Tuesday, February 5, 2013

BARAZA LA MADIWANI MBINGA NA NYASA LAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YAKE YA MAENDELEO YA WANANCHI KWA MWAKA 2013 / 2014

















Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Oddo Mwisho(Kushoto) aliyevaa joho, wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani bcha mapendekezo ya mpango na bajeti kwa halmashauri ya wilaya ya Nyasa na Mbinga. Kulia kwake ni mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi akifuatilia kwa makini kitabu cha bajeti hiyo.( Picha na Julius Konala)



Na Julius Konala,
Mbinga.


BARAZA la Madiwani katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga na Nyasa mkoani Ruvuma, limepitisha jumla ya shilingi bilioni 65.9 kwa ajili ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya halmashauri hizo katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2014.



Mapendekezo hayo yalipitishwa katika kikao cha baraza hilo, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo uliopo mjini hapa, na kuwasilishwa na kaimu ofisa mipango wa wilaya ya Mbinga Oscar Yapesa kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, chini ya Mwenyekiti wake Oddo Mwisho.



Yapesa alifafanua kwa kuanza na mapendekezo ya bajeti ya wilaya ya Nyasa, ambapo alisema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 28,842,596,431 zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kimaendeleo ya wananchi.



Kadhalika alieleza kuwa shilingi bilioni 37,073,888,863 nazo zitatumika kwa maendeleo ya wilaya ya Mbinga.




Yapesa alisema mipango na bajeti ya halmashauri hizo zimeandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya serikali, na matakwa ya msingi ya ugatuaji wa mamlaka kwa wananchi.



Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga Peter Mdaki alisema bajeti hizo zimezingatia kipaumbele katika sekta za elimu ya msingi na sekondari ujenzi wa nyumba za walimu, maabara, hosteli na kununua vifaa vya maabara kwa baadhi ya shule za sekondari.



Akizungumzia kwa upande wa sekta ya afya alisema wamezingatia ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati vijijini, kuweka vifaa vya umeme jua kwa baadhi ya zahanati, ujenzi wa jengo la upasuaji katika hospitali ya wilaya ya Mbinga pamoja na ununuaji wa madawa.



Mdaki alieleza kuwa bajeti hiyo imelenga pia ukamilishaji wa miundombinu ya miradi ya umwagiliaji, kuotesha miche ya kahawa, ununuzi wa mitambo ya kumenyea kahawa, ujenzi wa kituo cha mafunzo ya kilimo(Resource Centre) ambavyo vipo wilayani Mbinga katika kata ya Maguu na Mkako.



Hata hivyo alioongeza kuwa katika bajeti hiyo kutajengwa machinjio ya kisasa ambayo itajengwa katika kijiji cha Mtama wilayani humo na ukamilishaji ujenzi wa kituo cha mafunzo ya wanyama kazi.




No comments: