Monday, May 29, 2017

WAUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS DKT. JOHN MAGUFULI

Na Dustan Ndunguru,
Geita.

WACHIMBAJI wadogo wa madini katika migodi ya Kakola na Nyakagwe wilaya ya Kahama na Geita mkoani Geita, wamesema kuwa uamuzi aliochukua Rais Dkt. John Magufuli wa kuunda tume kwa ajili ya kuchunguza Makontena yenye mchanga wenye madini ulikuwa ni wa busara kutokana na ukweli kwamba mchanga huo uliokuwa ukisafirishwa kwenda nje ya nchi, ulikuwa wenye madini jambo ambalo lilikuwa likisababisha nchi kukosa mapato yake.

Dkt. John Magufuli.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wachimbaji wadogo, Robert Nyamaigolo na Golod Makinga walisema kuwa kila Mtanzania ambaye ana uzalendo wa kweli anapaswa kupongeza jitihada hizo zilizofanywa na Dkt. Magufuli baada ya kumaliza kazi hiyo na kuchukua hatua.

Nyamaigolo alisema uzoefu unaonesha kuwa miaka mingi tume za kuchunguza masuala mbalimbali zilizokuwa zikiundwa zilikuwa hazitoi majibu yenye kuzaa matunda na baadaye wananchi walikuwa wakikosa imani na serikali yao.

“Rais Magufuli ameunda tume ya kuchunguza tatizo hili, mara ilipobainika kulikuwa na uzembe kwa watendaji husika ambao wameufanya mara moja amechukua hatua ya kuwawajibisha, ni jambo ambalo anapaswa kupongezwa hasa kwa Watanzania ambao ni wazalendo na wenye uchungu na rasilimali za nchi yao”, alisema Nyamaigolo.

Sunday, May 28, 2017

RC RUVUMA AKERWA NA MJI WA MBINGA ULIVYOSHEHENI TAKA KATIKA MAENEO MBALIMBALI

Hali ya maghuba ya kuhifadhia taka jinsi ilivyo.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amechukizwa na hali ya mji wa Mbinga mkoani humo kuwa katika hali ya uchafu na kwamba ametoa agizo kwa viongozi husika wahakikishe kwamba ndani ya wiki mbili, mji huo unakuwa katika hali ya usafi.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa mkoa alilitoa jana wakati alipokuwa akizungumza na Wazee wa mji wa Mbinga katika kikao maalum kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, ambacho kililenga kusikiliza kero zao mbalimbali.

Hoja ya mji huo kuwa mchafu ilianza kuibuliwa na mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Yordan Konzo na kuungwa mkono na Wazee wenzake, ambapo walieleza kuwa taka zimekuwa hazizolewi kwa muda mrefu katika maghuba ya kuhifadhia taka, jambo ambalo limefikia hatua taka hizo zimekuwa zikitoa harufu na kuwa kero katika makazi ya watu na jamii kwa ujumla.

DKT. MAGUFULI NA MKEWE MAMA JANETH LEO WATEMBELEA WAGONJWA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI JIJINI DAR ES SALAAM



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akizungumza na mzee Francis Maige Kanyasu (Ngosha) aliyelazwa wodi ya Mwaisela katika hospitali ya Taifa Muhimbili akipatiwa matibabu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akiwa pamoja na mkewe Mama Janeth Magufuli wakimtakia heri mtoto Shukuru Kisonga aliyelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili pamoja na mama yake Mwanahabibi Mohamed Mtei.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akiwajulia hali wagonjwa wengine waliolazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Ikulu)

Thursday, May 25, 2017

KUFUNGWA KWA BENKI YA WANANCHI MBINGA MASWALI NI MENGI KULIKO MAJIBU

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

KUFUATIA Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kufunga milango ya Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) isiendelee kufanya kazi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Serikali (MBINGONET) wilayani humo wamesema kuwa kufilisika kwa benki hiyo kumesababishwa na viongozi waliopewa dhamana ya kuiendesha kutokuwa makini na utendaji kazi, usimamizi na utekelezaji wa majukumu husika.

Aidha MBINGONET wameiomba BOT ifanye uchunguzi wa kina juu ya suala hilo na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani, kwani ikumbukwe kuwa MCB ilikuwa ni mkombozi wa wakulima wadogo wadogo ikiwemo vikundi vya ujasiriamali vilivyopo ndani na nje ya wilaya hiyo.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Mtandao huo wa mashirika yasiyokuwa ya serikali wilayani Mbinga, Benedict Luena wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

Luena alieleza kuwa imekuwa ni jambo la aibu kwa wanambinga kupitia vijana wao wasomi ambao waliaminika katika kuendesha benki hiyo lakini hivi sasa wameshindwa kuiendesha kutokana na kutanguliza mbele maslahi yao binafsi.

Wednesday, May 24, 2017

RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI PROFESA SOSPETER MUHONGO


RAIS DKT. MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA KAMATI MAALUM ILIYOFANYA UCHUNGUZI WA MCHANGA WA MADINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, akipokea taarifa ya uchunguzi wa mchanga wa madini mbalimbali uliotakiwa kusafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini hapa nchini, kutoka kwa Mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Abdulkarim Hamis Mruma leo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Dkt. John Magufuli Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, akiangalia taarifa hiyo ya uchunguzi wa mchanga wa madini uliotakiwa kusafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo mbalimbali ya madini hapa nchini, mara baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Abdulkarim Hamis Mruma Ikulu Jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wa kwanza upande wa kulia wakishuhudia tukio hilo.

AKUTWA AMEFARIKI DUNIA KWENYE NYUMBA YA KULALA WAGENI

Na Mwandishi wetu,   
Songea.

ASHA Rais (41) ambaye ni mkazi wa Newala mkoani Mtwara, amekutwa akiwa amefariki dunia kwenye nyumba ya kulala wageni ambayo ipo karibu na uwanja wa michezo wa Majimaji, katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na Mwandishi wetu, Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Zubery Mwombeji alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya jioni kwenye nyumba ya kulala wageni inayofahamika kwa jina la Salama, ambayo ipo kwenye kata ya Mfaranyaki mjini hapa.

Mwombeji alisema kuwa inadaiwa siku hiyo kabla ya tukio hilo kutokea, Asha alikuwa amepanga chumba namba 412 katika nyumba hiyo ya kulala wageni ambako baadaye aligundulika akiwa amefariki dunia katika chumba hicho.

Sunday, May 21, 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA AMTEMBELEA RAIS MSTAAFU MKAPA NYUMBANI KWAKE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akisalimiana na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa wakati alipomtembelea Rais huyo mstaafu leo nyumbani kwake Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Rais mstaafu Benjamin Mkapa wakati alipomtembelea Rais huyo mstaafu leo nyumbani kwake Jijini Dar es salaam. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)

RAIS WA TANZANIA NA UGANDA WASAINI TAMKO LA PAMOJA UTEKELEZAJI WA UJENZI BOMBA LA MAFUTA HOIMA NA TANGA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni na wajumbe wenzao wakiwa katika mazungumzo ya mwisho,  kabla ya kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano na vipengele vya mkataba wa utekelezaji mradi wa ujenzi bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania kwenye hafla iliyofanyika leo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais Dkt. John Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakitia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano na vipengele vya mkataba wa utekelezaji mradi wa ujenzi bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga Tanzania katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akizungumza mara baada ya kukamuilisha zoezi la utiaji saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano na vipengele vya mkataba wa utekelezaji mradi wa ujenzi bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli akizungumza mara baada ya kukamuilisha zoezi la utiaji saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano na vipengele vya mkataba wa utekelezaji mradi wa ujenzi bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania katika hafla iliyofanyika leo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Rais Dkt. John Magufuli na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wakiwa na Mawaziri na maafisa waandamizi wa nchi zote mbili baada ya kukamilika zoezi la utiaji saini tamko la pamoja, kukamilika kwa majadiliano na vipengele vya mkataba wa utekelezaji mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania leo Ikulu Jijini     Dar es salaam. (Picha zote na Ikulu)

Saturday, May 20, 2017

VITAMBI BADO NI CHANGAMOTO KUBWA INAYOWAKABILI WATANZANIA

DAKTARI Mshauri kutoka Chama cha Afya ya Jamii Tanzania (TPHA) Dkt. Ali Mzige amewataka Watanzania kuepuka uzito mkubwa na kitambi ili kufanya miili yao kukaa mbali na magonjwa yanayosababishwa na vitu hivyo.

Aidha Dkt. Mzige amezungumza hayo leo katika ukumbi wa maelezo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakichukulia kawaida na wengine wanapenda kuwa na kitambi na uzito mkubwa, lakini ni vitu vyenye madhara makubwa na husababisha magonjwa ambayo ni magumu kutibika.

Friday, May 19, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI WAMUOMBA KUINGILIA KATI UJENZI MRADI WA MAJI MKAKO MBINGA

Rais Dokta John Magufuli.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MRADI wa maji ambao umejengwa katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, umeendelea kuingia dosari na kuchukua sura mpya baada ya Wananchi wa kata hiyo kuendelea kulalamikia kwamba mradi huo umekuwa ukitoa maji machafu ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Kadhalika licha ya kuunyoshea kidole kwamba unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika, bado wakazi hao wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kuingilia kati na kuwachukulia hatua kali watendaji wote waliohusika na usimamizi mbovu juu ya mchakato wa ujenzi wa mradi huo.

Baadhi yao wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa kuomba majina yao yasitajwe katika mtandao huu walisema kuwa wameshangazwa na serikali kwa kutochukua hatua za haraka licha ya kulalamikia jambo hilo kwa muda mrefu, hadi ilipofikia hatua ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour kutoa agizo lake Mei 8 mwaka huu kwa kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aunde Kamati ya kushughulikia suala hilo na kumpatia majibu haraka iwezekanavyo.

MAKATIBU MAHSUSI HAPA NCHINI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mkutano wa mwaka wa tano wa Chama cha Makatibu Mahususi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Jakaya Kikwete, mjini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria Mkutano mkuu wa Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

MAKAMU wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Makatibu Mahsusi hapa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuacha tabia ya kutoa siri za ofisi zao, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Samia Suluhu Hassan alitoa kauli hiyo leo wakati anafungua mkutano wa tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mji Dodoma.

Alisisitiza kuwa uadilifu na uaminifu ndio njia pekee ya kuaminiwa na viongozi wao, hivyo ni muhimu kwa makatibu hao kufanya kazi kwa bidii na ubunifu mkubwa katika maeneo yao ya kazi.

SONGEA YAELEZWA KUWA NA VIJANA 208 WALIOATHIRIKA NA MADAWA YA KULEVYA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

KATIKA Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeelezwa kuwa jumla ya vijana 208 wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alitoa takwimu hizo akieleza kuwa katika kundi la waathirika hao Wanawake wapo nane na wanaume ni 200 ambao wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.

Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo alifafanua kuwa waliokamatwa na dawa za kulevya kwa mwaka huu wapo 16 na kwamba baadhi yao mashauri tisa yamefikishwa Mahakamani huku kesi mbili tayari zimehukumiwa kutokana na matumizi ya madawa hayo.

Thursday, May 18, 2017

HALMASHAURI HAPA NCHINI KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI VIJIJINI

Mratibu wa mradi wa usafi wa mazingira uitwao Nipo tayari, Juliana Kitira akimuonyesha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kakonko, Kigoma, Elinatha Elisha takwimu za hali ya usafi wa mazingira katika halmashauri yake kwenye semina inayofanyika mjini Morogoro. Mradi huo pia unahamasisha uwepo wa vyoo bora na kunawa mikono na maji safi baada ya kutoka chooni.
Na Mwandishi wetu,
Morogoro.

HALMASHAURI za wilaya hapa nchini, zimetakiwa kuongeza ufanisi katika kusimamia miradi ya maji kwa kuchangamkia fursa ya fedha za kitanzania bilioni 250 zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji maji safi na salama vijijini kwa mwaka 2016-2020.

Mkurugenzi msaidizi wa Wizara ya maji na umwagiliaji Injinia Jackson Mutazamba aliwaambia wakurugenzi wa wilaya katika semina inayofanyika mjini Morogoro jana kuwa ni halmashauri chache tu ndio zimeanza kupata fedha hizi mara baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa na wafadhili hao.

“Kuna fedha za kutosha katika mradi huu ukilinganisha na mwamko wa halmashauri katika kuchangamkia fursa hii ya kuongeza mtandao wa maji katika maeneo yao”, alisema na kuongeza kuwa fedha hizi zinaweza kuzisaidia halmashauri kuanzisha miradi mipya na kukarabati ile ya zamani ili iweze kutoa maji kwa wakati wote wa mwaka.

Alisema moja ya sharti la upatikanaji wa fedha hizi ni ufanisi katika utekelezaji wa miradi iliyopita na ubora wa ripoti za kila mwezi kama ambavyo programu hii inavyozitaka halmashauri, huku akieleza kuwa kigezo hiki ni muhimu katika kuvuka hatua moja hadi nyingine na kupata fungu kubwa zaidi la fedha ambalo litawezesha kutekeleza miradi mikubwa zaidi katika halmashauri husika.

PAMS FOUNDATION WAFANIKIWA KUPUNGUZA MAUAJI YA TEMBO SELOU

Na Dustan Ndunguru, 
Songea.

SHIRIKA lisilokuwa la serikali, (PAMS Foundation) ambalo linajishughulisha na mapambano dhidi ya ujangili katika hifadhi ya pori la akiba la Selou, limefanikiwa kupunguza mauaji ya tembo kutoka mizoga 42 kwa mwezi hadi kufikia mzoga mmoja wa tembo baada ya miezi sita.

Pori hilo linaunganisha kati ya nchi mbili za Tanzania na Niassa Msumbiji ambapo shirika hilo lipo katika kukabiliana na uwindaji haramu unaofanywa na baadhi ya watu hapa nchini.

Akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa Mratibu wa shirika hilo, Maximillan Jenes alisema kuwa mafanikio hayo yametokana ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili, katika kuimarisha doria kwenye maeneo ya ushoroba wa Selou kwa upande wa Namtumbo mkoani Ruvuma, Nanyumbu mkoani Mtwara pamoja na hifadhi ya mto Ruvuma karibu na Msumbiji kwa kutumia ndege na magari.

Jenes alisema kuwa baada ya kuimarishwa kwa doria za anga katika hifadhi ya pori la akiba la Selou kwa upande wa Tanzania, vitendo hivyo vya ujangili hivi sasa vimeendelea kushamiri zaidi kwa upande wa pili wa mto Ruvuma ndani ya hifadhi ya Niasa nchini Msumbiji ambapo hatua mbalimbali zinachukuliwa kwa kushirikiana kati ya nchi hizo mbili kwa lengo la kumaliza tatizo hilo.

CHAMA CHA MAPINDUZI MKOANI RUVUMA CHASIKITIKA KUPOTEZA MADIWANI WAKE WILAYANI TUNDURU

Na Dustan Ndunguru, 
Songea.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Ruvuma kimesema kwamba, kimepatwa na mshtuko mkubwa kufuatia kufariki dunia kwa Madiwani wake wawili kutoka katika kata za Lukumbule na Kalulu wilayani Tunduru mkoani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Oddo Mwisho alisema vifo hivyo vilitokea Mei 13 mwaka huu na kuwaacha katika simanzi kubwa wananchi wa kata hizo.

Mwisho alisema diwani wa kata ya Lukumbule, Zubery Solo alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu na kwamba aliyekuwa diwani wa kata ya Kalulu Mnomba Kazembe amepoteza maisha baada ya kuvamiwa na watu wasiofahamika.

Wednesday, May 17, 2017

MHANDISI IDARA YA MAJI MBINGA ASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI UJENZI MRADI WA MAJI

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

SERIKALI wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imechukua hatua ya kumsimamisha kazi Mhandisi idara ya maji wilayani humo Vivian Mndolwa kwa lengo la kupisha uchunguzi juu ya ujenzi wa mradi wa maji uliopo katika kitongoji cha Mnazi mmoja kijiji cha Mkako kata ya Mkako, ambao unadaiwa kujengwa chini ya kiwango na kushindwa kuwafikishia maji wananchi katika maeneo husika ndani ya kata hiyo.

Vivian Mndolwa.
Aidha kusimamishwa kazi kwa Mhandisi huyo kunafuatia agizo lililotolewa Mei 8 mwaka huu na kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour wakati anaukagua mradi huo ili Mkuu wa wilaya hiyo, Cosmas Nshenye aweze kuunda kamati itakayofanya kazi ya kuchunguza tatizo hilo na baadaye hatua husika ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika waliouhujumu.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa Mhandisi huyo pia analalamikiwa akidaiwa kushindwa kusimamia kikamilifu taratibu za ujenzi wa mradi huo wa maji.

Mradi huo ulianza kujengwa Machi 28 mwaka 2014 kwa gharama ya shilingi milioni 718,896,533 chini ya ufadhili wa benki ya dunia ambapo ilibidi ujenzi wake ukamilike katika kipindi cha mwaka mmoja tangu uanze kujengwa, lakini hadi kufikia kipindi cha mwaka huu 2017 ujenzi huo bado haujakamilika na fedha za mradi huo zimetumika katika kazi hiyo ya ujenzi.

SAID MECK SADICK ATAJA SABABU ZILIZOMFANYA AACHIE NGAZI NAFASI YA MKUU WA MKOA


Na Mwandishi wetu,

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadick amesema kuwa ameamua kuondoka serikalini baada ya kufanya kazi ya utumishi wa umma kwa muda mrefu na anakwenda kupumzika mkoani Mwanza, huku akiwa mfugaji wa samaki.

Aidha Sadick alisema kuwa pia kulingana na afya yake, anahitaji kupisha vijana wadogo wamsaidie Rais Dkt. John Pombe Magufuli kulingana na kasi yake kwani yeye ameepuka kumkwaza Rais wakati wa utekelezaji wa majukumu yake kama mkuu wa mkoa.

“Uamuzi huu wa kupumzika nilimuomba Rais kwa muda mrefu sana na nikirudi kijijini nitaendelea na ufugaji samaki maana nilishaandaa bwawa la kufugia, nitaendelea nalo huku nikiwaza jambo lingine la kufanya,” alisema.

Sadick alisema hayo jana wakati akitaja sababu zilizochangia kumuomba Rais Dkt. Magufuli kuacha kazi yake ya ukuu wa mkoa wa Kilimanjaro.

Monday, May 15, 2017

SONGEA WAFURAHIA HUDUMA ZA SIMBANKING BENKI YA CRDB

Na Mwandishi wetu, 
Songea.

BAADHI ya Wananchi waishio katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameonesha kufurahishwa kwao na huduma za Simbanking ambazo zinatolewa na benki ya CRDB, hivyo kuwawezesha kufanya miamala ya kifedha kupitia simu zao za mkononi pasipo usumbufu wa aina yoyote ile.

Wameeleza kuwa wanaweza kufanya miamala mbalimbali kama vile kuhamisha fedha zao kutoka kwenye akaunti walizonazo katika benki hiyo kwenda kwenye mitandao mingine ya simu na kulipia bili za umeme na mambo mengineyo.

Aidha walisema kuwa huduma hiyo imerahisisha kwa kiwango kikubwa kufanya shughuli zao za kiuchumi kama vile kununua pembejeo kwa kufanya malipo moja kwa moja kwa kutumia huduma ya Simbanking.

Ibrahim Luanda ambaye ni mkazi wa mtaa wa Luhira, Yona Mkuta wa Miembeni na Elias Fanuel mkazi wa mtaa wa Majengo mjini hapa walisema huduma hiyo kwao imewasaidia kuongeza hata kiwango cha uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

WAHAMIAJI HARAMU NANE WAKUTWA WAKIWA WAMEFARIKI DUNIA KATIKA MAKABURI YA KIJIJI CHA AMANI MAKOLO MBINGA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

WATU nane wamekutwa wakiwa wamekufa na wengine 25 wakiwa hai katika eneo la makaburi ya kijiji cha Amani Makolo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambao inadaiwa kwamba walikuwa wakitoka nchini Ethiopia kwenda Afrika kusini kutafuta maisha.

Inadaiwa kuwa watu hao ni wahamiaji haramu ambapo walitelekezwa kwenye eneo hilo la makaburi, huku wakiwa na hali mbaya kutokana na kukosa chakula kwa muda mrefu hali ambayo ilisababisha wengine kufariki dunia.

Mmoja wa mashuhuda ambaye ni mkazi wa kijiji hicho, ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe aliwaambia waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilibainishwa na wachimbaji wadogo wa madini aina ya Salphire waliopo katika kijiji hicho, ambao walisikia sauti za watu wakiongea kutoka eneo hilo la makaburi na ndipo walipofuatilia waliona kundi la watu hao wakiwa wamelala chini.

Friday, May 12, 2017

BOT YAIFUNGA RASMI BENKI YA WANANCHI MBINGA MAMIA YA WANANCHI WAKUSANYIKA WATAKA KUVAMIA ENEO LA BENKI

Benki Kuu ya Tanzania (BOT)
Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

MAMIA ya Wananchi ambao ni baadhi ya wateja wa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma wamekusanyika na kutaka kuvamia eneo la benki hiyo huku wakipaza sauti zao, wakidai akiba za fedha zao walizoweka baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kuchukua maamuzi ya kuifunga MCB na kusitisha shughuli zake zote za kibenki.

“Tunataka fedha, tunataka fedha sisi hatma ya fedha zetu ipo wapi kama leo hii benki inafungwa, tunataka fedha zetu”, walisikika wakisema kwa sauti kubwa.

Tukio hilo lilitokea leo Mei 12 mwaka huu majira ya asubuhi ambapo Askari wa kutuliza ghasia (FFU) ndiyo waliokuwa wamezunguka kulinda eneo la benki hiyo, wakati wafanyakazi wa BOT wakitangaza hadharani kufuta leseni ya biashara ya Benki ya Wananchi Mbinga kuanzia sasa.

Wednesday, May 10, 2017

JANUARI HADI DISEMBA MALARIA MANISPAA SONGEA YAUA WATU 87

Na Mwandishi wetu,     
Songea.

IMEBAINISHWA kuwa ugonjwa hatari wa malaria katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana, katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma umesababisha vifo vya watu 87 sawa na asilimia 10.9 ya vifo vyote 798 vilivyotokea kutokana na magonjwa mengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyomfikia mwandishi wetu kutoka kwa Afisa habari wa Manispaa hiyo, Albano Midelo alisema kuwa katika vifo hivyo watoto chini ya miaka mitano waliokufa kutokana na ugonjwa wa malaria walikuwa 34 ambao ni sawa na asilimia tisa ya vifo vyote vilivyotokea kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambavyo vilikuwa 401.

Midelo alisema kuwa mwaka 2016 Manispaa ya Songea ilikuwa na wagonjwa wa malaria waliopata matibabu ya nje 5,928 ambao ni sawa na asilimia 2.4 ya wagonjwa wote 244,245 waliopata matibabu ya nje.

Alisema kuwa wagonjwa waliogua ugonjwa wa malaria na kulazwa kwa mwaka huo ni sawa na asilimia 2.5 ya wagonjwa wote  244,425 waliolazwa.

Tuesday, May 9, 2017

DOKTA MAGUFULI ATOA MSAADA WA MAGARI YA KUBEBEA WAGONJWA KWA WABUNGE WA NKASI, TABORA NA SHINYANGA

Katibu mkuu Balozi John Kijazi (katikati) akiwa na Katibu mkuu Ikulu Alphayo Kidata (kushoto) na Mkurugenzi wa huduma Ikulu Charles Mwankupili (kulia) na wabunge Mhe. Alli Mohamed Kessy ambaye ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Mhe. Munde Tambwe na Mhe. Lucy Mayenga (Wabunge viti maalum) baada ya kuwakabidhi magari ya kubebea wagonjwa ambayo wamepewa msaada na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Mei 9 mwaka huu. (Picha na Ikulu) 

WATU WATANO WA FAMILIA MOJA WAFARIKI DUNIA BAADA YA NYUMBA YAO KUANGUKIWA NA MTI

Baadhi ya wananchi wakiondoa paa la nyumba ili kuokoa watu waliokuwa wameangukiwa na mti huo majira ya usiku.
Miili ikiwa imeshapakiwa ndani ya gari la Polisi kwenda kuhifadhiwa hospitalini.
Na Mwandishi wetu,  
Arusha.

MVUA zinazonyesha mfululizo mkoani Arusha, zimeleta maafa makubwa katika familia ya mzee Jonathan Kalambiya (55) ambaye ni mkazi wa mtaa wa Sokoni katika kijiji cha Kinyeresi wilayani Arumeru mkoani humo, baada ya mti mkubwa uliong’olewa na maji ya mvua hizo kuangukia nyumba yake na kuua watoto wake watano.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya usiku baada ya mti huo kuangukia nyumba yake na kuleta madhara hayo.

Charles Mkumbo ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoani Arusha amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watoto hao waliofariki dunia kuwa ni Miliamu Jonathan (16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Inaboishu.

Monday, May 8, 2017

MAKAMU WA RAIS AONGOZA WATANZANIA KUAGA MIILI YA WANAFUNZI WALIOFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI MKOANI ARUSHA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa zoezi la kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.


Jeshi la Wananchi(JWTZ) wakiingiza miili ndani ya uwanja kwa ajili ya kuombewa pamoja na kuagwa leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitoa pole kwa ndugu na jamaa wa marehemu waliofika katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuaga miili hiyo.

Miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent ikiwa katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuombewa pamoja na kuagwa leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitoa heshima za mwisho kwenye miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwafariji ndugu na jamaa wa marehemu waliofika kuaga miili ya ndugu zao leo katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa Kiserikali na chama wakiwa kwenye uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha wakati wa kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent.

Wanafunzi wa shule ya Lucky Vicent wakiwa kwenye majonzi wakati wa kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.


Baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha wakiwa katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha kwa ajili ya kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent waliofariki kwenye ajali.
Na Mwandishi wetu,

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Mei 8 mwaka huu ameongoza mamia ya wananchi mkoani Arusha na mikoa jirani katika kuaga miili ya wanafunzi 32, walimu wawili pamoja na dereva mmoja wa shule ya Lucky Vicent Jijini Arusha katika uwanja wa Shekh Amri Abeid ambao walipata ajali kwenye eneo la Rhotia, wilayani Karatu mkoani humo.

Katika hotuba yake kwa wananchi hao waliojitokeza katika tukio hilo la kuaga miili hiyo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta John Pombe Magufuli, Makamu huyo wa Rais aliwahakikishia waombolezaji wote kuwa serikali ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu chenye majonzi mazito kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Makamu huyo wa Rais alihimiza wananchi wote hapa nchini kuungana pamoja katika msiba huo uliotokea, na kuwafariji wafiwa hasa kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi.

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU AWATAKA WATENDAJI MJI WA MBINGA KUSIMAMIA KIKAMILIFU MIRADI YA WANANCHI

Kiongozi Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour akiwasalimia wananchi (hawapo pichani) katikati ni Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya mji wa Mbinga Robert Mageni na upande wa kulia ni Meneja wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (MBIUWASA) Patrick Ndunguru.
Na Kassian Nyandindi,           
Mbinga.

KIONGOZI Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour amewataka Watendaji waliopo katika Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wahakikishe kwamba, fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo ili ziweze kuleta tija katika jamii.

Aidha ameagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa kwa wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.

Hayo yalisemwa juzi na kiongozi huyo wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru wakati alipokuwa katika halmashauri ya mji huo akikagua jumla ya miradi kumi yenye thamani ya shilingi milioni 435,332,081 ambayo Mwenge huo umeweza kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa, kukaguliwa na kuzinduliwa.

HALMASHAURI MJI WA MBINGA WATAKIWA KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Amour Hamad Amour akipokea zawadi ya kahawa iliyosagwa kitaalamu kutoka kwa Deogratias Haulle ambaye ni mtaalamu wa kutengeneza kinywaji hicho kutoka Kiwanda cha kukoboa kahawa Mbinga(MCCCO) mkoani Ruvuma. Hata hivyo kahawa hiyo alikabidhiwa katika eneo la banda la maonyesho kwenye mkesha wa Mwenge wa Uhuru uwanja wa Masumuni uliopo mjini hapa.
Na Kassian Nyandindi,         
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa hali ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa Malaria kwa akina mama Wajawazito, Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2016/2017 imefikia kuwa ni asilimia 1.9 na kwa upande wa Watoto chini ya miaka mitano ni asilimia 9.6 ambapo halmashauri hiyo inaendelea na mikakati mbalimbali ya mapambano dhidi ya kuutokomeza ugonjwa huo.

Mkuu wa wilaya ya Mbinga Cosmas Nshenye alisema hayo juzi alipokuwa akisoma risala ya utii wa wananchi wa halmashauri ya mji wa Mbinga kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ambayo ilisomwa mbele ya kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Amour Hamad Amour katika viwanja vya Masumuni mjini hapa.

Nshenye alisema kuwa mapambano hayo dhidi ya ugonjwa wa Malaria wamejipanga kikamilifu kwa kuhakikisha wanatekeleza, elimu ya Kinga dhidi ya ugonjwa huo inaendelea kutolewa kwa wananchi ambapo mpaka sasa jumla ya kata 19 na vijiji 49 vimefikishiwa elimu husika ikiwemo kufanya usafi wa mazingira na matumizi sahihi ya vyandarua.

Sunday, May 7, 2017

SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUTOKA KWA WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA KUFUATIA AJALI ILIYOPOTEZA MAISHA YA WANAFUNZI 32 HUKO KARATU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
WATANZANIA wenzangu, ninaungana na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pole nyingi sana kwa uongozi wa shule ya Lucky Vicent pamoja na wazazi wa watoto waliopoteza maisha kwenye ajali ya jana.

Mungu awape faraja katika kipindi hiki kigumu cha majonzi. Tuna muomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.

Amina.
Mhe. Kassim Majaliwa (MB)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


DOKTA MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA WANAFUNZI WA LUCKY VICENT


Saturday, May 6, 2017

RAIS DOKTA MAGUFULI AONGOZA MKUTANO WA BARAZA LA TAIFA LA BIASHARA NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza mkutano wa Baraza la kumi la Biashara Tanzania, katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam leo Mei 6, 2017. Wengine ni Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (kushoto), Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi (kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi.
Baadhi ya Mawaziri pamoja na Wajumbe, wakimsikililiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara, Dkt. John Pombe Magufuli wakati akizungumza katika mkutano wa Baraza la kumi la Biashara Tanzania, kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam leo Mei 6, 2017. (Picha zote na Ikulu)