Wednesday, November 22, 2017

WASIMAMIZI UCHAGUZI MDOGO VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUFUATA TARATIBU

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage upande wa kulia akisisitiza jambo wakati akizungumza na Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Moshi hivi karibuni, kushoto kwake ni Mwanasheria mwandamizi wa NEC, Mtibora Seleman.
Na Clarence Nanyaro – NEC 

MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Semistocles Kaijage amewataka Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi hapa nchini, kuwashirikisha viongozi wa vyama vya siasa katika maamuzi mbalimbali wanayofanya yenye maslahi kwa pande zote ili kuendeleza amani na utulivu tulionao.

Akizungumza na Wasimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Moshi, Jaji Kaijage alisema kuwa katika kipindi hiki ambacho vyama vya siasa vinashiriki kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani ambao utafanyika Novemba 26 mwaka huu, ni muhimu kwa wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha kuwa maadili ya uchaguzi wakati wa kampeni yanazingatiwa ili kuepusha uvunjifu wa amani miongoni mwa wananchi.

Jaji Kaijage ambaye yuko katika ziara ya kutembelea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kushuhudia utekelezaji wa maadili hayo katika kampeni za uchaguzi huo.
 
Amewataka wasimamizi kuhakikisha kuwa vifaa vyote ambavyo vinahitajika ili uchaguzi uweze kufanyika viwe vimepatikana na vile ambavyo havijapatikana wa wasiliane na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kasoro zinazobainika ziweze kupatiwa ufumbuzi mapema kabla ya siku ya uchaguzi kuwadia.

Kadhalika alitoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi huo kuhakikisha kuwa siku ya upigaji kura ulinzi unaimarishwa katika vituo vya kupigia kura, lakini usiwe ulinzi wa kuwatia wananchi hofu wakashindwa kufika katika vituo vya kupigia kura kuchagua viongozi wanaowataka ili waweze kushirikiana nao katika kujiletea maendeleo.

No comments: