Sunday, May 28, 2017

RC RUVUMA AKERWA NA MJI WA MBINGA ULIVYOSHEHENI TAKA KATIKA MAENEO MBALIMBALI

Hali ya maghuba ya kuhifadhia taka jinsi ilivyo.
Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge amechukizwa na hali ya mji wa Mbinga mkoani humo kuwa katika hali ya uchafu na kwamba ametoa agizo kwa viongozi husika wahakikishe kwamba ndani ya wiki mbili, mji huo unakuwa katika hali ya usafi.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa mkoa alilitoa jana wakati alipokuwa akizungumza na Wazee wa mji wa Mbinga katika kikao maalum kilichofanyika kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa, ambacho kililenga kusikiliza kero zao mbalimbali.

Hoja ya mji huo kuwa mchafu ilianza kuibuliwa na mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Yordan Konzo na kuungwa mkono na Wazee wenzake, ambapo walieleza kuwa taka zimekuwa hazizolewi kwa muda mrefu katika maghuba ya kuhifadhia taka, jambo ambalo limefikia hatua taka hizo zimekuwa zikitoa harufu na kuwa kero katika makazi ya watu na jamii kwa ujumla.


“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa mji huu ni mchafu unanuka sana, tumekuwa tukilalamika siku nyingi kwenye mikutano husika lakini hakuna hatua zinazochukuliwa na mji bado ni mchafu ni vizuri sasa, uwekwe mkakati kabambe wa kupambana na mazingira haya ili yawekwe katika hali nzuri ya usafi”, alisisitiza Konzo.

Kwa upande wake Dkt. Mahenge alipomtaka Mkurugenzi mtendaji wa mji huo, Robert Mageni kutolea ufafanuzi juu ya kero hiyo Mkurugenzi huyo alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kueleza kuwa, hatua zitachukuliwa za kuusafisha mji huo ili uweze kuwa katika hali ya usafi.

“Tatizo kubwa linalotukabili hapa Mheshimiwa Mkuu mkoa ni kutokana na kukosa rasilimali fedha, magari ya kuzolea taka na vifaa kwa ujumla vya kufanyia kazi hii lakini tumeanza zoezi la uzoaji wa taka hizi kulingana na vifaa vichache tulivyonavyo kwanza”, alisema Mageni.

Pamoja na Mkurugenzi huyo kutolea maelezo hayo Dkt. Mahenge bado alieleza kuwa uwezo wa halmashauri hiyo kuzoa taka hizo katika maghuba yaliyopo mjini humo upo, hivyo wanachopaswa ni kutilia mkazo suala hilo na sio kulifanyia uzembe kwa kuacha taka zirundikane kwa muda mrefu kwenye maghuba hayo.

Aliongeza kuwa mji wa Mbinga hautakiwi kuwa katika hali ya uchafu lengo la kufanya hivyo ni kuweza kuepukana na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kwamba, amewataka viongozi wanaosimamia masuala ya usafi washirikishe jamii katika maeneo yao wanayoishi ili waweze kuchangia kidogo gharama za uzoaji taka na usafi kwa ujumla ndani ya mji huo.

“Baada ya wiki hizi mbili kupita nitakuja mwenyewe kukagua mji huu kama agizo langu la usafi wa kuzoa taka katika maghuba limetekelezwa nataka elimisheni wananchi, kaeni nao pamoja ili mshirikiane katika zoezi hili wakati mwingine wanashindwa kuchangia kwa sababu hamuwashirikishi ipasavyo”, alisema Dkt. Mahenge.


  



No comments: