Monday, November 20, 2017

WANAFUNZI RUHUWIKO SEKONDARI SONGEA WATAKIWA KUEPUKA ANASA

Na Muhidin Amri,    
Songea.

WANAFUNZI wa shule ya Sekondari Ruhuwiko mkoani Ruvuma inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Brigedi ya 401 Tembo Kanda ya kusini, wametakiwa kusoma kwa bidii na kuzingatia masomo yao darasani ili waweze kutimiza ndoto ya kuwa viongozi bora watakao weza kulitumikia taifa hili.

Hayo yalisemwa  mwishoni mwa wiki na Mkuu wa mafunzo na utawala wa Brigedi hiyo Kanal John Mwaipaya wakati akizungumza na wananchi, walimu na wazazi katika mahafali ya 22 ya kidato cha nne shuleni hapo.

Aidha alisema kuwa lazima mwanafunzi atambue kwamba analo jukumu la kusoma kwa kujituma ili aweze kufanya vizuri katika mitihani yake ya mwisho jambo ambalo litamsaidia kuwa na uhakika wa ajira na  uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha ya kila siku.

Pia Kanal Mwaipaya aliwataka wanafunzi wa shule hiyo hasa watoto wa kike kujiheshimu na kujaribu kuzuia tamaa za miili yao kwa kujiepusha na vitendo vya anasa ambavyo vinachangia kuwa katika hatari ya kupata mimba na ugonjwa wa ukimwi.

Meneja wa shule hiyo, Luten Kanal Kassian Chausi aliwataka wazazi na walezi kuwa andaa vyema watoto wao kwa kuwapeleka shule kwa muda muafaka ili hapo baadaye waweze kuwa na sifa bora hata ya kujiunga na vikosi  vya ulinzi na usalama Jeshini.

Kwa mujibu wa  Chausi alieleza kuwa jamii lazima itambue kuwa zama hizi sio za ujanja ujanja na kubebana bali kila mmoja ataishi kwa kufanya kazi halali  itakayompatia  kipato cha kila siku badala ya kuendelea kuishi kwa mazoea.

Alitolea mfano, hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa imetangaza nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa vijana na kuweka vigezo, hata hivyo katika hali ya kusikitisha bado vijana wengi wa mkoa  wa Ruvuma waliojitokeza  kuomba nafasi hizo walikosa sifa na nafasi kuchukuliwa na vijana kutoka nje ya mkoa.

Sambamba na hilo amewaonya pia vijana hao kuacha kuishi maisha ya  sterehe badala yake wahakikishe wanatumia muda wao kusoma kwa bidii ili kujiandaa na maisha yao ya baadaye kwani maisha ya uraiani ni magumu tofauti na vile wanavyofikiria.

No comments: