Saturday, February 16, 2013

MADIWANI HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA WAMLALAMIKIA WAKALA WA BARABARA MKOANI RUVUMA

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.











Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemjia juu wakala wa barabara za mkoa huo(TANROAD) kwamba, ameshindwa kusimamia ipasavyo ujenzi wa barabara za wilaya hiyo, ambazo ujenzi wake unasimamiwa na wakala huyo.

Licha ya baraza hilo kutoa malalamiko hayo kadhalika wameilalamikia TANROAD mkoani humo kwa kuwapa tenda za ujenzi wa barabara za wilaya ya Mbinga, makandarasi ambao hawana sifa na vifaa vya kutosha, ambavyo vingeweza kukidhi mahitaji halisi ya kujenga barabara kwa kiwango kinachotakiwa.

Malalamiko ya madiwani hao yalitolewa leo kwenye kikao cha kawaida cha baraza hilo, kilichoketi katika ukumbi wa jumba la maendeleo uliopo Mbinga mjini.



Diwani wa kata ya Litembo Altho Hyera alisema, aliweza kukutana na Meneja wa TANROAD wa mkoa wa Ruvuma Abraham Kissimbo kuzungumzia suala hilo na kupewa majibu kwamba, barabara hizo zinashinddwa kufikia viwango vya ubora unaotakiwa kutokana na kutotengewa fedha za kutosha katika shughuli za ujenzi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu ya meneja huyu haingii akilini, barabara za Tanroad Mbinga zinaleta maswali mengi sana hapa Mbinga, tunahitaji uwazi na ukweli katika hili”, alisema Hyera.


Aidha pamoja na mambo mengine katika kikao hicho, Hyera alisema, ahadi iliyotolewa na Rais Dkt. Jakaya Kikwete katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2010, juu ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kutoka Mbinga mjini  hadi Litembo hospitali, haijatekelezwa hadi sasa na muda unazidi kwenda na ni kwa sababu gani.

Akitolea majibu juu ya suala hilo, Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo alisema amekwisha lifikisha suala hilo katika vikao husika ngazi ya mkoa, hivyo linafanyiwa kazi.

No comments: