Tuesday, June 21, 2016

WANAWAKE WILAYANI NAMTUMBO WANUFAIKA NA MAFUNZO YA ATHARI NA CHANGAMOTO ZA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Ali Mpenye akisisitiza jambo kwa Wanawake wa wilaya hiyo (hawapo pichani) ambao walikuwa wakishiriki mafunzo juu ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ambapo aliwataka huko waendako wakawe mabalozi wazuri wa kuelimisha jamii juu ya kukabiliana na hali hiyo ikiwemo utunzaji wa vyanzo vya maji na kuacha kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo. Upande wa kushoto ni Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la MWECO, Terdey Mhagama ambaye anaendesha mafunzo hayo ya siku mbili katika ukumbi wa Bikira Maria wa Fatima Parokia ya Namtumbo mjini hapa.  


Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Wanawake wa kutoka wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, wakisikiliza kwa makini mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika mafunzo hayo. (Picha zote na Muhidin Amri, Namtumbo.)
Na Kassian Nyandindi,

Namtumbo.

WILAYA ya Namtumbo na vitongoji vyake mkoani Ruvuma, inakabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama jambo ambalo linasababisha wananchi wake washindwe kuendesha shughuli zao za kiuchumi ipasavyo, katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya wilaya hiyo.   

Aidha imeelezwa kuwa hali hiyo inachangiwa na baadhi ya wananchi, kuharibu vyanzo vya maji kutokana na kukata miti hovyo na kuendesha shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo hivyo.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Ali Mpenye alisema hayo leo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili ya mradi wa athari na changamoto za madiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, ambayo yamefadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Women Fund Tanzania (WFT) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Namtumbo mjini hapa.

Mpenye alisema kuwa wilaya hiyo ambayo ina idadi ya watu 214,000 sehemu kubwa ya wananchi wake, wamekuwa wakijishughulisha na shughuli za kilimo katika vyanzo vya maji kitendo ambacho kinasababisha vianze kukauka na kupoteza uoto wake wa asili.

“Wale wote ambao wanafanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji, tunawataka waondoke, kwa sababu wanaharibu mazingira na kutishia usalama wa maendeleo ya viumbe hai ikiwemo sisi wenyewe binadamu”, alisema Mpenye.

Alisema kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua watu wanaoharibu mazingira ambapo katika wilaya ya Namtumbo, tayari kuna barua za onyo zimesambazwa kwenye maeneo husika kwa ajili ya kuwataka watu waondoke kwenye vyanzo hivyo.


Vilevile aliwataka wanawake wilayani humo ambao wanashiriki mafunzo hayo kuwa mstari wa mbele, kuelimisha jamii iachane na shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira.

“Tatizo hili ni kubwa, lakini watu bado ni wabishi wanataka waendelee kulima mashamba yao katika vyanzo vya maji ninyi akina mama mnatakiwa muwe mabalozi wazuri wa kukemea hali hii kwa nguvu zote ili tuweze kuwa na maji ya kutosha ya kuendeshea shughuli zetu kiuchumi”, alisema.

Awali kwa upande wake, Terdey Mhagama Mkurugenzi mtendaji wa shirika la MWECO lisilokuwa la kiserikali hapa nchini, ambalo linajishughulisha na kujenga uwezo wa masuala ya kiuchumi kwa jamii hususani wanawake katika upatikanaji wa rasilimali za maji, uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira alisema kuwa mabadiliko hayo ya tabia nchi husababisha madhara makubwa kwa jamii na hata kuathiri kizazi cha sasa na baadaye.  

Mhagama alieleza kuwa ni takribani miongo mitatu sasa, dunia imekuwa ikikabiliwa na majanga anuwai ambayo husababisha hasara kubwa na upotevu wa mali na maisha ya watu, hivyo kuongezeka kasi ya watu kuathirika kiuchumi na kuwa maskini.

“Kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kunaathiri mfumo mzima wa hali ya hewa na mazingira kama vile ukataji wa miti hovyo, uvuvi mkubwa baharini usiozingatia utaalamu, uanzishwaji wa viwanda vikubwa vya kemikali na madini na matumizi mabaya ya ardhi kunasababisha mabadiliko ya tabia nchi”, alisema Mhagama.

Alisema kuwa hali hiyo inapojitokeza waathirika wakubwa ni wanawake ambao hupoteza muda mwingi kutafuta maji, na hivyo kuathiri utekelezaji wa shughuli zingine za kujipatia kipato na kujiletea maendeleo.

Pamoja na mambo mengine alibainisha kuwa katika nchi za Afrika, Tanzania ni nchi ambayo inaathirika zaidi na athari za mabadiliko ya tabia nchi ukizingatia kwamba ni wachangiaji wadogo wa tatizo hilo, hivyo kuna kila sababu kuwa mstari wa mbele kukemea hali hiyo kwa kuzitaka nchi zinazoongoza kuleta mabadiliko hayo, kupunguza madhara ili jamii isiweze kuathirika.

Hata hivyo kusudio la mradi huo wilayani Namtumbo, ni pamoja na kuunda mtandao wa wanawake katika eneo lililokusudiwa kwa kuwajengea uwezo na kushawishi kuongea kwa kupaza sauti zao katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, sanjari na kuendesha mdahalo wa pamoja kati ya wanawake na wadau wengine.

No comments: