Saturday, February 9, 2013

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUTOA MIMBA


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MHUDUMU wa kuuza vinjwaji katika baa ya Tunduru Pub mjini hapa, aliyefahamika kwa majina ya  Mary Baby Obodo amefariki dunia wakati akijaribu kutoa mimba kwa njia za kienyeji.

Binti huyo ambaye alianza kufanya kazi hiyo mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka jana katika baa hiyo, inadaiwa kuwa alifanya jaribio hilo la kutoa mimba wakati akiwa katika nyumba ya kulala wageni ya iitwayo New Sety View ambako alikuwa akiishi tangu afike mjini hapa.

Wakizungumzia tukio hilo miongoni mwa mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa baada ya kufanya jaribio hilo,  na kufanikiwa kuua kiumbe hicho marehemu alianza kuishiwa nguvu na kuzidiwa ghafla hali ambayo iliwafanya wasamaria wema kumkimbiza hospitali ya serikali ya wilaya ya Tunduru kwa matibabu zaidi.


Walisema binti huyo ambaye alionekana kuweka siri alifichua siri hiyo akiwa katika hatua za mwisho za kukata roho, hali ambayo pia iliwafanya madaktari kumuongezea kwa haraka chupa mbili za damu, iliyotolewa na msamaria aliyefahamika kwa jina moja la Kaimu, ikiwa ni juhudi za kujaribu kuokoa maisha yake.

Walisema baada ya tukio la kifo hicho ndipo yakafichuka mengi kuwa majina hayo aliyokuwa akiyatumia marehemu yalikuwa ni ya uongo ambapo baada ya kumpigia simu baba yake mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Gerodi Msemwa, alieleza kuwa kama kweli aliyefariki dunia ni binti yake jina lake ni Tumaini na sio hayo.

Mzazi huyo ambaye ilimchukua muda mrefu kuyaelewa maelekezo ya kifo cha binti yake alisema kuwa yeye siyo mchaga na wala siyo mkazi wa mkoa wa Mbeya, bali ni mkazi wa mkoa wa Njombe na akaendelea kubainisha kuwa marehemu alitoweka nyumbani miaka mitatu iliyopita na hakuwa na mawasiliano naye.

Taarifa zilizotolewa na rafiki wa marehemu zinaeleza kuwa kabla ya kwenda kufanya kazi katika baa hiyo, alikuwa nafanya kazi katika miji ya Mbeya, Iringa, Songea na  Tunduma ambako inadaiwa kuwa ndiko alikoipatia ujauzito aliokuwa nao hivyo baada ya kuahidiwa kuolewa na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Jaki.

Taarifa zilizotolewa na maafisa tabibu katika hospitali ya Tunduru ambako alilazwa, kabla ya kupatwa na mauti zinaeleza kuwa chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na kutokwa na damu nyingi, pamoja na kiumbe hicho kilicho kuwa na umri wa miezi sita kushindwa kutoka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Msemwa, mwili wa marehemu utazikwa katika makaburi yaliyopo mtaa wa Nakayaya mjini Tunduru.  

No comments: