Thursday, June 16, 2016

PAD: UTEKELEZAJI SERA ZA WAZEE BADO NI TATIZO



Na Muhidin Amri,
Songea.

SHIRIKA lisilokuwa la serikali ambalo linahudumia wazee katika mikoa ya  Ruvuma, Iringa na Njombe (PAD) limesema kuwa bado kuna tatizo kubwa la utekelezaji wa sera za wazee katika mikoa hiyo kutokana na taratibu husika zilizowekwa kuhudumia watu hao, kutosimamiwa ipasavyo na kufikia hatua wazee kukosa haki zao za msingi.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo, Isihaka Msigwa alisema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ambapo ameitaka jamii kuwapa kipaumbele  wazee kila wanapofika katika maeneo ya kutolea huduma kama vile hospitali  na kwenye vyombo vya usafiri, kama vile magari ya kubeba abiria (daladala).

Msigwa alisema kuwa kukosekana kwa mapango mkakati wa utekelezaji wa sera ya  taifa ya wazee, kumesababisha hata vituo vya kulea watu hao kuwa vichache na miundombinu yake kutokuwa rafiki kwao.


Alitolea mfano akisema kwamba hadi sasa idadi ya vituo vya kulelea wazee hapa nchini vipo 20 tu kwa nchi nzima na kwamba, katika masuala ya ugonjwa wa Ukimwi hayajawekewa sera ya taifa itakayosaidia kundi hilo ambalo kwa kiasi kikubwa huathirika na ugonjwa huo.

Msigwa ambaye pia ni Katibu mtendaji wa mtandao wa kinga ya jamii hapa nchini alifafanua kuwa, mapitio mengi  ya sera ya Ukimwi mwaka 2010 yameingiza kundi la wazee na kuelekeza namna wazee, watakavyoshughulikiwa lakini bado inawalenga kuwasaidia hasa watu wa kuanzia miaka 15 hadi 45.

Kwa upande wake pia aliishukuru serikali ya awamu ya tano, kwa kuunda Wizara itakayohusika na masuala ya wazee ambapo hivi sasa  wameanza kunufaika na matunda ya serikali, kwa kuwekewa chumba  maalum cha matibabu pale wanapokwenda kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali.

Alibainisha kwamba hapo awali kuna baadhi ya vitu vilikuwa vikisababisha sera ya wazee kushindwa kutekelezeka na kushindwa kupata huduma zao za msingi, licha ya taifa kutambua kwamba wameitumikia nchi hii katika mambo mengi ya kimaendeleo.

No comments: