Thursday, June 23, 2016

MKUU WA WILAYA NAMTUMBO ACHARUKA JUU YA UHARIBIFU WA MAZINGIRA AITAKA MAMLAKA HUSIKA KUCHUKUA HATUA

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Chande Nalicho watatu kutoka kulia akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wenzake wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo, mara baada ya kufanya ufunguzi wa mdahalo wa athari na mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo. Wa pili kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa shirika la MWECO ambaye anaendesha mafunzo hayo, Terdey Mhagama. 

Mkuu wa wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Chande Nalicho akisisitiza jambo kwa kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kuacha kuharibu vyanzo vya maji, ikiwemo suala la ukataji miti na uchomaji misitu hovyo.

Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo, Shida Kapata akichangia mada katika mafunzo hayo na kusisitiza wanawake wenzake wilayani Namtumbo kwenda kuelimisha jamii, juu ya suala zima la utunzaji wa mazingira na kuacha tabia ya uharibifu wa vyanzo vya maji. (Picha zote na Muhidin Amri, Namtumbo)
Na Kassian Nyandindi,

Namtumbo.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho ametoa agizo kwa kuitaka mamlaka husika wilayani humo kuwachukulia hatua za kisheria watu waliovamia vyanzo vya maji, kutokana na wilaya hiyo hivi sasa kukabiliwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama.

Aidha ameagiza pia waharibifu hao wa mazingira, wanapaswa kufikishwa Mahakamani ili iweze kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia ya kuharibu mazingira, ikiwemo ukataji wa miti hovyo.

Tumaini Mgaya Ofisa maendeleo ya jamii Namtumbo, akisisitiza jambo kwenye mafunzo hayo.
Nalicho alisema kuwa tangu enzi za mababu zetu walikuwa wakikemea tabia hii ya uharibifu wa mazingira, hivyo kuna kila sababu kwa jamii kurithi tabia hiyo ili kuweza kuepukana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi, ambalo linahatarisha usalama wa maendeleo ya viumbe hai hapa duniani.

Agizo hilo la Mkuu huyo wa wilaya ya Namtumbo, Nalicho lilitolewa juzi alipokuwa akifungua mdahalo wa athari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake wa wilaya hiyo, uliofanyika ukumbi wa Bikira Maria wa Fatima, mjini hapa.


“Nimetoa maelekezo kwa watalaamu wangu wa wilaya, kamateni waharibifu wote wa mazingira pelekeni mahakamani wakalipe faini au wafungwe jela na wale wanaolima katika vyanzo vya maji watoke haraka, kabla dola haijachukua jukumu la kuwatoa kwa kutumia nguvu”, alisisitiza Nalicho.

Vilevile alisema kuwa athari za mabadiliko ya tabia nchi zinapotokea, wanaohangaika na kuteseka ni wanawake na watoto wadogo hivyo ameitaka jamii wilayani humo, kujenga ushirikiano ili waweze kukabiliana na hali hiyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kadhalika alifafanua kuwa endapo wananchi wasipozingatia maelekezo yanayotolewa na serikali, kuna hatari ya kuiweka nchi yetu katika mazingira mabaya na kubaki kuwa maskini huku akiongeza kuwa hata tabia ya uchomaji moto misitu hovyo katika wilaya ya Namtumbo, wananchi wanapaswa kuiacha mara moja.

Awali kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali hapa nchini la Mbarali Water Sanitation and Environmental Conservation Organisation (MWECO), Terdey Mhagama alifafanua kuwa mdahalo huo umeshirikisha baadhi ya wanawake 70  wa kutoka wilaya ya Namtumbo kwa lengo la kujenga uwezo katika masuala ya kiuchumi kwa jamii na kufanya utetezi katika upatikanaji wa rasilimali za maji, uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira.

Mhagama alieleza kuwa tafiti zinaonesha kwamba ndani ya miaka 20 ijayo ukanda wa Afrika ya kati, mashariki na kusini, Tanzania ikiwa mojawapo zitakuwa jangwa kabisa kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Alisema hali hii inabainisha kwamba ukame utakuwa umetokea kila mahali, mafuriko wakati wa mvua yataathiri makazi ya watu na hakutakuwepo miti ya kunyonya maji ya mvua chini ya ardhi, ili jamii isiweze kuathirika.

Hivyo wananchi wa wilaya ya Namtumbo, wamesisitizwa kutunza mazingira kwa kila hali ili waweze kuishi maisha mazuri na kwamba endapo kama watakuwa wamefanikiwa katika hili, watakuwa wamejenga historia kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

No comments: