Monday, January 19, 2015

KATIBU WA MADIWANI NA BAADHI YA VIGOGO MBINGA, WADAIWA KUSUKA MPANGO MCHAFU WA KUVUNJA KAMATI YA MIPANGO NA FEDHA

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

ULE mpango wa kutaka kuvunjwa kwa Kamati ya mipango na fedha katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, mapya yameendelea kuibuka ambapo imeelezwa kwamba, ni mpango ambao umesukwa na vigogo wachache wa wilaya hiyo huku Madiwani wake wakiendelea kulalamika kutoshirikishwa juu ya suala hilo. Mtandao huu unaripoti.

Taarifa za uhakika zilizotufikia leo zinaarifu kuwa, mkakati huo wa kuvunja kamati hiyo huenda ukagonga mwamba kufuatia baadhi ya Madiwani kuja juu na kueleza kwamba Katibu wao wa baraza la madiwani, Adolph Mandele ambaye naye ni diwani wa kata ya Mpapa, ndiye anayewachanganya na kuwauza wenzake, akidaiwa kutumiwa na vigogo hao (majina tunayo) kusuka mipango mibaya kwa lengo la kuhakikisha vigogo hao wanafanikisha jambo hilo.

Mandele analalamikiwa kutengeneza muhtasari hewa ambao unaonyesha kwamba wajumbe wa baraza hilo kwa maana ya madiwani wenzake, walikutana pamoja na kuketi kupitia kikao cha dharula (CCM) na kukubaliana kufanya hivyo jambo ambalo, madiwani wenzake wanamshangaa na kuanza kumjia juu wakisema sio kweli anadanganya.

Wengi wanapinga vikali kuhusika katika kufanya kikao hicho, ambapo Mandele alipofanya mahojiano na mwandishi wetu alithibitisha kwa kauli yake akisema kikao hicho kilifanyika Desemba Mosi mwaka huu, katika ofisi za makao makuu ya CCM wilayani Mbinga na madiwani hao walikubaliana juu ya kuvunjwa kwa kamati hiyo.


“Jambo hili madiwani tulikwisha kaa kikao cha dharula na mahudhurio niliyonayo pale ofisini tulikuwa madiwani 28, na mimi nimekwisha andika muhtasari nimepeleka kwa mkurugenzi wetu kwa hatua zaidi”, alisema Mandele.

Madiwani hao walisema baada ya kubaini hilo hata viongozi wa chama hicho wilayani humo, wanaelezwa kumuuliza ni nani aliyemtuma kufanya hivyo badala yake alishindwa kuweka bayana jambo hilo, na kuishia akisema kuwa yeye alitumwa afanye hivyo na kuonekana dhahiri kuwa suala hilo linapikwa bila kufuata taratibu kitendo ambacho kimefafanuliwa kuwa, kiongozi anayetumika kwa mtindo huu kwa lengo la kuwasaliti au kuwavuruga wenzake ni hatari katika jamii.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi, umebaini kwamba mchezo huo mchafu ni mpango ambao umesukwa na baadhi ya vigogo wa wilaya hiyo (majina tunayo) ambao mnamo Januari 15 mwaka huu, walikutana pamoja nyumbani kwa kigogo mwenzao (jina tunalo) na kuweka mikakati hiyo namna ya kuvunja kamati hiyo kwa lengo la matakwa yao binafsi.

“Sisi tunamshangaa sana huyu Katibu wetu kufikia hatua ya kutaka kutusaliti wanachama wenzake wa CCM (madiwani), anafikia hatua ya kutengeneza taarifa hewa na kupeleka kwa mkurugenzi mtendaji kwamba tumekubaliana kuvunja Kamati ya mipango na fedha wakati jambo hili halina ukweli, hafai kuwa kiongozi huyu ni muuaji”, walisema.

Awali Mkurugenzi mtendaji wa wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga alishutumiwa na madiwani wake kwamba, mpango huo wa kutaka kuvunja kamati hiyo amekuwa akiufanya chini kwa chini na tayari suala hilo, limefikishwa mezani kwake kwa utekelezaji, katika kikao cha baraza la madiwani kinachotarajiwa kuketi Januari 23 mwaka huu, wilayani humo kama alivyothibitisha Katibu huyo wa madiwani.

Jambo hilo limethibitishwa pale mkurugenzi huyo alipovunja ratiba za vikao vya kamati husika, ambapo hata baraza hilo ilibidi liketi mwishoni mwa mwezi huu na sio tarehe hiyo, ambapo madiwani wake wameshangazwa kupangiwa tarehe hiyo kufanya kikao cha baraza kinyume na ratiba husika inavyotaka.

Malalamiko hayo yametolewa na kufafanuliwa kuwa hakuna kikao ambacho madiwani hao walikaa na kukubaliana kuvunjwa kwa kamati hiyo, ambayo ndio mhimili wa kamati zote za baraza la madiwani.

Walisema kitendo hicho kinachofanywa, ni mpango mchafu ambao haupaswi kuigwa katika jamii, na hili mkurugenzi huyo analifanya akidaiwa kutokana na  wajumbe wachache waliomo ndani ya kamati hiyo ya mipango na fedha, kuwa mwiba kwake na kutotaka kuburuzwa wakati wa kupitisha mambo mbalimbali ya kimaendeleo ya wilaya hiyo, kinyume na taratibu husika.

“Leo anapotaka kuvunja kamati hii maana yake ikishavunjwa, kamati zote tulizonazo ndani ya baraza hili itabidi ziundwe nyingine upya, sisi tunashangaa sana hatuja kaa kikao chochote kama madiwani na kukubaliana kupitisha maamuzi haya”, walisema.

Kadhalika waliongeza kuwa kuvunjwa kwa kamati hiyo, huenda kanuni husika za baraza la madiwani hazitaruhusu kufanya hivyo kutokana na kile walichoeleza kuwa baraza hilo linaelekea mwishoni kuvunjwa, tayari kuelekea uchaguzi mkuu ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Mbinga, Ngaga wamemtaka kuwa makini katika hili na azingatie kanuni husika, na endapo kama zinamruhusu kufanya hivyo kabla ya yote ni muhimu akashirikisha kwanza madiwani wake, kupitia vikao halali kabla ya kuleta maamuzi katika kikao cha baraza la madiwani.

No comments: