Friday, February 15, 2013

DIWANI KAPINGA ATOA MSAADA WA CHAKULA KWA WALEMAVU, WAZEE NA WATU WASIOJIWEZA KATIKA KATA YA MKUMBI WILAYANI MBINGA

 Diwani wa kata ya Mkumbi Bruno Kapinga(aliyevaa shati la kijani) akikabidhi msaada wa gunia la mihogo iliyomenywa na kukaushwa vizuri tayari kwa kusagwa na kupata unga wa kupika ugali, kwa mtoto mwenye ulemavu wa miguu na mgongo Elekta Kapinga, ambaye ni mkazi wa kijiji cha Lugari katika kata hiyo. Wanaoshuhudia ni baadhi ya wazee ambao nao walipatiwa msaada huo wa chakula. (Picha na Kassian Nyandindi)





Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SERIKALI imetakiwa kuendelea kuelimisha jamii iwajali na kuwaheshimu watu wenye ulemavu, wazee na watu wasiojiweza kama walivyo watu wengine katika kupata haki sawa, ili waweze kusonga mbele kimaendeleo na kuondokana na migogoro isiyo ya lazima miongoni mwa jamii.

Rai hiyo ilitolewa na Diwani wa kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma Bruno  Kapinga, alipokuwa akitoa msaada wa chakula kwa watu wenye ulemavu, wazee na watu wasiojiweza katika kata hiyo.

“Ndugu zangu hawa ni wenzetu ni lazima tuwajali katika hata kuwapatia misaada mbalimbali, tukiwatenga tutakuwa tunakosea hivyo tushirikiane pamoja”, alisema Kapinga.


Sambamba na hilo Kapinga ambaye pia ni Mjumbe wa kamati ya chama cha mapinduzi(CCM) wilayani Mbinga, aliweza kutoa msaada wa chakula ambacho ni mihogo iliyomenywa na kukaushwa vizuri tayari kwa kusagwa kwa ajili ya kupata ugali.
Msaada huo ulitolewa kwa vijiji sita vilivyopo katika kata ya Mkumbi, ambavyo ni Luwino, Longa, kipegei, Mkumbi, Lugari na Mtawa ambapo jumla ya watu 300 walipatiwa msaada huo.

Vilevile alisema ni vyema elimu itolewe katika jamii ili kupunguza matatizo ya ukiukwaji wa haki za walemavu, wazee na watu wasiojiweza ikiwemo kutowabagua katika maamuzi ya kifamilia.
 
Hata hivyo aliitaka jamii katika karne hii ya sayansi na teknolojia ibadilike na kuachana na mambo ya kiubaguzi kwa watu wenye hali hiyo badala yake watoe ushirikiano mkubwa katika kufanikisha maisha yao.

No comments: