Friday, February 22, 2013

KANISA LAPIGWA MOTO TENA ZANZIBAR, WALIANZA KULIPIGA MAWE, WAHUSIKA WASAKWA, UTARATIBU WA KUYALINDA NA POLISI WAANDALIWA

WATU wasiofahamika, wamelishambulia kwa mawe na kulichoma moto Kanisa la Walokole la Shaloom lililopo eneo la Kiyanga kwa Sheha, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
 

Tukio hilo limetokea juzi saa 9:30 usiku siku mbili tangu kuuawa kwa Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki la Minara Miwili Zanzibar, aliyepigwa risasi tatu kichwani na watu wasiofahamika.

Padri Mushi aliuawa wakati akishuka katika gari lake ili kwenda kuongoza ibada kwenye Kanisa la Betras ambapo wauaji hao, walikuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, ACP Augostine Olomi, alisema moto huo ulizuka kanisani hapo baada ya kikundi cha watu watatu kuonekana wakipita karibu na kanisa hilo.

“Baada ya muda, mlinzi wa kanisa hili alisikia kishindo cha mawe juu ya paa hivyo alilazimika kukimbia na kwenda kujificha huku akiangalia kwa mbele kinachoendelea,” alisema Kamanda Olomi.

Aliongeza kuwa, wakati mlinzi huyo akiwa amejibanza mafichoni, aliona moto ukiwaka ndani ya kanisa ndipo alipopiga simu kwa kiongozi wa kanisa hilo ambaye naye aliwajulisha polisi.

Alisema baada ya polisi kufika eneo la tukio, walisaidiana na wananchi kuuzima moto huo ambao tayari ulishateketeza thamani za kanisa na vitu vingine vilivyokuwa ndani.

Kamanda Olomi alisema, moto huo ungeweza kusababisha athali kubwa kama usingedhibitiwa mapema ambapo dali zakeambazo ni Gibsam, zimesaidia kuunusuru moto huo usifike kwenye paa kuliteketeza kabisa.

“Wakati uongozi wa kanisa ukifanya tathmini ya hasara waliyoipata kutokana na moto huu, Jeshi la Polisi limeanza kuwasaka wahusika wa tukio hili kwa kushirikiana na raia...hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa na uchunguzi unaendelea,” alisema.

Hata hivyo, Kamanda Olomi alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na Vikundi vya Ulinzi Shirikishi na Polisi Jamii, wataanza utaratibu wa kuyalinda makanisa yote ili kuzuia matukio ya aina hiyo.

Mlinzi wa kanisa hilo Bw. Mussa Jackson, alisema awali alikimbilia vichakani ili kunusuru maisha yake na baadaye alikwenda kuomba hifadhi nyumba jirani iliyopo katibu na kanisa hilo.

“Wakati nikiwa lindoni, ghafla niliwaona watu watatu wanakuja ambao sikuwafahamu...nilipojaribu kuwafatilia wakaanza kurusha mawe hivyo nikaamua kukimbia,” alisema Bw. Jackson.

Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Penuel Wisdom alisema alipokea simu kutoka kwa Bw. Jackson ya kuchomwa kwa kanisa hilo ambapo thamani zilizoungua ni pamoja na viti, meza.

“Hii ni hujuma ya pili kufanywa katika kanisa letu ambapo mwaka 2011, kanisa hili lilivunjwa na watu wasiopungua 50, hasara iliyopatikana ilikuwa sh. milioni 20.



Alisema tukio la sasa ni pigo kwa kanisa hilo ambapo zaidi ya waumini 100 wa kanisa hilo, watakosa mahali pa kuabudia.

Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, PCI Yussuf Ilembo, alisema tayari wameanza uchunguzi wa tukio hilo ambapo hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa.(Source Majira)

No comments: