Saturday, February 9, 2013

WANA CCM WATAKIWA KUACHA UBAGUZI NA KUJENGA MAKUNDI


Na Steven Augustino,
Tunduru.

VIONGOZI na Wajumbe wa kamati ya Siasa ya Kata Mpya ya Majengo wilayani Tunduru Ruvuma, wamempongeza diwani wa kata hiyo Athumani Nkinde, kwa kuwafungulia miradi zaidi ya shilingi milioni 1.2 iikiwa ni juhudi za kuiendeleza kata yao.

Mwasisi wa Chama cha Mapinduzi(CCM) wilayani humo Neema Chiwinga na Mwenyekiti wa kamati wa kikundi hicho Alus Chibwana ni miongoni mwa viongozi waliotoa pongezi hizo, wakati wakitoa ushuhuda wa maendeleo ya kata yao katika mkutano wa maadhimisho ya CCM kutimiza miaka 36 toka kizaliwe yaliyofanyika kiwilaya katika kata hiyo.

Katika taarifa hiyo viongozi hao walimwelezea diwani Nkinde kuwa ni miongoni mwa madiwani wanaotakiwa kuigwa mfano, wilayani humo kutokana na upendo wake kwa wanachama na wakazi wote wa kata hiyo.


Alusi aliitaja miradi hiyo kuwa ni mradi wa kuuza kuni na mkaa uliogharimu shilingi 750,000 na sasa wameongezewa mradi wa kilimo cha mpunga utakaogharimu zaidi ya shilingi 400,000/ hadi kukamilika kwake na kwamba, miradi yote inaendelea vizuri na wanaouhakika kuwa itawasaidia kuwaletea maendeleo.

Upande wa vikundi vya Napasa na Cheleweni mjini hapa wakimpongeza kwa njia ya nyimbo walidai kuwa diwani huyo, ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, kwa kipindi cha miaka mitatu aliweza kuisaidia wilaya yao kwa moyo wa dhati ingawa kulikuwa na makundi ya watu wachache wasioitakia mema wilaya yao walimpiga vita na kumuangusha katika wadhifa huo.

Pongezi hizo ambazo pia ziliungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tunduru Hamisi Kaesa na mjumbe wake wa halmashauri kuu ya CCM Taifa Ajiri Kalolo walimwelezea   diwani Nkinde kuwa pamoja na wilaya hiyo kushamiri sera za ubaguzi  hasa kwa viongozi wasio kuwa wazawa wa wilaya hiyo, lakini diwani huyo ni hazina na mfano wa kuigwa ndani ya chama hicho kwa madai hata miradi aliyoianzisha na kuibuni kwa wanachama wake wa CCM haina hata sababu ya kuendelea kulumbana.

Pamoja na viongozi hao kusisitiza mshikamano ndani ya chama walikemea vikali tabia za ubaguzi kuwa zikiendelea ipo hatari ya kuiua wilaya yao na chama hicho kwa ujumla, kwa madai kuwa hakuna mji ambao unaweza kujengwa na kabila au wazawa peke yao na wakawataka watu wenye tabia hizo kujifunza kutoka katika miji mingine yenye maendeleo kwa asilimia kubwa imejengwa na wageni.

Katika mkutano huo diwani Athumani Nkinde alisema, pamoja na kuwapongeza wanakikundi hao kwa kumpa moyo katika uendelezaji wa miradi hiyo aliwahimiza kuitunza na kuienzi ili iweze kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Nkinde aliendelea kueleza kuwa lengo la kuwapatia miradi hiyo ni kuonesha njia na mfano kuwa chama katika ngazi zote kinatakiwa kuwa na miradi na kwamba ili kutimiza hayo chama katika ngazi zote kinahitaji viongozi wabunifu na wenye uwezo wa kujituma ili kuonesha njia ya mafanikio kwa wananchi wake.

No comments: