Sunday, January 25, 2015

AKUTWA AMEJINYONGA KATIKA MAHABUSU YA KITUO KIKUU CHA POLISI MBINGA

Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

MTUHUMIWA ambaye alikuwa akishikiliwa katika Kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Bosco Ndunguru (40) amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shati ambalo alikuwa amelivaa, wakati alipokuwa kwenye mahabusu ya kituo hicho cha polisi wilayani humo.

Ndunguru aliwekwa mahabusu, kwa tuhuma ya kuvunja jengo la polisi na kuiba Radio call ya kituo hicho mwaka jana, ambapo alitoroka kusikojulikana na Jeshi hilo lilikuwa likimtafuta kwa muda mrefu.

Taarifa zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea Januari 23 mwaka huu majira ya asubuhi, ambapo baada ya kukamatwa na kuswekwa rumande ilikuwa afikishwe Mahakamani kwa ajili ya kujibu tuhuma, ambazo zilikuwa zinamkabili.

Imedaiwa kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kuingizwa mahabusu, muda mwingi alikuwa akilia na kulalamika sana, huku akidai kuwa ndugu zake hawampendi.


Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema mara baada ya askari waliokuwa zamu kumaliza muda wao na kuingia wengine na kabla ya kutoka kazini, askari hao walikabidhiana kituo pamoja na mali zilizopo kituoni hapo ambapo mtuhumiwa huyo pamoja na watuhumiwa wengine watatu wenye makosa tofauti wakiwa katika mahabusu hiyo, ndipo Bosco alitumia muda huo kutoka na kujifanya akielekea chooni na kuingia chumba kilichopo jirani na mahabusu ambacho kilikuwa hakina mtu na kuchukua uamuzi wa kujitundika kwa kutumia shati hilo ambalo alikuwa amevaa.

Alisema aliweza kufanikisha tendo hilo la kujitundika kwenye nondo ya mlango wa chumba hicho, mpaka alipogunduliwa na mmoja kati ya watuhumiwa waliokuwepo ndani na kutoa taarifa kwa askari waliokuwa zamu, siku ya pili Januari 24 mwaka huu majira ya saa moja asubuhi.

Kamanda huyo aliongeza kuwa mwili wa marehemu huyo, ulifanyiwa uchunguzi na mganga kutoka hospitali ya wilaya ya Mbinga, ambapo baada ya kukamilisha kazi hiyo ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

No comments: