Tuesday, June 7, 2016

LITUHI NYASA WALALAMIKIA UGAWAJI CHAKULA CHA MSAADA KILICHOTOLEWA NA SERIKALI


Na Kassian Nyandindi,

Nyasa.

BAADHI ya Wananchi wa kijiji cha Kihuru na Nkaya katika kata ya Lituhi wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameilalamikia Ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo kwa kushindwa kusimamia ipasavyo ugawaji wa chakula cha msaada ambacho kimetolewa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo, ambao walikumbwa na maafa ya kuzolewa nyumba na mazao yao shambani.
Rais Dkt. John Magufuli.

Maafa hayo ambayo yalitokea Aprili 4 hadi 8 mwaka huu, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha siku nne mfululizo ambayo iliambatana na upepo mkali ambapo zaidi ya wananchi 1,000 walikosa mahali pa kuishi, kufuatia nyumba na mazao yao waliyolima shambani kuzolewa na mkondo mkubwa wa mafuriko ya maji ambao ulikuwa ukielekea ziwa Nyasa wilayani humo.

Wakizungumza kwa kuomba majina yao yasitajwe kwenye mtandao huu, walisema kuwa wameshangazwa na Ofisi hiyo ya Mkuu wa wilaya  kutosimamia  kwa karibu zoezi hilo la ugawaji wa mahindi hayo ambayo yametolewa na serikali tarehe 18 mwezi Mei mwaka huu, ili yaweze kuwasaidia wahanga hao ambao wamekumbwa na mkasa huo.


Aidha walieleza kwamba taarifa juu ya malalamiko hayo, Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Margaret Malenga yamemfikia lakini hawaoni jitihada zinazoendelea kufanyika katika kunusuru hali hiyo, hivyo wanauomba uongozi wa ngazi ya juu serikalini uingilie kati na kuweza kupata haki yao ya msingi.

Vilevile kufuatia hali hiyo walisema wamekosa imani na Afisa mtendaji wa kata hiyo, Charles Chikuni na Diwani wake Dominick Mahundi ambapo licha ya viongozi hao wa kata hiyo ya Lituhi kupewa dhamana ya kusimamia zoezi la ugawaji wa mahindi hayo kwa kufuata taratibu husika, wameshindwa kutekeleza ipasavyo badala yake wamekuwa wakiyagawa kwa upendeleo hata kwa watu wengine ambao hawahusiki katika zoezi hilo.

“Sisi inatusikitisha sana mahindi haya tokea yameletwa hapa Lituhi yana wiki tatu sasa zimepita, viongozi wetu hawa wa kata wamekuwa wabinafsi wanayagawa kwa kujuana na sio kwa kufuata utaratibu uliowekwa kulingana na mahitaji ya walengwa walioathirika na maafa haya”, walisema.

Jumla ya tani 43.2 za mahindi ndizo ambazo serikali ilipeleka kwa wahanga hao wa mafuriko katika kata ya Lituhi,  ambapo ofisi inayosimamia masuala ya maafa hayo yaliyotokea katika vijiji hivyo ni ya Mkuu wa wilaya hiyo.

Pamoja na mambo mengine, mwandishi wa habari hizi alipofanya mahojiano na Afisa mtendaji wa kata hiyo, Chikuni alisema yeye malalamiko hayo hayajamfikia ofisini kwake na hawezi kuzungumzia lolote.

“Naomba nikueleze sina malalamiko yoyote kwenye ofisi yangu yaliyoletwa na wananchi hawa kuhusiana na mahindi haya ya msaada uliotolewa na serikali, kwanza nakushangaa kwa nini uje unihoji mimi badala ya kwenda kuwahoji waliokuletea taarifa hizi”, alisema Chikuni.

Pia Diwani wa kata ya Lituhi, Mahundi naye alipotakiwa kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko haya alisema, “mimi wahanga wa maafa haya siwatambui, kama walikuja kwako siwezi kukueleza lolote juu ya taarifa zao kwa sababu siwatambui”.

Hata hivyo alipotafutwa Mkuu wa wilaya ya Nyasa, Malenga aweze kutolea ufafanuzi juu ya shutuma hizo hakuweza kupatikana ofisini kwake na simu yake ilipopigwa ilipokelewa na alipoulizwa juu ya malalamiko hayo ya wananchi wake, hakujibu lolote na badala yake aliishia kuikata na kwamba licha ya jitihada ya kupiga tena mara kwa mara haikupokelewa.

No comments: