Thursday, January 8, 2015

JESHI LA POLISI RUVUMA LABAINI MTANDAO WA KIGAIDI



Na Mwandishi wetu,
Songea.

JESHI la polisi mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na  vyombo vingine vya ulinzi na usalama limefanikiwa kukitambua  kikundi cha mtandao wa kigaidi  ambacho kinadaiwa kujihusisha na  majaribio matatu, ya  kuwashambulia  askari polisi wakiwemo wa kikosi cha usalama barabarani  na tayari linawashikilia watuhumiwa  kadhaa ambao majina yao yamehifadhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa,  Kamanda wa Polisi wa mkoa huo Mihayo Msikhela alisema kuwa Jeshi la polisi limefanikiwa kumtambua mtuhumiwa aliyelipukiwa na bomu hivi karibuni,  pamoja na mtandao wote unaojihusisha na matukio matatu ya  kigaidi ya ulipuaji mabomu, yaliyolenga kuwashambulia askari hao.

Alisema marehemu huyo jina lake limehifadhiwa, ambapo imebainika kuwa ni mzaliwa wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, ambaye alizikwa  Desemba 31 mwaka jana baada ya Baba yake mzazi kujitokeza  na kuchukua mwili wa mtoto wake na kwenda kuuzika.


Alisema Marehemu huyo alikuwa ni miongoni mwa watuhumiwa  wa kikundi cha kigaidi ambapo tukio la kwanza wanatuhumiwa kuwarushia askari polisi waliokuwa doria  kwa bomu lilotengenezwa kienyeji Septemba 16 mwaka jana katika eneo la Mabatini mjini hapa.

Tukio la pili lilitokea Oktoba 27 mwaka jana ambapo askari wa kikosi cha usalama barabarani wakiwa katika eneo la Mshangano, walilopangiwa kukagua magari  walitegeshewa bomu ambalo baadaye liligunduliwa na askari hao na kufanikiwa kuteguliwa kwa kushirikiana na Jeshi la wananchi, na kwamba tukio la tatu lilitokea Desemba 25 mwaka jana wakati askari hao wakiwa doria katika eneo la mtaa wa Majengo.

Alifafanua kuwa, katika matukio mawili  yaliyotokea  Mabatini na Majengo askari wanne walijeruhiwa  kwa mabomu hayo  mpaka sasa jeshi la polisi linawashikilia watuhumiwa kadhaa, na wengine wanaendelea kusakwa ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

“Jeshi  la polisi limejipanga vizuri kuhakikisha linawapata washiriki wote wa mtandao huu wa kigaidi waliokuwa wakishirikiana na marehemu, ili kuweza kutokomeza  wimbi hili la uhalifu  katika mkoa wetu wa Ruvuma na maeneo mengine ya nchi yetu, pia tunawaomba wananchi waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kuufichua mtandao huu”, alisema Mihayo.

No comments: