Saturday, January 24, 2015

VIONGOZI WACHAGULIWE KWA RIDHAA YA WANANCHI

Padre Baptiste Mapunda.

Na Padre Baptiste Mapunda,

SERIKALI iliyopo madarakani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) bado tumeshuhudia vituko vya hapa na pale, katika ulingo huu wa kisiasa huku ikijigamba ndiyo inayoendesha mambo yake kwa kutumia demokrasia, na utawala bora.

La hasha, mfano mzuri ni ule katika kipindi cha kampeni, upigajikura na utangazaji matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umefanyika hivi karibuni Desemba 14 mwaka jana, CCM kilionekana kufanya rafu kwa wapinzani wao wa kisiasa, ili kujihakikishia kinapata ushindi. 

Chama hiki tawala kilionekana kutumia mbinu nyingi, kama vile kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kwa namna moja au nyingine ikiwemo hata wakati mwingine, kutumia vyombo vya dola kama polisi ikiwa ni mbinu tu ya kutafuta ushindi.

Aidha baadhi ya matokeo katika vituo vya kupigia malalamiko yalijitokeza kwamba yalibatilishwa, na sio hilo tu bali hata pale yalipokuwa wazi kwamba wapinzani wameshinda  bado CCM haikukubali bali ulikuwa ni mwendo tu wa kulazimisha ushindi, kitu ambacho siasa za namna hii zinaweza kuiingiza jamii katika vurugu au machafuko kama yaliyotokea kule Kenya na sehemu nyinginezo.

Mbaya zaidi ni kile kitu cha kuwaapisha wagombea wengine ambao walikuwa wameshindwa kupata kura za kutosha na wananchi wakibaki wanalalamikia, jambo ambalo dhahiri linaonesha wazi kuwa bado ile dhana ya demokrasia huru ikiendelea kuminywa, kila kukicha hasa nyakati za chaguzi mbalimbali.

Watanzania wengi hivi sasa walio na akili timamu na wapenda amani, demokrasia na maendeleo wanachoshwa na vitendo hivi, ambavyo tunaweza tukaviita ni “uhuni uliopindukia.”

Mimi najiuliza hivi kweli Chama Cha Mapinduzi, ni siku gani kinaweza kushinda uchaguzi bila ghiliba, fitina, chuki, mizengwe, rushwa ya kura, uchakachuaji matokeo au utumiaji wa nguvu ya vyombo vya dola?

Wahenga husema; siku za mwizi ni arobaini, maana yake ni siku hiyo anayoshikwa hata kama itakuwa ya kumi na saba. Sasa naona mwisho wa kutawala kwa chama hiki unakaribia, kwani ile propaganda yao ya “ushindi wa kishindo” imeanza kujulikana  walikuwa wana maanisha nini?

Lakini pia kwa upande wangu siwezi kushangaa  vituko hivyo vya mwaka, kwa sababu hii yote ni alama ya kufilisika kimawazo na sera.

Mimi nakumbuka kama mchezaji wa mpira wa mguu mara nyingi timu yetu  tukiona inaelekea kushindwa na muda unapita, sasa kinachobaki ni kukata mtama kila mpinzani wetu anayekaribia goli letu. Yaani hapo sasa ni “mchezo wa bora liende” ni upiga juu, piga nje basi kwa maana sasa hakuna matumaini tena ya kushinda. 

Basi naona ndivyo na yalivyo mambo ndani ya CCM kwa sasa, alama za wananchi kuamka na kujua wanachotaka zimeonekana kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa. “Nyota ya asubuhi imewaangazia wananchi maskini wa Tanzania.” Mungu naye yupo upande wa maskini na wanyonge, basi ameamua kuwatia nguvu  watu wake akiwatuliza kwamba, “mimi ni Mungu wenu, msiogope, nitawakomboa tu.”

Wanaccm wenye upeo wameona upepo umebadilika ila wanaogopa kuwatonya na wenzao kwa sababu walio wengi, bado hawakubali kama watanzania wa leo wamebadilika. Walio wengi wanaendelea kujidanganya kwamba mtanzania bado mjinga, mpumbavu, zezeta na waoga wa kudai haki zao, zama za kufikiri  haya umepita.

Ndiyo maana nionavyo mimi, wanaona wanaweza tu kuapisha “wagombea wao walioshindwa” na kuendelea kutawala au kuongoza  wakisahau kwamba uchaguzi ndiyo msingi wa upatikanaji wa viongozi bora katika jamii kidemokrasia. Ni makosa kuwachagulia wananchi viongozi na mbaya zaidi kuwalazimisha wananchi kuongozwa na viongozi ambao siyo ridhaa yao.

Lakini kwa upande mwingine, mimi naona ni mojawapo sehemu ya “mnara wa Babeli” na pia ni utabiri wa Askofu mkuu Zakary Kakobe wa kanisa la Kipentekoste Full Gospel, itakumbukwa kwamba mwezi marchi 2013 Askofu huyo alitabiri kusambaratika kwa serikali ya chama hiki tawala, mithili ya mnara wa Babeli.

Kakobe akiwa ni mtumishi wa Mungu, mimi siwezi kumdharau kwani Mungu ana njia zake za kufikisha ujumbe kwake tofauti na tunavyofikiria sisi wanadamu. Unapoona jinsi makundi yanavyojipamba au kupasuana, wakati wa kuteua mgombea wa urais basi unaweza kutambua maana ya utabiri ule wa Askofu Kakobe.

Utabiri wa Askofu mkuu Kakobe, ulikuwa ukisema msambaratiko ndani ya CCM utatokea hatua kwa hatua na hili tunaendelea kuliona kila kukicha. Yesu aliwaambia wasikilizaji wake kwamba, utawala uliogawanyika haufai, kama uongozi umegawanyika basi utawezaje kuwaunganisha wananchi?

Ndani ya Chama cha mapinduzi hivi sasa kuna makundi kibao, na kila kundi likijigamba kuwa na mgombea wao ambaye  wanataka apeperushe bendera wakati wa kampeni mwezi Oktoba, tamaa ya urais imekuwa ni kubwa mno. 

Enzi za Mwalimu Julius Nyerere, nakumbuka kwamba ilikuwa mtu kujitangaza tangaza magazetini, katika luninga, radio na katika majukwaa ya kisiasa na wengine hata kwenda  katika nyumba za ibada isingewezekana. Kiongozi wa kweli anapendekezwa na wananchi na siyo kujipendekeza. Hakuna mtu anayeweza kujifanya mwenyewe kama kiongozi wa watu, bali anachaguliwa na watu wanaomuona anafaa kuwaongoza.

Hata hivyo kutokana na minyukano ya makundi hayo ndani ya chama hicho, kila kundi linajitahidi kujipigia debe na kuwaponda wenzao kwa kadiri liwezavyo na sasa hata kuna baadhi ya wazee, maarufu ndani ya chama kama Mheshimiwa Kingunge aliyejitokeza na kusema kwamba, wote waliotangaza kuwania urais hakuna mwenye sifa hata mmoja.

Inawezekana kabisa mzee Kingunge yupo sahihi, sasa kama hakuna hata mmoja bado watanzania  mzee wetu ametusaidia kutoa elimu ya urais, naiona  kauli yam zee huyu ni ya kinabii na ya kimapinduzi kuelekea uchaguzi mkuu, Oktoba mwaka huu.

Maovu yanayoendelea kujitokeza katika siasa kuelekea uchaguzi mkuu hakika mimi nasema yatupasa tubadilike na kuyaacha ikiwemo hata yale ya kihuni, kiharamia, kijasusi na ya kijambazi ndiyo maana nathubutu kwa kutumia safu hii kuwaelimisha watanzania wenzangu; Mungu atuepushe na maovu kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa barua pepe; frmapunda91@gmail.com

No comments: