Friday, May 19, 2017

SONGEA YAELEZWA KUWA NA VIJANA 208 WALIOATHIRIKA NA MADAWA YA KULEVYA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

KATIKA Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imeelezwa kuwa jumla ya vijana 208 wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya kuanzia kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu.

Albano Midelo ambaye ni Ofisa habari wa Manispaa hiyo alitoa takwimu hizo akieleza kuwa katika kundi la waathirika hao Wanawake wapo nane na wanaume ni 200 ambao wote wakiwa na umri kati ya miaka 15 hadi 45.

Kwa mujibu wa Ofisa habari huyo alifafanua kuwa waliokamatwa na dawa za kulevya kwa mwaka huu wapo 16 na kwamba baadhi yao mashauri tisa yamefikishwa Mahakamani huku kesi mbili tayari zimehukumiwa kutokana na matumizi ya madawa hayo.


Alisema kuwa matumizi ya dawa hizo hasa kwa vijana katika Manispaa hiyo bado ni tatizo kubwa kama ilivyokuwa nchi nzima na duniani kote kwa ujumla.

Takwimu zinaonesha kwamba katika kipindi cha mwaka jana Manispaa ya Songea ilikuwa na waathirika wa dawa za kulevya 97 wakiwemo wanaume 95 na wanawake wawili.

“Tunatoa wito kwa wananchi wote kutojihusisha kwa namna yeyote ile na matumizi ya dawa hizi za kulevya, halmashauri yetu kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ambao ni HJFMRI-WRP na Chama cha Uzazi na Malezi bora (UMATI) kinatoa huduma rafiki kwa makundi haya ili kupunguza hata maambukizi mapya ya ugonjwa wa Virusi Vya Ukimwi”, alisema.

Jumla ya vituo saba vimekuwa vikitoa huduma ya afya kwa makundi hayo yaliyopo katika hatari ya kupata VVU ambapo huduma hizo hutolewa na watoa huduma waliopata mafunzo maalum kulingana na mwongozo wa utoaji wa huduma husika.


Hata hivyo Midelo alieleza kuwa hadi sasa Manispaa ina jumla ya wateja 160 waliosajiliwa katika huduma hizo ambapo kati yao wanaume ni 120 na wanawake ni 40 na kwamba  wote hao wamepima VVU na kati yao wateja 30 wamegundulika kuwa na maambukizo hayo.

No comments: