Friday, May 19, 2017

MAKATIBU MAHSUSI HAPA NCHINI WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA KUZINGATIA MAADILI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia kwenye mkutano wa mwaka wa tano wa Chama cha Makatibu Mahususi Tanzania (TAPSEA) uliofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Jakaya Kikwete, mjini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe waliohudhuria Mkutano mkuu wa Chama Cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 
Na Mwandishi wetu,
Dodoma.

MAKAMU wa Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Makatibu Mahsusi hapa nchini kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuacha tabia ya kutoa siri za ofisi zao, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Samia Suluhu Hassan alitoa kauli hiyo leo wakati anafungua mkutano wa tano wa Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania, kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete mji Dodoma.

Alisisitiza kuwa uadilifu na uaminifu ndio njia pekee ya kuaminiwa na viongozi wao, hivyo ni muhimu kwa makatibu hao kufanya kazi kwa bidii na ubunifu mkubwa katika maeneo yao ya kazi.


Makamu wa Rais pia aliwahimiza makatibu mahsusi kufanya tathmini ya utendaji wao wa kazi za kila siku na wawe tayari katika kujifunza mbinu mpya za utendaji zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia.

“Sote tunafahamu kuwa dunia imekuwa ni kijiji kutokana na utandawazi unaoletwa na mifumo ya teknolojia, hivyo kutokana na mabadiliko haya hamna budi nanyi kubadilika na kwenda na wakati ili msiangaliwe kwa mtazamo hasi wa kuwa wapiga chapa tu”, alisema.

Kuhusu uanzishwaji wa Shahada ya Uhazili, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia makatibu hao kuwa serikali imekubali kuanzisha shahada hiyo ambapo masomo yake yataanza mapema mwezi wa tisa mwaka huu, kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania katika mikoa ya Dar es Salaam na Tabora.

Pia amewahimiza kuchangamkia fursa hiyo kwa ajili ya kujiendeleza kielimu kwa kuzingatia kuwa elimu haina mwisho.

Kwa upande wake, Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki alisema kwamba serikali inafanyia kazi baadhi ya kero zinazowakabili makatibu mahsusi ikiwemo kuboresha maslahi ya kada ya uhazili nchini.

Alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha kada hiyo pamoja na watumishi wengine, wanapata maslahi bora ambayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza ufanisi wa kazi.



No comments: