Thursday, January 8, 2015

MWANDISHI WA HABARI JINO KWA JINO NA GAUDENCE KAYOMBO, UCHAGUZI MKUU MWAKA HUU

Humphrey Kisika.
Na Kassian Nyandindi,


Mbinga.

KWA vyovyote iwavyo, mapigo ya moyo ya Mbunge wa Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, Gaudence Kayombo yataongezeka mara dufu baada ya kijana msomi ambaye ni Afisa Habari wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Humphrey Kisika (32) kutangaza nia ya kuwania ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
 
Kisika ambaye ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya uandishi wa habari, pia ni mwanafunzi wa chuo Kikuu cha Iringa, anayesoma shahada ya pili ya uandishi wa habari na utawala, anataka kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza na wanahabari kijijini kwake Ukata wilayani Mbinga, alisema anataka kupokea kijiti toka kwa Mbunge huyo wa sasa, ili atumie maarifa aliyonayo kusukuma zaidi maendeleo ya jimbo hilo.

Alisema anautambua na kuuthamini mchango wa mbunge wa sasa katika kusukuma maendeleo ya jimbo hilo, lakini kuna haja akampokea kijiti hicho ili aongeze kasi yake.


“Kipaumbele changu kitakuwa maendeleo kwanza yatakayoshirikisha makundi yote ya jamii likiwemo kundi muhimu sana la vijana, yatakayonufaisha wote,” alisema.

Alisema endapo nia yake hiyo itatimia, atahakikisha anaondoa pengo linalodumaza maendeleo baina ya wataalamu ambao ni watendaji wa shughuli mbalimbali za serikali, na wanachi ambao ni wapiga kura.

“Kumekuwepo na manung’uniko toka kwa wananchi, lakini kimsingi manung’uniko hayo yanachangiwa na baadhi ya watendaji ambao kwa maslahi yao binafsi au kwasababu ya kufanya kazi kwa mazoea, wanashindwa kuutumikia vyema umma wa watanzania”, alisema.

Alisema CCM ina sera nzuri, huenda kuliko chama kingine kile cha siasa ambazo hata hivyo yawezekana katika baadhi ya maeneo zimeshindwa kutekelezwa ipasavyo, kwasababu ya uzembe wa wataalamu hao.

Akizungumzia muonekano wa kundi kubwa la vijana kuonekana wakishabikia zaidi vyama vya upinzani kuliko chama chake cha CCM, Kisika alisema katika mazingira ambayo nchi ina demokrasia ya hali ya juu kama Tanzania, ni lazima wawepo vijana wanaopenda vyama vya upinzani.

Aidha alisema hiyo haina maana kwamba vijana wote wanavipenda vyama vya upinzani, kwani chama cha mapinduzi inao vijana wengi na ndio maana Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) upo imara kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa.

“Ombi langu kwa vijana wenzangu, ni muhimu katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa kisiasa, tukafanya siasa kwa misingi ya upendo na amani, tusikubali kutumiwa kwenye harakati za siasa chafu zitakazohatarisha amani ya nchi hii ili iendelee kuwa kisiwa cha amani,” alisisitiza

Endapo ndoto yake hiyo itatimia, Kisika alisema wanambinga wategemee maendeleo ya pamoja yatakayoletwa kupitia nguvu ya pamoja.

No comments: