Monday, November 27, 2017

CCM RUVUMA YAIBUKA KIDEDEA UCHAGUZI NAFASI YA UDIWANI




Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimeibuka kidedea kwa kuwa mshindi katika chaguzi za nafasi ya udiwani zilizofanyika mkoani humo baada ya wagombea wake kushinda kwa kura nyingi.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini hapa Katibu wa CCM mkoani humo, Amina Imbo alisema kuwa uchaguzi huo uliofanyika ulirudiwa baada ya wagombea wake kufariki dunia.

Imbo alisema kuwa katika mkoa huo kata ambazo uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika ni kata ya Mhongozi iliyopo wilayani Mbinga, Lukumbule na Kalulu zilizopo wilayani Tunduru mkoani hapa.

Katibu huyo alifafanua kuwa katika kata hizo vyama ambayo vilishiriki uchaguzi huo na kuweka wagombea wake ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo na Chama Cha Wananchi (CUF).

Alisema kuwa CCM katika kata ya Mhongozi wilayani Mbinga ilimsimamisha mgombea wake, Florian komba aliyepata kura 749, CHADEMA alikuwa Joseph Mahua alipata kura 284 na CUF Pasience Ndimbo kwa kura 15.

Vilevile katika wilaya ya Tunduru kata ya Lukumbule alikuwa Milepa Makande (CCM) alipata kura 1572, Omary Ghaibu (CUF) kura 1351, Nassoro Mkopoto (CHADEMA) kura 234 na Sian Mbwana (ACT) aliyepata kura 12.

Katika kata ya Kalulu wilayani humo Rabii Makunga (CCM) kura 706, Kauga Hassan (CHADEMA) alipata kura 56 na Kwali Ally (CUF) ambaye naye alipata kura 518.

Pamoja na mambo mengine, chaguzi hizo zilifanyika baada ya kuanza mchakato wake Oktoba 15 mwaka huu na kufikia hitimisho Novemba 26 mwaka huu.

No comments: