Sunday, June 5, 2016

JENISTA MHAGAMA WAMTAKA AWATUMBUE WALIOKULA FEDHA ZA WATOTO WALEMAVU MBINGA



Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WAKATI serikali ya Rais wa awamu ya tano, Dkt. John Magufuli ikifanya jitihada ya kupambana na ubadhirifu wa fedha za umma kwa lengo la kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali za umma hapa nchini, hali imekuwa kinyume kwa idara ya elimu msingi wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, ambapo shilingi milioni 2.5 za watoto wenye ulemavu zinadaiwa kutafunwa na kulipana posho baadhi ya watumishi wa idara hiyo badala ya kwenda kufanya kazi iliyolengwa.


Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama.
Fedha hizo zimechotwa kutoka sehemu ya shilingi milioni 6 ambazo zilitengwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kukarabati jengo la kusomea watoto hao shule ya msingi Kiwanjani iliyopo mjini hapa, kuwanunulia chakula, matibabu na manunuzi ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia pale wanapokuwa darasani.

Kwa mujibu wa vielelezo vinavyothibitisha juu ya fedha hizo kutumika kinyume na taratibu kwa watu kulipana posho ambavyo mwandishi wa habari hizi nakala yake anayo, vinabainisha kwamba ziliingizwa kwenye akaunti namba 61703700006 tawi la benki ya NMB ambayo ni ya shule hiyo wilayani humo.

Shule ya Kiwanjani ni moja kati ya shule za msingi zilizopo wilayani Mbinga, ambazo zinalea watoto wenye ulemavu na fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti hiyo Agosti 21 mwaka 2015, kwa cheki yenye namba 000008 wakati alipokuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga ambaye hivi sasa amehamishwa kwenda wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma.


Baada ya fedha hizo kuingizwa katika akaunti hiyo, Kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Alphonce Mwamwile alichukua jukumu la kumwandikia barua Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kiwanjani, Analis Mapunda ya Septemba 3 mwaka jana ambayo ina kumbukumbu namba W/E/MB/12/43 akimtaka atoe sehemu ya fedha hizo shilingi milioni 2.5 kwa kumwidhinisha Afisa elimu maalumu, Sixbertha Kumburu azichukue na kwenda kulipana posho na maafisa wenzake wa ufuatiliaji na ukusanyaji takwimu mashuleni wilayani humo.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa baada ya kumwidhinisha afisa huyo, alikwenda shuleni hapo na kuandikiwa hundi ya malipo ambayo ilimwezesha kwenda benki hiyo ya NMB tawi la Mbinga, Septemba 7 mwaka 2015 na kutoa kiasi hicho cha fedha taslimu.

Baada ya fedha hizo kuchukuliwa ambazo kwa maelezo ya awali, ilielezwa kwamba wanakwenda kufanyia kazi ya ukusanyaji wa takwimu za wanafunzi wenye ulemavu mashuleni, jambo ambalo kazi hiyo haikufanyika na taarifa za watu hao wenye mahitaji maalumu imethibitishwa kuwa zilikwisha kusanywa siku za nyuma zilizopita na kufanyiwa kazi mapema na kwamba ujanja huo wa kuchukua fedha hizo za walemavu, inadaiwa kwamba ulikuwa ni wa kujinufaisha wao wenyewe.

Gazeti hili lilipokwenda shuleni hapo na kukutana na Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Mapunda ambapo alithibitisha kutolewa kwa fedha hizo kutoka kwenye akaunti ya shule yake kwa mtindo wa kuandikiwa hundi Afisa huyo wa elimu maalumu, Kumburu na kufanikiwa kuzichukua.

Taarifa hizo zilipoufikia pia uongozi wa Chama Cha Walemavu (CHAWATA) wilaya ya Mbinga, umesikitishwa nazo na kueleza kuwa kuna kila sababu kwa wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo warejeshe fedha hizo ambazo wamezitumia kinyume na maelekezo waliyopewa.

Pia uongozi huo ulieleza masikitiko yake na kumtaka Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama kuingilia kati suala hilo na kuchukua hatua za haraka dhidi ya wahusika wanaonyoshewa kidole kutumia fedha hizo vibaya bila kufuata miongozo waliyopewa.

“Malipo ya posho kwa kazi yoyote wanayoifanya ndani ya Halmashauri walitakiwa walipwe kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji na sio kama walivyotumia mbinu za ujanja kutafuna fedha hizi ambazo zilikwisha pelekwa shuleni hapo zikafanye kazi iliyolengwa, kwa ajili ya kuweza kusaidia kundi hili tete”, alisema Martin Mbawala Mwenyekiti CHAWATA wilaya ya Mbinga.

Kadhalika mwandishi wetu amefanikiwa kupata nakala ya mchanganuo wa malipo ya posho walizolipana kutoka sehemu ya fedha hizo za walemavu, ambapo Kaimu Afisa elimu msingi Alphonce Mwamwile amelipwa shilingi 675,000 kwa idadi ya siku 15 ambapo kwa kila siku alikuwa akilipwa shilingi 45,000 ikieleza kuwa alikwenda kufanya kazi katika tarafa ya Namswea, Hagati na Kigonsera.

Ambrose Ngonyani ambaye naye ni mmoja kati ya maofisa wa idara ya elimu wilayani hapa, amelipwa shilingi 630,000 kwa siku 18 na kwamba kila siku alikuwa akilipwa shilingi 35,000 kwa siku, ikieleza pia amekwenda kufanya kazi tarafa ya Namswea, Hagati, Kigonsera, Mbuji, Mkumbi na Mbinga mjini.

Vilevile Sixbertha Kumburu, Afisa elimu maalumu naye alilipwa shilingi 630,000 kwa siku 18 hivyo kiasi cha shilingi 35,000 kwa kila siku alikuwa akilipwa na kwenda kufanya kazi tarafa ya Namswea, Hagati, Kigonsera, Mbuji, Mkumbi na Mbinga mjini.

Vilevile Albert Ngimba afisa elimu vifaa na takwimu wilayani Mbinga, amelipwa shilingi 415,000 kwa siku 12 ambapo kiasi cha shilingi 35,000 alikuwa akilipwa kila siku na kuonesha amekwenda kufanya kazi katika kata mbili tu, ya Namswea na Mkumbi huku dereva Bosco Gayo katika malipo hayo akiwa amelipwa shilingi 150,000 kwa siku 6 ambapo kwa kila siku alikuwa akilipwa shilingi 25,000 huku mchanganuo huo wa malipo ukifafanua kwamba alikwenda kufanya kazi katika tarafa ya Namswea, Hagati, Mkumbi na Mbuji. 

Alipohojiwa Kaimu Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mwamwile ili aweze kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo, alikiri kuchukuliwa kwa fedha hizo na kulipana posho na kuongeza kuwa walifanya hivyo, kwa lengo la kwenda kutekeleza majukumu waliyopewa na serikali.

“Siwezi tena kutoa ufafanuzi zaidi ya haya niliyosema, sisi tulichukua fedha hizi kwa ajili ya kwenda kukusanya takwimu za watu hawa wenye ulemavu, sina nyongeza yoyote katika hili”, alisema Mwamwile.

Hata hivyo aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya suala hilo alionesha kushangaa juu ya kitendo hicho na kueleza kuwa, yeye hana taarifa kamili juu ya matumizi ya fedha za watu wenye ulemavu wa wilaya hiyo huku akisisitiza kwamba zilipopelekwa shule ya msingi Kiwanjani, ilibidi zikafanye kazi iliyolengwa na sio vinginevyo.

No comments: