Saturday, June 25, 2016

DC TUNDURU APOKEA MSAADA WA SHILINGI MILIONI 2.5 KWA AJILI YA KUBORESHA MAZINGIRA YA KUSOMEA WANAFUNZI

Upande wa kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,  Agnes Hokororo akipotea hundi yenye thamani ya shilingi milioni 2.5 kutoka kwa Meneja wa sheria na usuluhishi wa kampuni ya Export Trading Group (ETG) Nasser Mansour, katika hafla fupi iliyofanyika juzi katika ofisi za kiwanda cha kubangulia korosho mjini hapa.


Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo amewataka wafanya biashara na wadau wengine wa maendeleo wilayani humo kujitokeza na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika kusaidia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za wilaya hiyo, ambazo zimekuwa chakavu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kusomea wanafunzi.

Hokororo alitoa wito huo juzi, alipokuwa akipokea msaada wa shilingi milioni 2.5 kutoka kwa Meneja wa sheria na usuluhishi wa kampuni ya Export Trading Group (ETG) Nasser Mansour, katika hafla fupi iliyofanyika katika  kiwanda cha kubangua Korosho kinachofahamika kwa jina la Korosho Afrika Limited kilichopo mjini hapa.

Alisema kuwa fedha hizo zimetolewa kwa wakati muafaka huku akiahidi kuzisimamia kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, zinatumika kwa ajili ya kufanyia kazi iliyolengwa.


Kadhalika akitoa maelezo mafupi juu ya msaada huo, Meneja Mansour alimweleza Mkuu wa wilaya hiyo, Hokororo kuwa msaada huo ni sehemu ya faida ambayo kampuni imejipangia kurejesha kwa njia ya kutoa huduma kwa jamii na kwamba, zitafanya kazi ya kufanya ukarabati wa madarasa na kutengeneza madawati katika shule ya msingi majengo iliyopo mjini Tunduru.

Vilevile akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho, Meneja wa kampuni hiyo ya (ETG) Vinesh Mathew alifafanua kuwa kiwanda hicho kilianza shughuli za ubanguaji korosho wilayani humo, mapema mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka 2008 ambapo kimekuwa ni tegemeo la kutoa ajira kwa wakazi wa wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka ndani ya uongozi wa kiwanda hicho, zinaeleza kuwa jumla ya watu 700 wanawake na wanaume wamekuwa wakinufaika kwa kupewa ajira katika eneo la kiwanda, wakati wa msimu wa mavuno ya korosho na shughuli za ubanguaji zinapofanyika.

Pia watu hao huishi kwa kutegemea ajira  za muda, lakini hunufaika kutokana na kipato wanachokipata wao na familia zao zinazowazunguka katika kujiletea maendeleo.

Shughuli zinazofanywa katika kiwanda hicho ni pamoja na ununuzi wa korosho, ukaushaji, ubanguaji, upangaji kwa madaraja husika, upakiaji na uuzaji wa zao hilo katika masoko yaliyopo nje ya nchi.

No comments: