Thursday, June 2, 2016

ALIYEMUUA SHEKHE MSIKITI WA LIKWESO TUNDURU APANDISHWA KIZIMBANI



Na Steven Augustino,

Tunduru.

ALLY Mchumwa (45) ambaye ni mtuhumiwa wa tukio la mauaji ya Shekhe wa Msikiti wa kijiji cha  Likweso, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma amefikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili juu ya tukio hilo.

Habari zinaeleza kuwa, kabla ya mtuhumiwa huyo kutekeleza unyama huo alimuua kwa kumchoma kisu shingoni Shekhe, Seleman Mwarabu Selemani (45) katika tukio la fumanizi lililotokea Mei 22 mwaka huu.

Akimsomea shauri hilo la mauaji namba 4/2016 mbele ya Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelaeli Jwagu alisema kuwa, tukio hilo lilitokea siku  hiyo majira ya saa 3.30 asubuhi katika eneo la mashamba ya Mkasandimbe yaliyopo tarafa ya Nakapanya, wilayani Tunduru.


Inspekta Jwagu alidai Mahakamani hapo kuwa, kitendo alichokifanya mtuhumiwa Ally ni kosa kinyume cha sheria namba 196 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Pamoja na mambo mengine, kutokana na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji mtuhumiwa huyo, hakutakiwa kujibu chochote Mahakamani hapo na kwamba shauri hilo litatajwa tena Juni 4 mwaka huu.

No comments: