Wednesday, November 8, 2017

RC RUVUMA AWAONYA WATUMISHI WA SERIKALI UFISADI MAJUNGU NA FITINA ACHUKIZWA NAO

Aliyesimama ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme akizungumza juzi na baadhi ya watumishi wa Halmashauri ya mji wa Mbinga na wilaya ya Mbinga pamoja na Madiwani wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mndeme amesema kuwa mtumishi yeyote ambaye amekuwa na mazoea ya kufanya kazi kwa mfumo wa ufisadi, majungu na fitina katika utawala wake mkoani humo hana nafasi tena badala yake atafute sehemu nyingine ya kwenda kufanyia kazi.

Kadhalika amewataka watumishi hao wasifanye kazi kwa mazoea bali wanapaswa kuwa wazalendo zaidi katika kazi, ikiwemo kuonesha uhalali wao wa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dokta John Pombe Magufuli katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya wananchi.

Mndeme alisema hayo juzi wakati alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, akizungumza na baadhi ya watumishi wa Serikali wa kada mbalimbali pamoja na Madiwani mjini hapa. 


“Kila mtu katika kazi yake ajitambue kuwa ni muhimu katika jamii, ndugu zangu wafanyakazi wa Mbinga ninachowataka kuwaambia hapa ondokeni na kufanya kazi kwa mazoea”, alisisitiza.

Alisema kuwa hapendi kuona matumizi ya fedha za Serikali yanakwenda ovyo hivyo amewataka watumie fedha vizuri kwa kufuata miongozo iliyowekwa katika shughuli yenye tija kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mkuu huyo wa mkoa alibainisha kuwa semina na posho kwa safari ambazo hazina umuhimu hataki kusikia badala yake wanapaswa kubana matumizi.

“Viongozi mliopewa dhamana acheni kukaa maofisini muda mwingi utumieni kuwa karibu na wananchi kule vijijini kusikiliza kero zao na kuzitekeleza kwa wakati”, alisema Mndeme.

Vilevile aliwashutumu maafisa utumishi kuwa mara nyingi wamekuwa hawaendi vijijini kuonana na viongozi wa ngazi ya vijiji na kata katika kutatua matatizo mbalimbali, badala yake hivi sasa amewataka waende huko kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.


Pamoja na mambo mengine, alikemea pia tabia ya uchomaji moto misitu huku akiwataka maafisa misitu ambao ndiyo wamepewa dhamana ya kusimamia hilo wahakikishe wanazuia shughuli za uharibifu wa mazingira, ikiwemo katika vyanzo vya maji ambapo alisisitiza wasiwe na huruma pale wanapomkamata mtuhumiwa haraka wamfikishe kwenye vyombo vya kisheria ikiwemo Mahakamani.

No comments: