Thursday, January 1, 2015

MAKAHABA WATIKISA MANISPAA YA SONGEA, WAITAKA SERIKALI KUCHUKUA HATUA



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WANANCHI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameshtushwa na kuwepo kwa wimbi la wasichana kutoka nje ya wilaya hiyo, wanaofika na kufanya vitendo vya ukahaba katika mitaa mbalimbali  nyakati za usiku huku wengine  wakicheza muziki wakiwa nusu uchi kwenye nyumba za starehe maarufu  kwa jina la Kangamoko, jambo linalohofiwa kuongezeka kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi.

Ilielezwa kuwa kundi hilo la makahaba linadaiwa kutoka mikoa ya Mbeya, Tanga, Dar es Salaam na miji mingine mikubwa wamekuja Songea kwa ajili ya kufanya biashara hiyo ya ukahaba, ambapo ikifika majira ya saa tatu usiku wamekuwa wakijipanga katika mitaa mbalimbali kutafuta wanaume.

Makahaba hao ambao wanalalamikiwa wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 18 hadi 30 ambao wamekuwa wakifanya shughuli hiyo isiyo rasmi hasa katika mitaa maarufu ya Delux, Serengeti, Majimaji na barabara ya Sokoine, huvaa nguo fupi na nyingine zinazoonesha maumbile ya miili yao kwa lengo la kutaka kuwavutia wanaume, ambao hujikuta wakiingia mtegoni bila kutarajia kutokana na ushawishi unaofanywa na wasichana hao.


Wananchi hao walisema kuwa tabia inayofanywa na wasichana hao haipaswi kufumbiwa macho, kwani licha ya kumdhahalilisha mwanamke lakini pia inachangia maambukizi mapya ya ukimwi wakati serikali na wadau wengine wapo katika mapambano ya kuzuia maambukizi mapya ambapo jamii imekuwa ikiaswa kuunga mkono jitihada hizo kwa kuepuka vishawishi mbalimbali.

Aidha wameliomba Jeshi la polisi wilaya ya Songea, kuangalia uwezekano wa kufanya msako mkali wa kushitukiza mara kwa mara katika mitaa hiyo ili kuwakamata watu hao, kwani iwapo wataachwa kuendelea vitendo hivyo viovu, kuna uwezekano mkubwa wa kuhatarisha jamii kuingia katika majanga ambayo yatasababisha hata kudumaza shghuli za kimaendeleo.

Naye Siwajibu Athuman (34) mkazi wa Mjimwema alisema, mwanamke kucheza muziki au ngoma yoyote akiwa nusu uchi ni fedheha  na uzalilishaji, sio kwa yule tu anayeendekeza vitendo hivyo bali ni kwa wanawake wote na kwamba aliitaka jamii kuungana katika kukomesha tabia hiyo ambayo imeshanza kuota mizizi katika Manispaa ya Songea.

Hata hivyo msichana mmoja aliyefahamika kwa jina la Paulina mkazi wa Majengo  mjini hapa, aliiomba jamii kuacha kushabikia na kufurahia vitendo  hivyo, kwani licha ya kumdhalilisha mwanamke pia ni kwenda kinyume na maagizo ya Mungu ambayo yanakataza tabia na matendo machafu.

No comments: