Tuesday, January 20, 2015

DIAMOND PLATINUM KUTUMBUIZA SHEREHE ZA CCM KITAIFA MKOANI RUVUMA

Nassib Abdul, maarufu Diamond Platinum

Na Mwandishi wetu,
Songea.

MKOA wa Ruvuma, umepata heshima kubwa ya kuandaa sherehe za kutimiza miaka 38 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitaifa mwaka huu.

Mbunge wa Songea Mjini Dokta Emmanuel Nchimbi ameanza kuratibu sherehe hizo ambazo zitafanyika mkoani humo, na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete. 

Dokta Nchimbi alisema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari mjini hapa, ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni; Umoja ni Ushindi, Katiba yetu nchi yetu.

Mbunge huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi, alisema kila kitu kimekamilika juu ya maandalizi ya sherehe hizo ambazo zitafanyika Februari Mosi mwaka huu, badala ya Februari tano kama ilivyozoeleka. 


“Februari tano ni siku ya kazi, sasa tusiharibu utaratibu wa watu, tumeona tuiweke tarehe hii katika kuadhimisha sherehe hizi za chama cha mapinduzi” alisema.

Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuwapa fursa wananchi wengi ili waweze kushiriki, siku hiyo ambayo itakuwa siku ya Jumapili.

Maandalizi ya vijana wa halaiki, uwanja na vikundi mbalimbali vya ngoma yanaendelea, vijana wa bendi kutoka Zanzibar wameshawasili na wanaendelea na mazoezi, bendi yetu ya Tanzania One Theatre (TOT) nayo itatumbuiza.

Kadhalika watakuwapo wasanii mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platinum.

Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho alisema chama hicho kimeendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilani inavyoelekeza kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

“Tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu huku barabara nyingi zimejengwa kwa kiwango cha lami ikilinganishwa na miaka iliyopita,” alisema Mwisho.

No comments: