri yenye rutuba inayofaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama vile kahawa, chai, korosho, mahindi tangawizi pamoja na uwepo wa mto Ruhuji wenye samaki wengi wazuri ambao hawapatikani sehemu yoyote hapa nchini na misitu mikubwa yenye wanyama kwa ajili ya shughuli za utalii na uwindaji.