Wednesday, June 8, 2016

AKUTWA AMEFARIKI DUNIA HUKU UUME WAKE UKIWA UMEVESHWA KONDOMU



Na Kassian Nyandindi,
Songea.

MTU mmoja ambaye ni mkazi wa Bombambili Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Peter Christopher (35) amekutwa akiwa amefariki dunia huku sehemu zake za siri zikiwa zimevalishwa mpira wa kiume maarufu kwa jina la Kondomu ambayo ilikutwa ikiwa imekwisha tumika.

Habari zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Zubery Mwombeji zinasema kuwa mwili wa marehemu huyo ulikutwa hivi karibuni majira ya mchana kwenye pori lililopo eneo la Making’inda, kata ya Msamala mjini hapa.

Kamanda huyo alisema kuwa Christopher alikutwa amefariki dunia, mwili wake ukiwa hauna jeraha la aina yeyote badala yake alikutwa akiwa amevaa mpira huo kwenye uume wake, huku mpira mwingine ukiwa bado haujatumika ambao ulikutwa kwenye mfuko wake wa suruali ambayo ilikuwa kando kando ya mwili wake.


Alisema kuwa mpaka sasa bado haijafahamika chanzo cha tukio hilo, licha ya kwamba taarifa za awali kutoka kwa ndugu wa marehemu huyo zinaeleza kuwa tangu Mei 17 mwaka huu alitoweka nyumbani kwake, ambapo baadaye walichukua jukumu la kutoa taarifa kituo kikuu cha Polisi Songea mjini huku juhudi za kumtafuta zilipokuwa zikiendelea walifanikiwa mwili wake kuupata katika eneo hilo la Making’inda.

Mwombeji alifafanua kuwa mwili huo ulipopatikana, ndugu waliweza kuutambua ambapo baada ya uchunguzi wa madaktari kufanyika kwa kushirikiana na Polisi, walibaini kwamba haukuwa na majeraha yoyote na baadaye waliukabidhi kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.

Hata hivyo Kamanda huyo wa Polisi mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi kufuatia kutokea kwa tukio hilo huku akitoa mwito kwa wananchi, kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa jeshi hilo ili kuweza kubaini chanzo cha kifo chake.

No comments: