Thursday, June 30, 2016

WANANCHI MBALATSE MAKETE WALALAMIKIA ARDHI YAO KUPORWA NA MWEKEZAJI



Na Kassian Nyandindi,

Njombe.

WANANCHI wa kata ya Mbalatse wilaya ya Makete mkoa wa Njombe, wamemuomba Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuona umuhimu wa kuingilia kati mgogoro uliopo kati yao na mwekezaji wa Kampuni ya Silverlands Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Iringa, ambaye anadaiwa kwamba amepora ardhi yao zaidi ya hekta 3,000 ambazo zilikuwa zikiwasaidia kuzalisha mazao ya aina mbalimbali.

Aidha kufuatia ardhi hiyo kuchukuliwa na mwekezaji huyo, wananchi hao wanakosa maeneo ya kulima mazao ya chakula na biashara jambo ambalo hivi sasa baadhi yao wanalazimika kwenda kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji kulima mazao hayo.

William Lukuvi.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wananchi hao walifafanua kuwa miaka iliyopita kwa muda mrefu walikuwa wakilima mahindi kwa wingi katika eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ludodolela, ambalo lina rutuba tofauti na maeneo mengine yaliyopo kwenye kata hiyo.

Aloyce Chaula mkazi wa kijiji cha Mbalatse alifafanua kuwa tangu kuzaliwa kwake miaka ya 60 iliyopita wazazi wake pamoja na wananchi wengine wa kata hiyo walikuwa na mashamba yao katika eneo hilo ambalo amepewa mwekezaji, bila wananchi kushirikishwa hivyo wanaiomba serikali kupitia Wizara hiyo kunusuru hali hiyo ili wananchi wa kata hiyo waweze kurejeshewa mashamba yao.

“Ndugu waandishi wa habari mnaliona kundi hili kubwa la wananchi wakilalamikia kuporwa maeneo yao, kwani awali huyu mwekezaji alikuja hapa kwetu kijijini kuomba eneo dogo kwa muda kwa ajili ya kufanya majaribio ya kupanda mbegu za zao la shairi, lakini tuna mshangaa ghafla amemilikishwa eneo kubwa na sisi wazawa tumefukuzwa huku akiendelea na uzalishaji wa zao hili la shairi”, alisema Chaula.

Tuesday, June 28, 2016

LIKWERA WAENDELEA KUNUFAIKA NA MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII

Elimu juu ya matumizi bora fedha za TASAF kwa wananchi imekuwa ikitolewa mara kwa mara kwa wanufaika, ili waweze kuondokana na umaskini. Katika picha ni Justiner Sigera ambaye ni mwezeshaji wa mfuko huo akiwaelimisha hivi karibuni wanufaika wa kijiji cha Mkako wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,

Mbinga. 

KAYA maskini zilizopo katika kijiji cha Likwera kata Nyoni Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameweza kunufaika na mpango wa kunusuru kaya hizo kwa kupewa fedha shilingi milioni 3,925,000 na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu, kwa ajili ya kuendeshea miradi ya ufugaji bora wa kuku, nguruwe na mbuzi.

Husna Chiponda ambaye ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho alisema kuwa jumla ya kaya 91 zimewezeshwa fedha hizo, ambazo wamelipwa kwa awamu ya mwisho kwa lengo la kuwawezesha waweze kujikwamua kimaisha na kuondokana na umaskini uliokithiri miongoni mwao.

Aidha aliongeza kuwa kwa upande wa sekta ya elimu, watoto wa shule za msingi wamenunuliwa mahitaji ya shule na kwamba wa sekondari wamelipiwa ada na kupewa mahitaji ya aina mbalimbali, kama vile sare za shule, madaftari na kalamu za kuandikia.

KAMPUNI YA ILYANA YATOA MSAADA WA MADAWATI KWA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI NAMTUMBO MKOANI RUVUMA



Na Kassian Nyandindi,

Songea.

WANANCHI wa kata ya Namtumbo wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamepongeza jitihada zinazofanywa na Kampuni ya Ilyana iliyopo mkoani humo, kwa kutoa msaada wa madawati kwa shule za msingi na sekondari ambazo zilikuwa zinakabiliwa na tatizo la upungufu madawati ya kukalia wanafunzi wanapokuwa darasani.

Khalfan Kigwenembe ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayofanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka Songea kwenda Dar es Salaam, alisema kuwa msaada wa madawati 220 yametolewa kwa shule hizo ambapo imekuwa ni kawaida yao kutoa michango ya aina mbalimbali kwa wananchi wa kata hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mjini hapa, Mkurugenzi huyo wa Ilyana alisema kuwa anayaomba makampuni mengine ambayo yamewekeza katika mkoa huo waige mfano kama huo katika kuisaidia jamii, ili iweze kuondokana na kero mbalimbali wanazokabiliana nazo.

Sunday, June 26, 2016

BREAKING NEWS: RAIS DKT. JOHN MAGUFULI ATEUA WAKUU WA WILAYA WAPYA 139 NA KUFANYA MABADILIKO KWA WAKUU WA MIKOA

Rais Dkt. John Magufuli.
IKULU, JIJINI DAR ES SALAAM.
 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya mabadiliko madogo katika safu ya wakuu wa mikoa na amewateua wakuu wa wilaya 139. 

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika mabadiliko hayo Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Bi. Zainab R. Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. 

Bi. Zainab R. Telack anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Anna Kilango Malecela ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. 

Rais Magufuli pia amemteua Dkt. Binilith Satano Mahenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma. 

Dkt. Binilith Satano Mahenge anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Said Thabit Mwambungu ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu Dar es salaam ambako atapangiwa majukumu mengine. 

Aidha, Rais Magufuli amemteua Dkt. Charles F. Mlingwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Dkt. Charles F. Mlingwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Stanslaus Magesa Mulongo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Wakuu wapya wa mikoa walioteuliwa wataapishwa tarehe 29 Juni, 2016 saa tatu kamili asubuhi Ikulu Jijini Dar es salaam na mara baada ya kuapishwa watakula kiapo cha maadili ya uongozi.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 26 Juni, 2016 amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 139.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi amesema katika uteuzi huo Rais Magufuli amezingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na umri ambapo kwa wale ambao umri wao ni zaidi ya miaka 60 ameamua wastaafu.

Mhe. Rais amewashukuru sana kwa utumishi wao mzuri na amesema pale ambapo itahitajika, serikali itaendelea kuwatumia katika majukumu mengine.

Katika uteuzi huo, Wakuu wa Wilaya waliopo sasa ambao wamebaki katika nafasi zao ni 39. Pia Rais Magufuli amewateua Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri 22 kuwa Wakuu wa Wilaya kutokana na utendaji wao mzuri.

Aidha, nafasi 78 za uteuzi wa Wakuu wa wilaya zimejazwa na watanzania wengine ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza wengi wao wakiwa ni vijana, wenye elimu ya kutosha na uzoefu katika maeneo mbalimbali.

Walioteuliwa kuwa wakuu wa wilaya ni kama ifuatavyo (Orodha imepangwa kulingana na mikoa)

ARUSHA
1. Arusha - Mrisho Mashaka Gambo
2. Arumeru - Alexander Pastory Mnyeti
3. Ngorongoro - Rashid Mfaume Taka
4. Longido - Daniel Geofrey Chongolo
5. Monduli - Idd Hassan Kimanta
6. Karatu - Therezia Jonathan Mahongo

DAR ES SALAAM
1. Kinondoni - Ally Hapi
2. Ilala - Sophia Mjema
3. Temeke - Felix Jackson Lyaviva
4. Kigamboni - Hashim Shaibu Mgandilwa
5. Ubungo - Hamphrey Polepole

DODOMA
1. Chamwino - Vumilia Justine Nyamoga
2. Dodoma - Christina Solomon Mndeme
3. Chemba - Simon Ezekiel Odunga
4. Kondoa - Sezeria Veneranda Makutta
5. Bahi - Elizabeth Simon
6. Mpwapwa - Jabir Mussa Shekimweli
7. Kongwa - John Ernest Palingo

GEITA
1. Bukombe - Josephat Maganga
2. Mbogwe - Matha John Mkupasi
3. Nyang'wale - Hamim Buzohera Gwiyama
4. Geita - Herman C. Kipufi
5. Chato - Shaaban Athuman Ntarambe

IRINGA
1. Mufindi - Jamhuri David William
2. Kilolo - Asia Juma Abdallah
3. Iringa - Richard Kasesela

KAGERA

1. Biharamulo - Saada Abraham Mallunde
2. Karagwe - Geofrey Muheluka Ayoub
3. Muleba - Richard Henry Ruyango
4. Kyerwa - Col. Shaban Ilangu Lissu
5. Bukoba - Deodatus Lucas Kinawilo
6. Ngara - Lt. Col. Michael M. Mtenjele
7. Missenyi - Lt. Col Denis F. Mwila

KATAVI
1. Mlele - Rachiel Stephano Kasanda
2. Mpanda - Lilian Charles Matinga
3. Tanganyika - Saleh Mbwana Mhando

KIGOMA
1. Kigoma - Samsoni Renard Anga
2. Kasulu - Col. Martin Elia Mkisi
3. Kakonko - Col. Hosea Malonda Ndagala
4. Uvinza - Mwanamvua Hoza Mlindoko
5. Buhigwe - Col. Elisha Marco Gagisti
6. Kibondo - Luis Peter Bura

KILIMANJARO
1. Siha - Onesmo Buswelu
2. Moshi - Kippi Warioba
3. Mwanga - Aaron Yeseya Mmbago
4. Rombo - Fatma Hassan Toufiq
5. Hai - Gelasius Byakanwa
6. Same - Rosemary Senyamule Sitaki

LINDI

1. Nachingwea - Rukia Akhibu Muwango
2. Ruangwa - Joseph Joseph Mkirikiti
3. Liwale - Sarah Vicent Chiwamba
4. Lindi - Shaibu Issa Ndemanga
5. Kilwa - Christopher Emil Ngubiagai

MANYARA

1. Babati - Raymond H. Mushi
2. Mbulu - Chelestion Simba M. Mofungu
3. Hanang' - Sara Msafiri Ally
4. Kiteto - Tumaini Benson Magessa
5. Simanjiro - Zephania Adriano Chaula

MARA
1. Rorya - Simon K. Chacha
2. Serengeti - Emile Yotham Ntakamulenga
3. Bunda - Lydia Simeon Bupilipili
4. Butiama - Anarose Nyamubi
5. Tarime - Glodious Benard Luoga
6. Musoma - Dkt. Vicent Anney Naano

MBEYA
1. Chunya - Rehema Manase Madusa
2. Kyela - Claudia Undalusyege Kitta
3. Mbeya - William Ntinika Paul
4. Rungwe - Chalya Julius Nyangidu
5. Mbarali - Reuben Ndiza Mfune

MOROGORO
1. Gairo - Siriel Shaid Mchembe
2. Kilombero - James Mugendi Ihunyo
3. Mvomero - Mohamed Mussa Utali
4. Morogoro - Regina Reginald Chonjo
5. Ulanga - Kassema Jacob Joseph
6. Kilosa - Adam Idd Mgoyi
7. Malinyi - Majula Mateko Kasika


MTWARA

1. Newala - Aziza Ally Mangosongo
2. Nanyumbu - Joakim Wangabo
3. Mtwara - Dkt. Khatibu Malimi Kazungu
4. Masasi - Seleman Mzee Seleman
5. Tandahimba - Sebastian M. Walyuba

MWANZA

1. Ilemela - Dkt. Leonald Moses Massale
2. Kwimba - Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon
3. Sengerema - Emmanuel Enock Kipole
4. Nyamagana - Mary Tesha Onesmo
5. Magu - Hadija Rashid Nyembo
6. Ukerewe - Estomihn Fransis Chang'ah
7. Misungwi - Juma Sweda

NJOMBE

1. Njombe - Ruth Blasio Msafiri
2. Ludewa - Andrea Axwesso Tsere
3. Wanging'ombe - Ally Mohamed Kassige
4. Makete - Veronica Kessy

PWANI
1. Bagamoyo - Alhaji Majid Hemed Mwanga
2. Mkuranga - Filberto H. Sanga
3. Rufiji - Juma Abdallah Njwayo
4. Mafia - Shaibu Ahamed Nunduma
5. Kibaha - Asumpter Nsunju Mshama
6. Kisarawe - Happyness Seneda William
7. Kibiti - Gulamu Hussein Shaban Kifu

RUKWA

1. Sumbawanga - Dkt. Khalfan Boniface Haule
2. Nkasi - Said Mohamed Mtanda
3. Kalambo - Julieth Nkembanyi Binyura

RUVUMA
1. Namtumbo - Luckness Adrian Amlima
2. Mbinga - Cosmas Nyano Nshenye
3. Nyasa - Isabera Octava Chilumba
4. Tunduru - Juma Homela
5. Songea - Polet Kamando Mgema

SHINYANGA
1. Kishapu - Nyambonga Daudi Taraba
2. Kahama - Fadhili Nkulu
3. Shinyanga - Josephine Rabby Matiro

SIMIYU

1. Busega - Tano Seif Mwera
2. Maswa - Sefu Abdallah Shekalaghe
3. Bariadi - Festo Sheimu Kiswaga
4. Meatu - Joseph Elieza Chilongani
5. Itilima - Benson Salehe Kilangi

SINGIDA
1. Mkalama - Jackson Jonas Masako
2. Manyoni - Mwembe Idephonce Geofrey
3. Singida - Elias Choro John Tarimo
4. Ikungi - Fikiri Avias Said
5. Iramba - Emmanuel Jumanne Luhahula

SONGWE
1. Songwe - Samwel Jeremiah
2. Ileje - Joseph Modest Mkude
3. Mbozi - Ally Masoud Maswanya
4. Momba - Juma Said Irando

TABORA
1. Nzega - Geofrey William Ngudula
2. Kaliua - Busalama Abel Yeji
3. Igunga - Mwaipopo John Gabriel
4. Sikonge - Peres Boniphace Magiri
5. Tabora - Queen Mwashinga Mlozi
6. Urambo - Angelina John Kwingwa
7. Uyui - Gabriel Simon Mnyele

TANGA
1. Tanga - Thobias Mwilapwa
2. Muheza - Mhandisi Mwanaisha Rajab Tumbo
3. Mkinga - Yona Lucas Maki
4. Pangani - Zainab Abdallah Issa
5. Handeni - Godwin Crydon Gondwe
6. Korogwe - Robert Gabriel
7. Kilindi - Sauda Salum Mtondoo
8. Lushoto - Januari Sigareti Lugangika


Wakuu wote wa Wilaya walioteuliwa wanapaswa kufika Ikulu Dar es salaam siku ya Jumatano tarehe 29 Juni, 2016 saa tatu kamili asubuhi kwa ajili ya kiapo cha maadili ya uongozi na maelekezo mengine kabla ya kuapishwa na wakuu wa mikoa watakaporejea katika mikoa yao.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Juni, 2016.

Saturday, June 25, 2016

DC TUNDURU APOKEA MSAADA WA SHILINGI MILIONI 2.5 KWA AJILI YA KUBORESHA MAZINGIRA YA KUSOMEA WANAFUNZI

Upande wa kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,  Agnes Hokororo akipotea hundi yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 kutoka kwa Meneja wa sheria na usuluhishi wa kampuni ya Export Trading Group (ETG) Nasser Mansour, katika hafla fupi iliyofanyika juzi katika ofisi za kiwanda cha kubangulia korosho mjini hapa.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo amewataka wafanya biashara na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo kujitokeza na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za wilaya hiyo, ambazo zimekuwa chakavu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi.

Hokororo alitoa wito huo juzi, alipokuwa akipokea msaada wa shilingi milioni 2.5 kutoka kwa Meneja wa sheria na usuluhishi wa kampuni ya Export Trading Group (ETG) Nasser Mansour, katika hafla fupi iliyofanyika katika  kiwanda cha kubangua Korosho kinachofahamika kwa jina la Korosho Afrika Limited kilichopo mjini hapa.

Alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa wakati muafaka huku akiahidi kuzisimamia kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, zinatumika kwa ajili ya kufanyia kazi iliyolengwa.

Thursday, June 23, 2016

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO ACHARUKA JUU YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA AITAKA MAMLAKA HUSIKA KUCHUKUA HATUA

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho watatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wenzake wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, mara baada ya kufanya ufunguzi wa mdahalo wa athari na mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa shirika la MWECO ambaye anaendesha mafunzo hayo, Terdey Mhagama. 

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Chande Nalicho akisisitiza jambo kwa kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha kuharibu vyanzo vya maji, ikiwemo suala la ukataji miti na uchomaji misitu hovyo.

Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo, Shida Kapata akichangia mada katika mafunzo hayo na kusisitiza wanawake wenzake wilayani Namtumbo kwenda kuelimisha jamii, juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira na kuacha tabia ya uharibifu wa vyanzo vya maji. (Picha zote na Muhidin Amri, Namtumbo)
Na Kassian Nyandindi,

Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ametoa agizo kwa kuitaka mamlaka husika wilayani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu waliovamia vyanzo vya maji, kutokana na wilaya hiyo hivi sasa kukabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.

Aidha ameagiza pia waharibifu hao wa mazingira, wanapaswa kufikishwa Mahakamani ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuharibu mazingira, ikiwemo ukataji wa miti hovyo.

Tumaini Mgaya Ofisa maendeleo ya jamii Namtumbo, akisisitiza jambo kwenye mafunzo hayo.
Nalicho alisema kuwa tangu enzi za mababu zetu walikuwa wakikemea tabia hii ya uharibifu wa mazingira, hivyo kuna kila sababu kwa jamii kurithi tabia hiyo ili kuweza kuepukana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi, ambalo linahatarisha usalama wa maendeleo ya viumbe hai hapa duniani.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo, Nalicho lilitolewa juzi alipokuwa akifungua mdahalo wa athari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, uliofanyika ukumbi wa Bikira Maria wa Fatima, mjini hapa.

Tuesday, June 21, 2016

WANAWAKE WILAYANI NAMTUMBO WANUFAIKA NA MAFUNZO YA ATHARI NA CHANGAMOTO ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ali Mpenye akisisitiza jambo kwa Wanawake wa wilaya hiyo (hawapo pichani) ambao walikuwa wakishiriki mafunzo juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo aliwataka huko waendako wakawe mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii juu ya kukabiliana na hali hiyo ikiwemo utunzaji wa vyanzo vya maji na kuacha kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo. Upande wa kushoto ni Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la MWECO, Terdey Mhagama ambaye anaendesha mafunzo hayo ya siku mbili katika ukumbi wa Bikira Maria wa Fatima Parokia ya Namtumbo mjini hapa.  


Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Wanawake wa kutoka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika mafunzo hayo. (Picha zote na Muhidin Amri, Namtumbo.)
Na Kassian Nyandindi,

Namtumbo.

WILAYA ya Namtumbo na vitongoji vyake mkoani Ruvuma, inakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama jambo ambalo linasababisha wananchi wake washindwe kuendesha shughuli zao za kiuchumi ipasavyo, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wilaya hiyo.   

Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo inachangiwa na baadhi ya wananchi, kuharibu vyanzo vya maji kutokana na kukata miti hovyo na kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ali Mpenye alisema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya mradi wa athari na changamoto za madiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Namtumbo mjini hapa.

Mpenye alisema kuwa wilaya hiyo ambayo ina idadi ya watu 214,000 sehemu kubwa ya wananchi wake, wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji kitendo ambacho kinasababisha vianze kukauka na kupoteza uoto wake wa asili.

“Wale wote ambao wanafanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, tunawataka waondoke, kwa sababu wanaharibu mazingira na kutishia usalama wa maendeleo ya viumbe hai ikiwemo sisi wenyewe binadamu”, alisema Mpenye.

Alisema kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu wanaoharibu mazingira ambapo katika wilaya ya Namtumbo, tayari kuna barua za onyo zimesambazwa kwenye maeneo husika kwa ajili ya kuwataka watu waondoke kwenye vyanzo hivyo.

Thursday, June 16, 2016

WANANCHI WASHAURIWA KUWA NA MAZOEA YA KUTUNZA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI

Kiongozi wa mbio za Mwenge uhuru mwaka 2016, George Mbijima upande wa kulia akikabidhi chandarua chenye dawa kwa  mkazi wa kijiji cha Mbuji kata ya Mbuji wilayani Mbinga Sailice Komba ikiwa ni mpango wa halmashauri ya wilaya hiyo kutokomeza ugonjwa wa Malaria kwa wananchi wake, kati kati ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Venance Mwamengo. Tukio hilo la kukabidhi chandarua lilifanyika juzi wakati Mwenge huo ulipowasili wilayani hapa, kwa ajili ya kutembelea miradi ya aina mbalimbali ya kimaendeleo.


Na Muhidin Amri,
Mbinga.

WANANCHI mkoani Ruvuma, wamehimizwa kuwa na tabia ya kutunza miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa fedha nyingi, yenye lengo la kuharakisha kukua kwa uchumi wa  mkoa huo na taifa kwa jumla.

Aidha wametakiwa kuacha kuhujumu miradi hiyo, ili kuepusha uwezekanao wa kukatisha tamaa baadhi ya wahisani ambao  wanajitolea fedha zao nyingi kujenga miundombinu husika, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na changamoto zilizopo hasa katika utoaji wa huduma muhimu za kijamii.

Wito huo umetolewa juzi na kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa George Mbijima, alipokuwa akifungua zahanati ya kijiji cha Kihulila wilayani Mbinga ambayo ilijengwa  kwa  fedha za mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya hiyo, ili kuwaondolea kero wakazi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

WAVUVI NYASA WALIA NA HALMASHAURI KUPANDISHA BEI YA LESENI ZA UVUVI



Na Mwandishi wetu,
Nyasa.

WAKAZI wanaoishi katika mji mdogo wa Mbamba bay wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wamesema kwamba hivi sasa tangu kuanza kwa mfungo mtukufu wa mwezi wa Ramadhani wanashindwa  kula kitoweo cha samaki, kutokana na kuuzwa kwa bei ghali tofauti na miezi mingine ya kawaida.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu, baadhi ya wakazi hao walidai kuwa hali hiyo inatokana na kutoweka kwa samaki katika ziwa nyasa ambapo hivi sasa hawapatikani kwa urahisi, hivyo wavuvi hutumia  nafasi hiyo kuongeza bei mara dufu zaidi.

Walisema kuwa wilaya ya Nyasa upatikanaji wa mazao mengine ya jamii ya mboga mboga kama vile maharage, kunde, mbaazi na choroko imekuwa ni tatizo ambapo watu wengi hutegemea samaki pekee ikiwa ni mboga ya kila siku katika kuendeshea familia zao.

SENYI NGAGA AWATAKA WATENDAJI MBINGA KUSIMAMIA MAZAO YA WAKULIMA


Na Muhidin Amri,

Mbinga.

WAKULIMA katika kata ya Litumbandyosi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuandaa sheria kali itakayowabana wafanyabiashara kuacha tabia ya kununua mazao ya wakulima, kwa kutumia vipimo haramu (lumbesa) ambapo hununua kwa bei ndogo isiyolingana na gharama ya uzalishaji.

Senyi Ngaga.
Wakulima hao walisema hayo kwa nyakati tofauti, wakidai kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa na tabia ya kwenda vijijini hasa mashambani na kutumia vipimo visivyokubalika kisheria kama vile bakuri na ndoo, kwa ajili ya kununua mazao  kama vile mpunga na mahindi  jambo ambalo huchangia kuwanyonya wakulima na kuwaacha maskini, licha ya kazi kubwa wanayofanya kila mwaka.

Aidha walieleza kuwa kutokana na kuwa na hali ngumu ya maisha ikiwemo suala la upatikanaji wa masoko, wamekuwa wakati mwingine wakilazimika kuuza mazao yao kwa mtindo huo wa vipimo wanavyotumia walanguzi hao ili waweze kujikimu kimaisha ikiwemo suala la kupeleka watoto wao shule.

PAD: UTEKELEZAJI SERA ZA WAZEE BADO NI TATIZO



Na Muhidin Amri,
Songea.

SHIRIKA lisilokuwa la serikali ambalo linahudumia wazee katika mikoa ya  Ruvuma, Iringa na Njombe (PAD) limesema kuwa bado kuna tatizo kubwa la utekelezaji wa sera za wazee katika mikoa hiyo kutokana na taratibu husika zilizowekwa kuhudumia watu hao, kutosimamiwa ipasavyo na kufikia hatua wazee kukosa haki zao za msingi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Isihaka Msigwa alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo ameitaka jamii kuwapa kipaumbele  wazee kila wanapofika katika maeneo ya kutolea huduma kama vile hospitali  na kwenye vyombo vya usafiri, kama vile magari ya kubeba abiria (daladala).

Msigwa alisema kuwa kukosekana kwa mapango mkakati wa utekelezaji wa sera ya  taifa ya wazee, kumesababisha hata vituo vya kulea watu hao kuwa vichache na miundombinu yake kutokuwa rafiki kwao.

Sunday, June 12, 2016

WILAYA YA MBINGA YATEKELEZA AGIZO LA RAIS MAGUFULI YATENGA MILIONI 475.8 KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MADAWATI

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa,  George Mbijima akiangalia ubora wa meza na madawati juzi katika kijiji cha Mbuji wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kabla ya kusambazwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WILAYA ya Mbinga mkoani Ruvuma, imetenga zaidi ya shilingi milioni 475.8 kwa ajili ya  kukabiliana na upungufu wa madawati, meza na viti  kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. John Magufuli, alilotoa hivi karibuni wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa  na kuzitaka halmashauri zote hapa nchini kuhakikisha zinamaliza tatizo hilo.

Aidha wilaya hiyo tayari imefanikiwa kutengeneza madawati 6,134 kati ya madawati 12,952 ambapo kwa shule za msingi madawati yaliyokamilika ni 3,634 na shule za sekondari 2,500 sawa na asilimia 47.6 ya lengo kwa gharama ya shilingi milioni 169 na tayari yamekwisha sambazwa kwenye shule husika, huku mchakato wa kumaliza madawati 5,510 kwa shule za msingi 3,810 na sekondari 1,700 ukiwa katika hatua ya mwisho kukamilika kwake.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini, Venance Mwamengo wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, George Mbijima katika kijiji cha Mbuji kata ya Mbuji wilayani humo.

Kwa mujibu wa Mwamengo alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha ni gharama za kununulia mashine za kuranda, kukata na kukunja vyuma, mashine za kupasulia mbao, umeme na gharama zingine ndogo ndogo na kwamba madawati hayo yametengenezwa kwa kutumia mbao pamoja na chuma ili yaweze kuwa imara tofauti na madawati yanayotengenezwa kwa mbao tupu, ambayo huharibika kwa haraka na hayadumu kwa muda mrefu.

NYASA WALIA NA BAADHI YA VIGOGO WA SERIKALI WALIOPEWA VIWANJA NA KUTOVIENDELEZA KWA MUDA MREFU



Na Muhidin Amri,
Nyasa.

HALMASHAURI ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, imetakiwa kuongeza kasi ya kupima viwanja katika mji mdogo wa Mbamba bay wilayani humo kutokana na mji huo kukua kwa haraka na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu wanaokwenda huko, kwa lengo la kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kuwekeza katika sekta ya uchumi.

Hayo yalisemwa mwishoni wa wiki na baadhi ya wakazi wa mji  wa Mbamba bay, walipokuwa wakizungumzia juu ya ukosefu wa huduma muhimu kama vile hoteli za kisasa na huduma ya usafiri  wa uhakika, kutoka kwenye mji huo na maeneo mengine ya  wilaya jirani ya Mbinga.

Samwel Sogolo na Mariam Majika kwa nyakati tofauti walifafanua kuwa licha ya serikali kuanza kupima viwanja na maeneo ya wazi, kwa ajili ya makazi na shughuli mbalimbali bado kunahitajika kasi kubwa ya upimaji na utambuzi wa maeneo hayo ambapo kufanya hivyo kutasaidia  watu watakaopata viwanja hivyo kuviendeleza kwa kujenga nyumba za kisasa, ikiwemo kuwekeza katika miradi ya  kiuchumi.

Saturday, June 11, 2016

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE APONGEZA HALMASHAURI YA MBINGA USIMAMIZI MZURI KATIKA SEKTA YA ELIMU

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru George Mbijima, akiangalia ubora wa meza na madawati ya kukalia wanafunzi darasani katika kijiji cha Mbuji wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, kabla ya kusambazwa katika shule mbalimbali za msingi na sekondari wilayani humo.

Mratibu elimu kata katika kata ya Litura Halmashauri ya wilaya ya Mbinga vijijini mkoani Ruvuma, Nicodem Hyera akijaribu kuwasha moja kati ya pikipiki zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya kuwawezesha Waratibu elimu kata wanaofanya kazi katika mazingira magumu  ziweze kuwasaidia kufuatilia maendeleo ya elimu kwa shule za msingi na sekondari wilayani humo. (Picha zote na Muhidin Amri Mbinga)


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imepata zawadi ya shilingi milioni 331,252,720 baada ya kukidhi vigezo vitatu vya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo, katika sekta ya elimu wilayani humo.

Vigezo vilivyoifanya halmashauri hiyo iweze kupata tuzo hiyo ni kupanga walimu katika shule zake kulingana na mahitaji husika, kuandaa takwimu za shule zote na kuziweka kwenye mtandao pamoja na kutuma fedha za ruzuku ya uendeshaji kwa wakati kwenye shule husika.

Ofisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Samwel Komba alisema hayo wakati alipokuwa akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa, George Mbijima juu ya mikakati ya kukuza elimu katika shule za msingi wilayani humo.

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBINGA YAENDELEA KUTEKELEZA ZOEZI LA UFUNGAJI MASHINE ZA EFD'S



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba, Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma inadhibiti vyanzo vyake vya mapato kupitia vituo vya kukusanyia ushuru wa mazao, hivi sasa imenunua mashine za Kieletroniki (EFD’S) ambazo zitatumika kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Ujenzi wa jumla ya vituo 13 vya kukusanyia ushuru huo vilivyopo wilayani humo, vitafungwa mashine hizo ambapo jumla ya shilingi milioni 400,000,000 kutoka mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, zitatumika katika kukamilisha kazi ya ujenzi wa vituo hivyo na kufungwa mashine za EFD’S.

Hayo yalisemwa juzi na Mweka hazina wa wilaya ya Mbinga, Joseph Mazito wakati alipokuwa akisoma taarifa ya uzinduzi wa kituo cha kukusanyia ushuru wa mazao kilichopo kijiji cha Kihulila wilayani humo, kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima.

HALMASHAURI YA WILAYA MBINGA MWENGE WA UHURU WAZINDUA MIRADI YENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 701.6 VIONGOZI WATAKIWA KUTEKELEZA MIRADI YA WANANCHI KWA WAKATI

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, Oscar Yapesa upande wa kushoto akikabidhi Mwenge wa uhuru jana kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo mara baada ya kumaliza mbio zake katika mji wa Mbinga, ambapo Mwenge huo sasa ulikuwa ukiendelea kupelekwa katika miradi mbalimbali ya wilaya hiyo ya Mbinga.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima amewataka viongozi waliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi, zinafanya kazi iliyolengwa ipasavyo ili ziweze kuleta tija katika jamii.

Aidha aliagiza kwamba miradi hiyo inapaswa kutekelezwa kwa wakati, ili kuweza kusaidia kuharakisha mipango mbalimbali ya kimaendeleo ambayo inalenga kuwaondolea umaskini wananchi.

Mbijima alisema hayo jana alipokuwa kwenye ziara ya mbio za Mwenge wa uhuru wilayani humo, ambapo jumla ya miradi saba yenye thamani ya shilingi milioni 701,652,180 Mwenge huo katika miradi hiyo baadhi yake umeweza kufanya kazi ya kuweka mawe ya msingi, kufunguliwa na kuzinduliwa.

Thursday, June 9, 2016

KUSILE RESTAURANT AND LODGE YAFUNGULIWA RASMI NA KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA

Mkurugenzi wa kampuni ya Ovans Construction Company Limited, ambao ni wamiliki wa Kusile Restaurant and Lodge, Valence Urio upande wa kulia akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru mara baada ya Kiongozi wa mbio za Mwenge George Mbijima kufungua rasmi hoteli hiyo iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma.

Msimamizi wa hoteli ya Kusile Restaurant and Lodge, Mary Thomas upande wa kushoto akisoma taarifa ya maendeleo juu ya ujenzi wa hoteli hiyo ya kisasa kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge, George Mbijima wa pili kutoka kulia. Wa pili kutoka kushoto ni mmiliki wa hoteli hiyo, Verena Urio.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijimi akiondoa kitambaa ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa hoteli ya kisasa ya Kusile Restaurant and Lodge iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma. (Picha zote na Muhidin Amri Mbinga)
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, George Mbijima amefungua mradi wa Hoteli ya kisasa iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa hoteli unaoukabili mji huo, yenye thamani ya shilingi milioni 110,000,000.

Akisoma taarifa ya mradi huo mbele ya Kiongozi wa mbio hizo za Mwenge, Mary Thomas ambaye ni msimamizi wa mradi huo alisema kuwa mradi huo ambao ni kitega uchumi yaani, “Kusile Restaurant and Lodge” ulibuniwa baada ya kuona mji huo, una tatizo la upatikanaji wa hoteli ya kisasa.

Mary alifafanua kuwa kufunguliwa kwa jengo hilo ni kuunga mkono jitihada za kimaendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais shupavu, John Magufuli katika kutengeneza ajira kwa vijana wa Mbinga na Watanzania wote kwa ujumla ili kuweza kuongeza kipato na kukuza uchumi.

“Ndugu kiongozi wa mbio hizi za Mwenge wa Uhuru, mradi huu umefanikiwa pia kuwawezesha wakulima wadogo wadogo 10 kuanzisha kilimo cha mboga mboga maalumu ambazo hazipatikani hapa Mbinga, hivyo kutengeneza soko la uhakika kwa mboga mboga hizo na zile za kawaida”, alisema Mary.

Wednesday, June 8, 2016

AKUTWA AMEFARIKI DUNIA HUKU UUME WAKE UKIWA UMEVESHWA KONDOMU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MTU mmoja ambaye ni mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Peter Christopher (35) amekutwa akiwa amefariki dunia huku sehemu zake za siri zikiwa zimevalishwa mpira wa kiume maarufu kwa jina la Kondomu ambayo ilikutwa ikiwa imekwisha tumika.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji zinasema kuwa mwili wa marehemu huyo ulikutwa hivi karibuni majira ya mchana kwenye pori lililopo eneo la Making’inda, kata ya Msamala mjini hapa.

Kamanda huyo alisema kuwa Christopher alikutwa amefariki dunia, mwili wake ukiwa hauna jeraha la aina yeyote badala yake alikutwa akiwa amevaa mpira huo kwenye uume wake, huku mpira mwingine ukiwa bado haujatumika ambao ulikutwa kwenye mfuko wake wa suruali ambayo ilikuwa kando kando ya mwili wake.

WALIMU SHULE SEKONDARI KITURA WALIA NA JENGO LA UTAWALA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JENGO la utawala ambalo hutumika na Walimu wa shule ya sekondari Kitura katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lina hali mbaya ambapo wakati wowote huenda likabomoka na kuleta madhara kwa watumiaji.

Miundo mbinu ya jengo hilo ambayo ni chakavu na imetengeneza nyufa, hivi sasa baadhi ya kuta zake zimeanza kubomoka na kuhatarisha usalama wa walimu wanaofundisha katika shule hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea shuleni hapo huku wakiomba majina yao yasitajwe gazetini, walimu hao walisema kuwa hata mazingira ya shule yao yamekuwa magumu ambapo vyoo vya wanafunzi na nyumba za walimu zilizopo hazikidhi mahitaji husika.

Tuesday, June 7, 2016

LITUHI NYASA WALALAMIKIA UGAWAJI CHAKULA CHA MSAADA KILICHOTOLEWA NA SERIKALI


Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

BAADHI ya Wananchi wa kijiji cha Kihuru na Nkaya katika kata ya Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo kwa kushindwa kusimamia ipasavyo ugawaji wa chakula cha msaada ambacho kimetolewa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo, ambao walikumbwa na maafa ya kuzolewa nyumba na mazao yao shambani.
Rais Dkt. John Magufuli.

Maafa hayo ambayo yalitokea Aprili 4 hadi 8 mwaka huu, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku nne mfululizo ambayo iliambatana na upepo mkali ambapo zaidi ya wananchi 1,000 walikosa mahali pa kuishi, kufuatia nyumba na mazao yao waliyolima shambani kuzolewa na mkondo mkubwa wa mafuriko ya maji ambao ulikuwa ukielekea ziwa Nyasa wilayani humo.

Wakizungumza kwa kuomba majina yao yasitajwe kwenye mtandao huu, walisema kuwa wameshangazwa na Ofisi hiyo ya Mkuu wa wilaya  kutosimamia  kwa karibu zoezi hilo la ugawaji wa mahindi hayo ambayo yametolewa na serikali tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu, ili yaweze kuwasaidia wahanga hao ambao wamekumbwa na mkasa huo.

Sunday, June 5, 2016

JENISTA MHAGAMA WAMTAKA AWATUMBUE WALIOKULA FEDHA ZA WATOTO WALEMAVU MBINGA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WAKATI serikali ya Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Magufuli ikifanya jitihada ya kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma kwa lengo la kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za umma hapa nchini, hali imekuwa kinyume kwa idara ya elimu msingi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo shilingi milioni 2.5 za watoto wenye ulemavu zinadaiwa kutafunwa na kulipana posho baadhi ya watumishi wa idara hiyo badala ya kwenda kufanya kazi iliyolengwa.


Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.
Fedha hizo zimechotwa kutoka sehemu ya shilingi milioni 6 ambazo zilitengwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kukarabati jengo la kusomea watoto hao shule ya msingi Kiwanjani iliyopo mjini hapa, kuwanunulia chakula, matibabu na manunuzi ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia pale wanapokuwa darasani.

Kwa mujibu wa vielelezo vinavyothibitisha juu ya fedha hizo kutumika kinyume na taratibu kwa watu kulipana posho ambavyo mwandishi wa habari hizi nakala yake anayo, vinabainisha kwamba ziliingizwa kwenye akaunti namba 61703700006 tawi la benki ya NMB ambayo ni ya shule hiyo wilayani humo.

Shule ya Kiwanjani ni moja kati ya shule za msingi zilizopo wilayani Mbinga, ambazo zinalea watoto wenye ulemavu na fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti hiyo Agosti 21 mwaka 2015, kwa cheki yenye namba 000008 wakati alipokuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga ambaye hivi sasa amehamishwa kwenda wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma.

MBINGA WAIOMBA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI KUPANUA MRADI WA MAJI

Mji wa Mbinga ambao hivi sasa unakua kwa kasi.


Na Muhidin Amri,
Mbinga.

WANANCHI wanaoishi katika mji wa Mbinga mkoani Ruvuma wameiomba serikali kupitia Wizara ya maji na Umwagiliaji, kuchukua hatua katika mipango yake kupanua mradi wa maji safi na salama katika mji huo, hatua ambayo itawezesha wananchi wengi kupata huduma ya maji safi na salama.

Ushauri huo ulitolewa na wananchi hao walipokuwa wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, kufuatia hivi sasa wamekuwa wakitumia muda mwingi kwenda umbali mrefu kutafuta huduma ya maji hayo kwa ajili ya matumizi mbalimbali majumbani kwao.

Walisema kuwa hali hiyo inatokana na miundombinu inayotumika sasa kuchakaa na wakati mwingine huharibika mara kwa mara, jambo ambalo limekuwa likiwafanya kupata maji kwa mgao na kuwa kero kubwa kwao.

HALMASHAURI KUKAMILISHA UJENZI SKIMU YA UMWAGILIAJI SANGAMABUNI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imesema kwamba, itaendelea kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa mfereji mkuu unaoleta maji shambani katika skimu ya umwagiliaji Sangamabuni, iliyopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilayani humo ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha zao la mpunga kupitia umwagiliaji wanaoufanya katika mradi huo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kuona kazi ya kilimo cha zao la mpunga, kinachofanywa na kikundi cha Sangamabuni kijijini humo.

“Hivi sasa tuna tatizo kubwa la ukosefu wa fedha katika halmashauri yetu ili tuweze kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi, lakini tunawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu mara tupatapo pesa tutaikamilisha ujenzi wake haraka iwezekanavyo”, alisema Mwamengo.

Saturday, June 4, 2016

AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA PIKIPIKI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

MAWAZO Jabili (24) ambaye ni fundi maarufu wa kutengeneza pikipiki aina ya Powertiller wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amefariki dunia katika ajali mbaya ya pikipiki aliyokuwa akiiendesha.

Aidha katika ajali hiyo pia fundi msaidizi wa marehemu huyo, aliyetambuliwa kwa jina la Abdalah Ngalibeyi naye amelazwa katika hospitali ya wilaya hiyo, akiwa hajitambui baada ya kunusurika kifo katika ajali hiyo. 

Mashuhuda wa tukio hilo walisema kuwa,  ajali hiyo ilitokea kijiji cha Msinji kilichopo kata ya Ligoma wilayani humo.

WANANCHI WAILALAMIKIA TANROADS KWA KUTOFANYIA MATENGENEZO BARABARA KWA MUDA MREFU



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANANCHI waishio katika kata ya Kitura wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wameulalamikia uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani humo kwa kushindwa kufanyia matengenezo kwa muda mrefu barabara ya kutoka kata ya Litembo hadi kijiji cha Nkili wilayani Nyasa, jambo ambalo limekuwa likisababisha kero kubwa kwao hasa pale wanaposafirisha wagonjwa au mazao yao kutoka shambani.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.

Barabara hiyo ambayo ina zaidi ya kilometa 30 walisema, kutokana na kuwa katika hali mbaya wamekuwa wakati mwingine wakilazimika kutumia jembe la mkono kuitengeneza, hasa nyakati za masika magari yao yanapokuwa yanakwama barabarani.

Malalamiko hayo yalitolewa juzi na wananchi hao, kwenye kikao cha baraza la kata kilichofanyika kwenye ofisi ya makao makuu ya kata ya Kitura wilayani Mbinga na kuhudhuriwa na Diwani wa kata hiyo, Alex Ngui ambacho kililenga kujadili maendeleo ya kata hiyo.

Thursday, June 2, 2016

SHULE YA MSINGI NGAPA TUNDURU WALIMU NA WANAFUNZI WAJISAIDIA PORINI



Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.


Na Steven Augustino,

Tunduru.

WANAFUNZI na walimu wa shule ya msingi Ngapa katika kata ya Ngapa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanajisaidia porini  kwa miaka miwili mfululizo sasa kufuatia shule hiyo kutokuwa na vyoo safi na salama, ambavyo vitawawezesha kwa ajili ya matumizi husika na utunzaji wa mazingira katika hali ya usafi kuzunguka shule hiyo.

Kufuatia hali hiyo shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 589 wanaosoma hapo, wanaishi katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya mlipuko kama vile homa za matumbo.

Vilevile walimu na wanafunzi hao wamekuwa wakiweka rehani maisha yao,  huenda wakashambuliwa na wanyama wakali wakiwemo chui, simba, fisi, mbweha na nyoka ambao hupatikana katika msitu uliopo jirani na shule hiyo wa kijiji cha Ngaga pale wanapoenda kujisaidia msituni humo.

ALIYEMUUA SHEKHE MSIKITI WA LIKWESO TUNDURU APANDISHWA KIZIMBANI



Na Steven Augustino,

Tunduru.

ALLY Mchumwa (45) ambaye ni mtuhumiwa wa tukio la mauaji ya Shekhe wa Msikiti wa kijiji cha  Likweso, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma amefikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili juu ya tukio hilo.

Habari zinaeleza kuwa, kabla ya mtuhumiwa huyo kutekeleza unyama huo alimuua kwa kumchoma kisu shingoni Shekhe, Seleman Mwarabu Selemani (45) katika tukio la fumanizi lililotokea Mei 22 mwaka huu.

Akimsomea shauri hilo la mauaji namba 4/2016 mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelaeli Jwagu alisema kuwa, tukio hilo lilitokea siku  hiyo majira ya saa 3.30 asubuhi katika eneo la mashamba ya Mkasandimbe yaliyopo tarafa ya Nakapanya, wilayani Tunduru.

Wednesday, June 1, 2016

WAUMINI TUNDURU KUSHIRIKI KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU MWANZA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

WAUMINI wa dhehebu la Roman Katoliki, kutoka Jimbo la Tunduru – Masasi mkoani Ruvuma wamepangwa kushiriki kongamano la kitaifa la Ekaristi takatifu na utoto mtakatifu, ambalo limepangwa kufanyika mkoani Mwanza Juni Mosi mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa kamati ya Kongamano hilo, Chrispin Mumba alipokuwa kwenye mahojiano maalumu, yaliyofanyika na mwandishi wetu katika ofisi za jimbo hilo.

Mumba alisema kuwa katika msafara huo kutakuwa na watoto wa Kipapa, mapadre na walei kutoka Parokia mbalimbali za Jimbo la Tunduru - Masasi. 

MKUU WA WILAYA YA MBINGA AWATAKA MADIWANI KUWA WAKALI JUU YA MATUMIZI FEDHA ZA SERIKALI



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

SENYI Ngaga ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, amewataka Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo kusimamia kikamilifu na kuwa wakali juu ya matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali, ili ziweze kufanya kazi husika na kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu huyo wa wilaya, Ngaga alipokuwa akizungumza na Madiwani hao kwenye kikao maalumu cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ((CAG) kwa mwaka fedha unaoishia Juni 30 mwaka 2015, ambapo Halmashauri ya Mbinga imepata hati yenye mashaka.
Senyi Ngaga, Mkuu wa wilaya ya Mbinga.

Ngaga alisema hayo kufuatia mapungufu na hoja mbalimbali zilizotolewa na CAG kwa Halmashauri hiyo, kufuatia kuwepo kwa matumizi ya fedha yasiyofuata miongozo na taratibu husika.

“Hoja hizi zilizotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ndugu zangu Madiwani zinapaswa kufanyiwa kazi mapema, vilevile muwe wakali juu ya matumizi na manunuzi ya fedha za serikali”, alisema Ngaga.

Alisema kuwa hategemei tena kuona mapungufu yaliyojitokeza katika mwaka huo yanajirudia tena kwa mwaka 2016/2017 na kwamba aliwataka kutumia nafasi zao za udiwani kutekeleza majukumu ya wananchi ipasavyo.