Tuesday, May 2, 2017

MWENYEKITI AWATAKA WATUMISHI WAONDOKANE NA TABIA YA WIZI MALI ZA UMMA

Na Kassian Nyandindi,   
Mbinga.

KUFUATIA kufukuzwa kazi kwa baadhi ya watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ambrose Nchimbi amewataka watumishi wengine waliopo katika wilaya hiyo waondokane na tabia ya wizi wa mali za umma na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.

“Taswira mpya ni kufanya kazi kwa misingi ya utawala bora inayotaka serikali hii ya awamu ya tano na sio muda mwingi kufikiria vitendo viovu ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi wetu”, alisema.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha juzi kikao cha baraza la Madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo.


Nchimbi alitoa rai kwa watumishi hao kwamba hivi sasa wanapaswa kubadilika na sio kila siku wanakuwa ni watu ambao wanafanya makosa kwa makusudi huku wakijiua kwamba wanaumiza wananchi.

Alisisitiza kuwa yeye na Madiwani wenzake wamefikia hatua ya kuwafukuza kazi watumishi wanne waliobainika kufanya makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umma ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

“Madiwani tumefanya hivi kuweza kutoa fundisho kwa wale wengine waliobaki ili waweze kufanya kazi vizuri kwa misingi bora na taratibu zilizowekwa na serikali, hatutaki kumuona mtumishi anakuwa na tabia ya wizi na udanganyifu katika utendaji wake wa kazi za kila siku za utumishi wa umma”, alisema.

Vilevile aliwataka pia Madiwani wahakikishe kwamba wajitambue katika nafasi zao walizonazo kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi kwenye maeneo yao ili iweze kujengwa kwa viwango vinavyokubalika.

Pamoja na mambo mengine watumishi waliofukuzwa kazi katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga kuwa ni aliyekuwa afisa mtendaji wa kata ya Kitura, Daniel Komba ambaye amefukuzwa kazi kutokana na kufanya matendo kinyume na dhamira njema ambapo alifoji risiti za marejesho ya fedha shilingi 350,000 ambazo ni michango ya wananchi wa kata hiyo.

Imebainishwa kuwa fedha hizo walikuwa wamechanga wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao ambapo alizitafuna kwa manufaa yake binafsi na halmashauri ilipofanya ufuatiliaji wa kina ilibaini kwamba risiti aliyoitumia kukusanyia fedha hizo haikuwa risiti halali ya serikali.


Vilevile wengine ni Ramadhan Mang’una ambaye ni afisa kilimo msaidizi, Allan Ndunguru afisa mtendaji wa kijiji cha Ulima na Michael Nakitundu naye ni afisa mtendaji wa kijiji cha Ulolela ambao nao walishiriki kufanya ubadhirifu wa mali za umma katika vijiji hivyo.

No comments: