Monday, November 27, 2017

CCM RUVUMA YAIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI NAFASI YA UDIWANI




Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimeibuka kidedea kwa kuwa mshindi katika chaguzi za nafasi ya udiwani zilizofanyika mkoani humo baada ya wagombea wake kushinda kwa kura nyingi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa Katibu wa CCM mkoani humo, Amina Imbo alisema kuwa uchaguzi huo uliofanyika ulirudiwa baada ya wagombea wake kufariki dunia.

Imbo alisema kuwa katika mkoa huo kata ambazo uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika ni kata ya Mhongozi iliyopo wilayani Mbinga, Lukumbule na Kalulu zilizopo wilayani Tunduru mkoani hapa.

WAGANGA WAKUU MIKOA NA WILAYA WAPEWA MENO

Na Kassian Nyandindi,   
Namtumbo.

WAGANGA Wakuu wa mikoa na wilaya hapa nchini wameagizwa kuendelea kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa sekta ya afya ambao wanajihusisha na vitendo vya wizi wa dawa za Serikali.

Kassim Majaliwa ambaye ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo hilo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliojumuisha wananchi pamoja na viongozi wa wilaya ya Namtumbo katika uwanja wa michezo mjini hapa.

Alisema kuwa katika kuimarisha sekta hiyo Serikali imeongeza bajeti ya fedha kutoka shilingi bilioni 32 hadi kufikia bilioni 220 kwa mwaka huku akisisitiza dhamira ya Serikali ina lengo la kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa dawa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali zake za Serikali kote nchini.

Saturday, November 25, 2017

MAJALIWA ASIKITISHWA NAMTUMBO KUWA NA REKODI MBAYA WANAFUNZI KUPATA UJAUZITO

Na Kassian Nyandindi,  
Namtumbo.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuweka miundombinu ya uhakika katika sekta ya elimu hapa nchini, ili kuweza kutoa fursa kwa watoto waliopo shuleni waweze kusoma vizuri na kutimiza malengo yao ya maendeleo ya maisha ipasavyo.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Nasuli wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma huku akiwataka wazazi watekeleze jukumu la kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule ni lazima apelekwe shuleni ili aweze kusoma.

Aidha alifafanua kuwa mpango wa Serikali hivi sasa ni  kuhakikisha kwamba kila kwenye shule ya kidato cha kwanza hadi cha nne kunakuwa na shule ya kidato cha tano, ikiwa ni lengo la kuwarahisishia watoto wanaofanya vizuri katika mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne waendelee na  masomo yao jambo ambalo litasaidia kupata vijana wengi watakaokwenda vyuo vikuu.

MIGOGORO NAMTUMBO YAMCHUKIZA WAZIRI MKUU ASEMA INAKWAMISHA KUKUA KWA MAENDELEO YA WANANCHI

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Na Kassian Nyandindi,    
Namtumbo.

SERIKALI imewataka watumishi wa umma wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, kuchapa kazi na kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea ili waweze kuleta tija sehemu ya kazi badala ya kutumia muda mwingi katika migogoro inayorudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipokuwa akizungumza na watumishi wa umma wa wilaya hiyo akiwa katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi siku tatu mkoani Ruvuma.

Alisema kuwa Serikali imedhamiria kuwatumikia na kuwaletea maisha bora wananchi, hivyo kila mtumishi ni lazima awajibike kwa kufanya kazi ipasavyo kwa lengo la kuchochea kukua kwa haraka maendeleo ya wilaya na wananchi wake kwa ujumla.

Wednesday, November 22, 2017

WASIMAMIZI UCHAGUZI MDOGO VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUFUATA TARATIBU

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage upande wa kulia akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Moshi hivi karibuni, kushoto kwake ni Mwanasheria mwandamizi wa NEC, Mtibora Seleman.
Na Clarence Nanyaro – NEC 

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage amewataka Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi hapa nchini, kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa katika maamuzi mbalimbali wanayofanya yenye maslahi kwa pande zote ili kuendeleza amani na utulivu tulionao.

Akizungumza na Wasimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Moshi, Jaji Kaijage alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vinashiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani ambao utafanyika Novemba 26 mwaka huu, ni muhimu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha kuwa maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni yanazingatiwa ili kuepusha uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.

Jaji Kaijage ambaye yuko katika ziara ya kutembelea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kushuhudia utekelezaji wa maadili hayo katika kampeni za uchaguzi huo.

MAKAMU WA RAIS AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WAKE WAKUU OFISI YA MAKAMU WA RAIS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan upande wa kulia akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira January Makamba, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Joseph Malongo na Naibu Katibu Mkuu Bi. Butamo Philip leo Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wake wakuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais leo Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kufanya nao mazungumzo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

WADAIWA SUGU TTCL KUPANDISHWA KIZIMBANI

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akizungumza na Menejimenti ya kampuni ya simu Tanzania (TTCL) wakati alipotembelea makao makuu ya kampuni hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwake na kuwataka kuwachukulia hatua wale wote wanaodaiwa madeni sugu, upande wa kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dokta Mary Sassabi.
Na Mwandishi wetu,

NAIBU Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa wadaiwa sugu ambao hawafuati taratibu za kulipa madeni wanayodaiwa na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) watapelekwa Mahakamani kwa mujibu wa sheria.

Hayo yalisemwa na Waziri huyo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi makao makuu ya Ofisi za TTCL jijini Dar es Salaam, akizungumza na Menejimenti ya kampuni hiyo.

Alisema kuwa wale wanaodaiwa ambao hawafuati taratibu za kulipa madeni hayo wanatakiwa wapelekwe Mahakamani kwani wamekuwa wakiendelea kutumia huduma za kampuni hiyo huku wakijua kuwa ni wadaiwa sugu.

RAIS MAGUFULI AKUTANA NA RAIS SHEIN NA BALOZI WA JAPAN IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida alipokutana naye na kufanya mazungumzo leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Alli Mohamed Shein walipokutana na kufanya mazungumzo leo Ikulu jijini Dar es Salaam.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA KUFANYA ZIARA KESHO MKOANI RUVUMA

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Novemba 23 mwaka huu anatarajia kuwasili mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku tatu na kupokelewa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na Serikali katika uwanja wa ndege uliopo Ruhuwiko mjini Songea.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme akizungumza leo na vyombo mbalimbali vya habari Ofisini kwake alisema kuwa Waziri Mkuu huyo anatarajia kuwasili katika uwanja huo mjini hapa majira ya saa saba kamili mchana.

Alisema kuwa mara baada ya kuwasili atapokea taarifa ya maendeleo ya mkoa huo na ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa ndege mjini Songea na baada ya hapo ataelekea wilayani Namtumbo ambapo atafungua ghala la MIVARF, kuongea na madiwani, watumishi wa umma na wananchi wa wilaya hiyo katika mkutano wa hadhara.

Monday, November 20, 2017

KAMBAS GROUP OF COMPANIES YATOA MSAADA VIFAA VYA UJENZI SHULE YA MSINGI MIPETA SONGEA

Mkurugenzi wa kampuni ya Kambas Group of Companies, Yahaya Yusuph wa pili kushoto akikabidhi msaada wa bati 100 kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema juzi kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa, Ofisi mbili za walimu na nyumba mbili za walimu wa shule ya msingi Mipeta kata ya Muhukuru Halmashauri ya wilaya ya Songea ambayo paa zake ziliezuliwa na upepo ulioambatana na mvua mapema mwanzoni mwa mwezi huu.

Mkurugenzi wa kampuni ya Kambas Group of Companies, Yahaya Yusuph katikati akikabidhi msaada wa mifuko ya saruji kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema kwa ajili ya ukarabati wa shule ya msingi Mipeta na nyumba mbili za walimu kata ya Muhukuru halmashauri ya wilaya ya Songea.
Na Muhidin Amri,     
Songea.

KAMPUNI ya Kambas Group of Companies, inayofanya utafiti wa makaa ya mawe katika kitongoji cha Mipeta na Manyamba kata ya Muhukuru Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, imetoa msaada wa mifuko ya saruji 150 na bati 100 kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa, nyumba mbili za walimu na ofisi ya shule ya msingi Mipeta iliyopo wilayani humo.

Mwanzoni mwa mwezi huu upepo mkali ulioambatana na mvua uliezua paa katika baadhi ya madarasa, ofisi za walimu pamoja na nyumba mbili za walimu hali iliyosababisha wanafunzi kuanzia darasa la kwa kwanza hadi sita kulazimika kusomea vyumba viwili vya madarasa huku walimu walioezuliwa nyumba zao za kuishi wakiomba hifadhi ya kulala kwa walimu wenzao na wenyeji wa kitongoji hicho.

Akikabidhi msaada huo jana kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Palolet Mgema Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Yahaya Yusuph alisema wameamua kutoa vifaa hivyo vya ujenzi ikiwa ni mkakati wa kampuni yake kuunga mkono mpango wa Serikali ya Rais Dokta John Pombe Magufuli ya kutoa elimu bure, hivyo yeye kama mdau wa maendeleo ameona ni vyema kuchangia vifaa hivyo ili watoto hao waweze kuendelea na masomo katika mazingira mazuri.

WANAFUNZI RUHUWIKO SEKONDARI SONGEA WATAKIWA KUEPUKA ANASA

Na Muhidin Amri,    
Songea.

WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Ruhuwiko mkoani Ruvuma inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedi ya 401 Tembo Kanda ya kusini, wametakiwa kusoma kwa bidii na kuzingatia masomo yao darasani ili waweze kutimiza ndoto ya kuwa viongozi bora watakao weza kulitumikia taifa hili.

Hayo yalisemwa  mwishoni mwa wiki na Mkuu wa mafunzo na utawala wa Brigedi hiyo Kanal John Mwaipaya wakati akizungumza na wananchi, walimu na wazazi katika mahafali ya 22 ya kidato cha nne shuleni hapo.

Aidha alisema kuwa lazima mwanafunzi atambue kwamba analo jukumu la kusoma kwa kujituma ili aweze kufanya vizuri katika mitihani yake ya mwisho jambo ambalo litamsaidia kuwa na uhakika wa ajira na  uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha ya kila siku.

DIWANI MBINGA MJINI B AMSHUKURU MBUNGE SIXTUS MAPUNDA KWA KUUNGA MKONO UJENZI WA VYOO VYA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI MBINGA

Katibu wa Mbunge wa jimbo la Mbinga mjini, Geddy Ndimbo akiwa ameshikana mkono na walimu wa shule ya msingi Mbinga mara baada ya kukabidhi vifaa vya ujenzi wa choo cha wanafunzi wa shule hiyo ambavyo vilitolewa na Ofisi ya Mbunge wa jimbo hilo Sixtus Mapunda, upande wa kulia aliyevaa koti rangi nyeusi ni diwani wa kata hiyo, Frank Mgeni ambaye naye alishiriki wakati wa makabidhiano hayo.


Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

OFISI ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga mjini katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, imetoa vifaa vya ujenzi kwa shule ya msingi Mbinga vyenye thamani ya shilingi milioni 1,178,000 kwa ajili ya kukamilisha kazi ya ujenzi wa choo cha wanafunzi wa shule hiyo.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mbunge wa jimbo hilo Sixtus Mapunda Katibu wa Mbunge huyo, Geddy Ndimbo alisema kuwa vifaa walivyokabidhi wanaunga mkono nguvu za wananchi ambao walijitolea kujenga vyoo vya matundu nane ili wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo waweze kuwa na mazingira mazuri yenye vyoo vya kisasa.

Ndimbo alifafanua kuwa shule hiyo ambayo ipo katika kata ya Mbinga mjini B vyoo walivyokuwa wanatumia watoto hao hapo awali, vilikuwa chakavu havifai kwa matumizi hivyo anawapongeza wananchi waliojitokeza na kuchangia michango yao ya ujenzi huo.

WATU 72 WANAOISHI KIPIKA MBINGA WANUSURIKA KUPOTEZA MAISHA WAKIDAIWA KUNYWA KINYWAJI CHENYE SUMU


Wagonjwa wanaodaiwa kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na sumu wakiwa wamelazwa katika hospitali ya Mji wa Mbinga.

Baadhi ya Wahudumu wa afya katika hospitali ya Mji wa Mbinga wakiendelea kuwahudumia wagonjwa jana ambao wanadaiwa kunywa kinywaji kinachodaiwa kuwa sumu aina ya togwa, ambacho hata hivyo hali za wagonjwa hao zinaendelea vizuri baada ya kuwahi matibabu katika hospitali hiyo.
Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

WATU 72 ambao ni Wakazi wa kitongoji cha Kipika kata ya Matarawe katika Mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamenusurika kupoteza maisha baada ya kunywa kinywaji aina ya togwa kinachodaiwa kuwa na sumu.

Aidha imeelezwa kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 19 mwaka huu majira ya mchana, ambapo kinywaji hicho walikunywa wakiwa kwenye sherehe (Harusi) iliyokuwa ikifanyika katika kitongoji hicho.

Mmoja kati ya wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wanaume hospitalini hapo, Chirwa Mohamed Hassan akizungumza na mwandishi wetu alisema kuwa baada ya kunywa kinywaji hicho na masaa machache kupita, ghafla yeye na wenzake walijikuta tumbo linauma na kuanza kuharisha mfululizo ndipo walikimbizwa hospitali kwa matibabu zaidi.

“Baada ya kula chakula tulipewa togwa tulikuwa tunakunywa masaa machache yalipopita ndipo tumbo lilianza kuuma na kuharisha lakini baada ya kuwahi hapa hospitalini, tunawashukuru waganga kwa kutupatia matibabu kwa uharaka na sasa tunajisikia kuna unafuu kidogo”, alisema Hassan.

Sunday, November 19, 2017

OFISI YA DED HALMASHAURI MJI WA MBINGA LAWAMANI WANAFUNZI MASUMUNI WASOMEA NJE YA MADARASA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma imeshushiwa tuhuma kwa kutelekeza baadhi ya miradi ya maendeleo ya wananchi kwa kushindwa kuchangia vifaa vya kiwandani pale inapofikia hatua ya kufanya hivyo.

Christine Mndeme Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Frank Mgeni ambaye ni diwani wa kata ya Mbinga mjini B, aliibua tuhuma hiyo katika kikao cha baraza la Madiwani lililoketi hivi karibuni mjini hapa na kueleza kuwa miradi hiyo ya wananchi halmashauri imekuwa ikishindwa kutekeleza hilo licha ya wananchi kuchangia nguvu zao kwa asilimia kubwa.

Mgeni alisema kuwa hata ujenzi wa choo katika shule ya msingi Mbinga iliyopo mjini hapa ambacho wananchi wamejitolea kwa nguvu zao kukijenga, licha ya kupeleka ombi kwa uongozi husika wa halmashauri hiyo ili waweze kupewa vifaa vya kiwandani kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo ni muda mrefu sasa umepita hakuna utekelezaji uliofanyika.

KAYOMBO AMWAGIWA SIFA MCHANGO WAKE WA KUKUZA SEKTA YA ELIMU MBINGA

Viongozi mbalimbali wa wilaya ya Mbinga wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Ubalozi wa Korea kusini akiwemo na aliyekuwa Mbunge wa Mbinga, Gaudence Kayombo (Aliyeketi akiwa amevaa suti rangi nyeusi kutoka upande wa kulia) siku ya uzinduzi wa eneo la ujenzi wa Kituo cha elimu, Novemba 15 mwaka huu katika eneo la mtaa wa Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa.  
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

PONGEZI zimetolewa na baadhi ya Wananchi wanaoishi katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, kwa jitihada za kuchangia maendeleo katika mji huo zinazofanywa na aliyekuwa Mbunge wao, Gaudence Kayombo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wananchi hao walisema kuwa Kayombo, wanampongeza kwa kutafuta Wafadhili kutoka Ubalozi wa Korea kusini na hivi sasa wanatarajia kuanza kujenga Kituo cha elimu katika mtaa wa Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa.

“Ushirikiano huu anaoufanya wa kutujali na kutukumbuka sisi wananchi wake ni ishara tosha inayothibitisha ni mtu ambaye anafaa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo yetu, tunachoomba kituo hiki kijengwe kwa wakati ili kuweza kuanza kutoa huduma kwa jamii”, walisema.

HALMASHAURI YASHINDWA KULIPA FIDIA WANANCHI WAREJESHEWA VIWANJA VYAO

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

HATIMAYE Wananchi wa kata ya Lusonga waliopo katika halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamerejeshewa viwanja vyao ambavyo vilitwaliwa kwa muda mrefu na halmashauri hiyo kwa makubaliano kwamba watalipwa fidia.

Aidha hatua ya kurejeshewa viwanja hivyo imefuatia baada ya halmashauri hiyo kukosa fedha za kuweza kutekeleza jambo hilo.

Muafaka wa kurejesha viwanja mikononi mwa wananchi wa kata hiyo ulifikia juzi kwenye kikao cha baraza la Madiwani wa mji huo, lilikoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi uliopo mjini hapa.

UUZWAJI MAGUNIA KIHOLELA MTWARA WAMTIBUA NAIBU WAZIRI KILIMO

Naibu Waziri wa Kilimo, Mary Machuche Mwanjelwa akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Gasper Byakwana wakikagua baadhi ya magunia ambayo yamewasilishwa katika Ofisi ndogo ya Chama cha ushirika wilayani Masasi mara baada ya kumalizika mnada wa tano wa Korosho kijijini Chiungutwa wilayani humo. 
Na Mathias Canal,
Mtwara.

NAIBU Waziri wa kilimo, Mary Machuche Mwanjelwa amemtaka Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Mtwara, kukamilisha haraka kazi ya uchunguzi kwenye bodi za vyama vya ushirika mkoani humo ili kubaini sababu zilizosababisha kuuzwa kwa magunia kiholela bila kufuata taratibu.

Alisema kuwa kumalizika kwa uchunguzi huo kutarahisisha kuchukuliwa haraka hatua kali za kisheria kwa wale wote watakaobainika kukiuka sheria namba 17 ya vyama vya ushirika.

Naibu Waziri huyo alitoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Chiungutwa, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara mara baada ya kugundua kuwa kuna viashiria vya ukiukwaji wa taratibu katika upatikanaji wa magunia ya kuhifadhia korosho wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

Saturday, November 18, 2017

AGIZO LA RAIS MAGUFULI LA PUUZWA

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WAKATI Rais Dokta John Pombe Magufuli akisisitiza suala la usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hali hiyo imekuwa kinyume kwa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo agizo hilo linaonesha kupuuzwa kutotekelezwa ipasavyo na sasa mji huo umeshamiri uchafu katika mitaa yake na kuwa kero katika jamii.

Mara baada ya Rais Dokta Magufuli kuingia madarakani Novemba 5, mwaka jana alianzisha Operesheni maalum ya kufanya usafi ambayo imeendelea hadi sasa, kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa ndiyo siku ya usafi kuanzia alfajiri hadi saa 5:00 asubuhi.

Katika uzinduzi huo Rais alifanya usafi eneo la Feri jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu walifanya eneo la Kariakoo huku viongozi wengine wakishirikiana na wananchi kufanya usafi katika maeneo yao.

Hivyo basi pamoja na wananchi wa mji huo kuchangishwa fedha mara kwa mara kwa ajili ya kufanyia utekelezaji wa kazi hiyo lakini hakuna jitihada zinazo onesha kuzaa matunda.

HATI ZA KUMILIKI ARDHI KUTOLEWA NDANI YA SIKU 30 TANGU KUPOKELEWA KWA MAOMBI

Waziri wa ardhi nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi.
Na Frank Mvungi - Maelezo,
Dodoma.

SERIKALI imeanza kutoa hati za kumiliki ardhi ndani ya kipindi cha siku 30 tangu kupokelewa kwa maombi tofauti na awali ambapo mchakato wa kupata hati hizo ulichukua zaidi ya siku 90, ikiwa ni matokeo ya mikakati madhubuti iliyowekwa ili kuondoa changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi hapa nchini.

Akizungumza katika kipindi maalum cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO), Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kwamba kila kipande cha ardhi kinapimwa na kumilikishwa.

“Tumejipanga vizuri na sasa taarifa zote za ardhi zitakuwa katika mfumo wa kielektroniki utakaounganisha taarifa za nchi nzima hivyo tutaweza kudhibiti vitendo vyote vilivyokuwa vikifanyika awali kinyume na utaratibu na kuchochea kuongezeka kwa migogoro ya ardhi hapa nchini”, alisisitiza Lukuvi.

DED HALMASHAURI MJI WA MBINGA "AJISAFISHA" KWA MADIWANI WAKE

Madiwani wa Halmashauri mji wa Mbinga wakivaa majoho kabla ya kuanza kikao chao cha baraza la Madiwani kujadili taarifa za maendeleo ya wananchi robo ya kwanza ya mwaka kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Robert Kadaso Mageni amezungumza katika baraza la Madiwani wa halmashauri ya mji huo akieleza kwamba matatizo yaliyojitokeza nyuma kati yake na Madiwani hao hakuna ubaya wowote na kazi zinaendelea kufanyika.

Mageni alisema hayo juzi mbele ya msaidizi wa Katibu tawala wa mkoa huo, Joel Mbewa katika kikao cha Madiwani kilichoketi kwenye ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi mjini hapa.

Madiwani hao walipozungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu walisema kuwa kufuatia mgogoro mzito unaoendelea kufukuta kati yake na Madiwani wa mji huo, juu ya uvunaji wa msitu wa Mbambi ambao anashutumiwa kwamba yeye na baadhi ya watendaji wake wametafuna kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 800 ndiyo maneno hayo sasa amekuwa akiyazungumza kwa lengo la kutaka kujisafisha.

Thursday, November 16, 2017

KOREA KUSINI NA TANZANIA KUIMARISHA USHIRIKIANO KITUO CHA ELIMU KUJENGWA MBINGA

Uzinduzi wa ujenzi Kituo cha elimu ulifanyika jana katika kitongoji cha Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa, ambapo Balozi wa Korea kusini Song, Geum - Young ndiye aliyeshiriki kufanya kazi hiyo ya uzinduzi kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya ya Mbinga.  
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa ushirikiano uliopo kati ya Korea kusini na Tanzania, utaendelea kuimarishwa katika kusaidia kukuza maendeleo ya wananchi hapa nchini, hususan katika kuboresha sekta ya elimu na afya.

Aidha wananchi wa Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameombwa kuzingatia hilo ili viongozi wa ubalozi wa Korea kusini waweze kufanikiwa hatua ya kuboresha sekta hizo wilayani humo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Song, Geum – Young ambaye ni Balozi wa nchi hiyo hapa Tanzania alisema hayo jana wakati alipokuwa kwenye sherehe ya uzinduzi wa shughuli ya ujenzi wa Kituo cha elimu zilizofanyika katika mtaa wa Lulambo kata ya Matarawe mjini hapa.

NFRA MANISPAA SONGEA KUNUNUA TANI 400 ZA MAHINDI


Na Mwandishi wetu,       
Songea.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma imepangiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika msimu huu mkoani humo kununua mahindi tani 400.

Afisa kilimo wa Manispaa ya Songea, Mushoborozi Christian amefafanua kuwa halmashauri hiyo imepokea barua toka kwa wakala huyo ambayo inatoa maelekezo ya ununuzi wa mahindi hayo kwa awamu ya tatu msimu wa mwaka 2017/2018.

Alisema katika Manispaa ya Songea kata saba tu, kati ya kata 21 NFRA inaruhusiwa kununua mahindi katika vituo husika ambapo wananchi wanatakiwa kuyapeleka haraka kwa ajili ya kuuza.

WAUMINI ANGLIKANA SONGEA WACHANGA MAMILIONI YA FEDHA KUJENGA KANISA

Na Albano Midelo,    Songea

WAUMINI wa Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Augustino Mjimwema Songea Dayosisi ya Ruvuma, wamechanga zaidi ya shilingi milioni 57 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.

Katibu wa kanisa hilo Dokta Daniel Mtamakaya alisema ili waweze kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo, zinahitajika zaidi ya shilingi milioni 186.

Dokta Mtamakaya alisema kuwa kanisa hilo limefanikiwa pia kuchangisha zaidi ya shilingi milioni 33 ambazo zitatumika kwa ajili ya kuezeka kanisa na kwamba kinachohitajika hivi sasa ni shilingi milioni 15 ambazo ni gharama za kumlipa fundi.

KLINIKI TIBA MBADALA SONGEA ZAFUNGIWA KUTOA HUDUMA

Hiki ni moja kati ya kituo cha tiba mbadala kilichopo mjini Songea ambacho kimefungwa kisitoe huduma kutokana na kutokidhi vigezo husika.
Na Albano Midelo,    
Songea.

ZIARA ya kushitukiza ambayo ilikuwa ikiongozwa na Mganga mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dokta Gozibert Mutahyabarwa imefanyika katika Kliniki zilizopo katika Manispaa ya Songea na kubaini Kliniki mbili zinaendeshwa kinyume cha taratibu na sheria za tiba asili na tiba mbadala.

Baada ya ukaguzi huo kufanyika na timu mbili za wataalam wa afya ngazi ya mkoa huo na wale wa Manispaa hiyo wameweza kubaini vituo vya Ndulu Herbal Clinic kilichopo Mahenge na Bethlehemu Samaritan Clinic kilichopo Mfaranyaki Songea vinapima wagonjwa kwa kutumia kipimo cha Qantum Resonance Magnetic Analzer ambacho kimepigwa marufuku na Serikali.

Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dokta Gozibert alisema vituo vyote vya tiba asili viliandikiwa barua kutoka Manispaa ya Songea kuacha kutumia kipimo hicho, ambacho kinawarubuni wananchi kuwa wanaumwa magonjwa mengi wakati sivyo ndivyo hivyo kuwafanya walipe gharama kubwa kwa ajili ya matibabu ambazo ni kati ya shilingi 150,000 hadi 300,000.

Tuesday, November 14, 2017

WANAOTOA KIBALI CHA KUSAFIRISHA KAHAWA MBINGA WALALAMIKIWA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

VIONGOZI waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuondoa urasimu kwenye masuala yanayohusiana na biashara ya zao la kahawa ili mfanyabiashara anayeuza kahawa yake mnadani Moshi aweze kuiuza kwa wakati uliopangwa.

Hayo yalisemwa na Meneja uzalishaji wa Kampuni ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Mbinga (MCCCO), Injinia Rabiel Ulomi wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu huku akielezea namna wafanyabiashara wa zao hilo wanavyopata vikwazo pale wanapohitaji kupata kibali cha kusafirishia kahawa.

“Ni muhimu jambo hili viongozi wetu wa ngazi ya halmashauri zetu wakaondoa urasimu wa mambo fulani fulani, hasa wakati wa kutoa kibali cha kusafirishia kahawa kwa sababu tu ya sahihi ya mtu mmoja hili ni lazima tuliseme wazi linaharibu biashara ya kahawa”, alisema Ulomi.

VIONGOZI WATAKIWA KUSIMAMIA BEI YA PEMBEJEO ZA KILIMO

Na Mwandishi wetu,  
Songea.

MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Palolet Mgema amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali wilayani humo, kusimamia ipasavyo bei ya pembejeo za kilimo ili kuepusha ulaghai unaoweza kufanywa na baadhi ya mawakala ambao sio waaminifu waliopewa dhamana na Serikali kusambaza pembejeo hizo kwa wakulima katika kuelekea msimu huu wa kilimo.
Palolet Mgema.

Mgema alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipokuwa akitoa salamu za Serikali kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba huku akisisitiza kuwa wanaowajibu pia wa kusimamia hilo kuhakikisha mkulima anauziwa kwa bei iliyopangwa.

Alisisitiza kuwa endapo viongozi hao watapuuza na kuwaachia mawakala wafanye wanavyotaka, kuna uwezekano mkubwa kwa wakulima kuuziwa kwa gharama kubwa hatimaye kushindwa kumudu gharama husika na kusababisha baadhi yao kutozalisha mazao yao shambani.

KUKOSEKANA SOKO LA UHAKIKA WAKULIMA SONGEA WATELEKEZA MBAAZI MASHAMBANI

Zao la Mbaazi.
Na Muhidin Amri,      
Songea.

WAKULIMA wanaojishughulisha na kilimo cha zao la mbaazi katika kata ya Mgazini Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wametelekeza zao hilo mashambani baada ya kukosa soko la uhakika.

Kata ya Mgazini ni kati ya maeneo ambayo uzalishaji mkubwa wa mazao mbalimbali unafanyika ikiwemo zao hilo.

Msimu wa mwaka huu zao hilo limekumbwa na changamoto ya kukosa soko la uhakika jambo ambalo limewafanya baadhi ya wakulima waache kuvuna mashambani walikozalisha huku wengine wakisema hawaoni sababu ya kuendelea kupoteza nguvu zao.

CHANGAMOTO YA MAGUNIA ADUI WA MAENDELEO KIWANDA CHA KUKOBOA KAHAWA MBINGA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KAMPUNI ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa Wilayani Mbinga (MCCCO) mkoa wa Ruvuma, inalazimika kuwatumia wazabuni waliopo nje ya nchi kusambaza magunia ya kuhifadhia kahawa safi ambayo inakobolewa kiwandani hapo, kutokana na mzabuni aliyepewa kazi hiyo hapa nchini kushindwa kufanya kazi hiyo.

Aidha kufuatia hali hiyo, Serikali imeombwa kuruhusu wazalishaji wa magunia hayo wawe wengi ili kuweza kunusuru hali hiyo na kufanya kahawa inayokobolewa hivi sasa kiwandani hapo iweze kuhifadhiwa katika mazingira mazuri.

Injinia Rabiel Ulomi ambaye ni Meneja uzalishaji wa kiwanda hicho, alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza ofisini kwake na mwandishi wa habari hizi juu ya maendeleo ya uzalishaji wa zao la kahawa wilayani humo.

WANANCHI MWENGEMSHINDO SONGEA KULIPWA FIDIA

Meya wa Manispaa Songea, Abdul Hassan Mshaweji akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni mjini hapa, juu ya mikakati ya Serikali katika kuwaletea maendeleo ya wananchi.
Na Albano Midelo,   
Songea.

IMEELEZWA kuwa Serikali hapa nchini, imekubali kuwalipa fidia ya ardhi shilingi bilioni 3.3 wananchi wanaoishi katika kata ya Mwengemshindo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Aidha eneo ambalo hulipwa fidia ni lile lenye ukubwa wa ekari 5,000 lililochukuliwa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2008/2009 kwa ajili ya eneo maalum la Ukanda wa Uwekezaji Viwanda (EPZA).

Hayo yalisemwa na Meya wa Manispaa hiyo, Abdul Hassan Mshaweji wakati alipokuwa akitoa taarifa katika mkutano wa baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Songea lililoketi mjini hapa.

Thursday, November 9, 2017

DOKTA MAGUFULI ATENGUA UTEUZI MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI TUNDURU

Na Mwandishi Wetu,

RAIS Dokta John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Abdallah Mussa kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi wilayani humo.

Kutenguliwa kwa uteuzi wa Mkurugenzi huyo leo Alhamisi Novemba 9 mwaka huu kumefanyika siku tatu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa wakurugenzi wengine wawili.

Taarifa ya Rebecca Kwandu, Mkuu wa kitengo cha mawasiliano Serikalini katika Ofisi ya Tamisemi imesema kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ndiye aliyotoa taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi huo leo mjini Dodoma.

MAKAMU WA RAIS AFUNGA KILELE CHA MAADHIMISHO MTANDAO WA POLISI WANAWAKE TANZANIA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akikagua gwaride maalum la Polisi wanawake kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania yaliyofanyika kwenye chuo cha taaluma ya Polisi, Kurasini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipata maelezo juu ya umuhimu wa alama za barabarani kutoka kwa Koplo Faustina Ndunguru wa kitengo cha usalama barabarani makao makuu ya Polisi Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka kumi ya Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania yaliyofanyika kwenye chuo cha taaluma ya Polisi, Kurasini Dar es Salaam.

NEC YAENDELEA KUTEKELEZA ZOEZI LA USAMBAZAJI VIFAA VYA UCHAGUZI

Na Mwandishi wetu,

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba maandalizi ya vifaa kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa madiwani, unaofanyika katika kata 43 yamekamilika na awamu ya pili ya vifaa hivyo vitaanza kusafirishwa kesho Ijumaa kwenda katika kata husika.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC Kailima Ramadhani alisema kuwa vifaa vitakavyosafirishwa kuanzia kesho ni maalum kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa vituo, makarani waongozaji pamoja na  mfano wa karatasi za kupigia kura.

Ramadhani alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya kusafirisha vifaa hivyo ulifanywa na tume wakati wa mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi ambayo yalifanyika mjini Dodoma ambavyo vilitumika wakati wa uteuzi wa wagombea udiwani katika kata zote.

CHRISTINE MNDEME AWAPA SOMO MADIWANI MBINGA AWATAKA KUSIMAMIA MIRADI YA WANANCHI

Na Mwandishi wetu,     
Mbinga.

MADIWANI waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa wahakikishe kwamba wanasimamia ipasavyo maendeleo ya wananchi ili mwisho wa siku wananchi waliowachagua waendelee kuwa na imani nao.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa mkoa huo, Christine Mndeme wakati alipokuwa juzi katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa huku akiwataka Madiwani hao katika kata zao kufanya mikutano na wananchi ambayo inalenga kujadili masuala ya kimaendeleo.

“Ndugu zangu maana mkizembea kufanya hivi siku ya mwisho wa utawala wenu kule katani waliotuajiri hawatatuelewa tena”, alisema Mndeme.

Wednesday, November 8, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI AZUNGUMZA NA WANANCHI MISENYI NA KUTEMBELEA KIWANDA CHA SUKARI KAGERA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akizungumza na wanachi wa wilaya ya Misenyi (Hawapo pichani) wakati akielekea katika kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar kilichopo wilayani humo.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dokta John Pombe Magufuli akiandika wakati wananchi wa Misenyi walipokuwa wakiwasilisha kero zao mara baada ya kusimama wakati akiwa njiani kuelekea katika Kiwanda cha Sukari cha Kagera Sugar kilichopo wilayani humo.

UJENZI KITUO CHA AFYA KALEMBO UKAMILIKE KWA WAKATI ULIOPANGWA

Christine Mndeme ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akizungumza na wananchi wa kata ya Kihungu katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo, wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo aliwataka washiriki kikamilifu katika shughuli ya ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata hiyo ili ujenzi wake uweze kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christine Mndeme akishiriki juzi katika shughuli za ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani humo wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi ambapo ujenzi wa kituo hicho unagharimu shilingi milioni 500.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

AGIZO limetolewa kuwa fisadi au mwizi yeyote atakayejitokeza kuiba sehemu ya fedha shilingi milioni 500 ambazo zimetolewa na Serikali, kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Kalembo kilichopo katika kata ya Kihungu Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, haraka achukuliwe hatua za kisheria asionewe huruma.

Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme alitoa agizo hilo juzi akimtaka Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha hizo ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa, wakati alipokuwa ametembelea eneo la ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa lengo la kujionea ujenzi ambao unaendelea kufanyika huko.

Alisema kuwa fedha hizo ambazo zimetolewa na Serikali ya awamu ya tano zinalenga kuboresha huduma ya afya katika kata hiyo ili wananchi wanaoishi huko waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa kilometa 35 kwenda hospitali ya wilaya kutafuta matibabu pale wanapougua.