Thursday, June 30, 2016

WANANCHI MBALATSE MAKETE WALALAMIKIA ARDHI YAO KUPORWA NA MWEKEZAJI



Na Kassian Nyandindi,

Njombe.

WANANCHI wa kata ya Mbalatse wilaya ya Makete mkoa wa Njombe, wamemuomba Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi William Lukuvi kuona umuhimu wa kuingilia kati mgogoro uliopo kati yao na mwekezaji wa Kampuni ya Silverlands Tanzania yenye makao yake makuu mkoani Iringa, ambaye anadaiwa kwamba amepora ardhi yao zaidi ya hekta 3,000 ambazo zilikuwa zikiwasaidia kuzalisha mazao ya aina mbalimbali.

Aidha kufuatia ardhi hiyo kuchukuliwa na mwekezaji huyo, wananchi hao wanakosa maeneo ya kulima mazao ya chakula na biashara jambo ambalo hivi sasa baadhi yao wanalazimika kwenda kwenye maeneo karibu na vyanzo vya maji kulima mazao hayo.

William Lukuvi.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, wananchi hao walifafanua kuwa miaka iliyopita kwa muda mrefu walikuwa wakilima mahindi kwa wingi katika eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la Ludodolela, ambalo lina rutuba tofauti na maeneo mengine yaliyopo kwenye kata hiyo.

Aloyce Chaula mkazi wa kijiji cha Mbalatse alifafanua kuwa tangu kuzaliwa kwake miaka ya 60 iliyopita wazazi wake pamoja na wananchi wengine wa kata hiyo walikuwa na mashamba yao katika eneo hilo ambalo amepewa mwekezaji, bila wananchi kushirikishwa hivyo wanaiomba serikali kupitia Wizara hiyo kunusuru hali hiyo ili wananchi wa kata hiyo waweze kurejeshewa mashamba yao.

“Ndugu waandishi wa habari mnaliona kundi hili kubwa la wananchi wakilalamikia kuporwa maeneo yao, kwani awali huyu mwekezaji alikuja hapa kwetu kijijini kuomba eneo dogo kwa muda kwa ajili ya kufanya majaribio ya kupanda mbegu za zao la shairi, lakini tuna mshangaa ghafla amemilikishwa eneo kubwa na sisi wazawa tumefukuzwa huku akiendelea na uzalishaji wa zao hili la shairi”, alisema Chaula.


Kwa upande wake Damian Mwinuka mkazi wa kijiji hicho alieleza kuwa kufuatia mwekezaji huyo kunyang’anya eneo hilo la mashamba bila kufuata taratibu za utwaaji ardhi, hivi sasa vijana wengi wanakwenda mikoa ya jirani kwenda kutafuta mashamba ya kulima wakati nyumbani kwao kulikuwa na eneo kubwa la kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ikiwemo viazi mviringo, ufuta, alizeti na ngano.

Alisema kuwa kutokana na usumbufu huo wanaoupata sasa, bado wanalazimika kuiangukia serikali ili iweze kuwasaidia na ardhi yao irejeshwe mikononi mwao na sio vinginevyo.

Uchunguzi uliofanywa na timu ya waandishi wa habari umebaini pia katika mashamba hayo yanayolalamikiwa, mwekezaji huyo wa Silverlands Tanzania yenye makao makuu yake mkoani Iringa ndiyo anayeendesha shughuli za kilimo cha zao la shairi kwenye eneo hilo linalolalamikiwa na wananchi hao.

Waandishi hao wameshuhudia ndani ya eneo hilo kuna kiwanja cha ndege ambapo inadaiwa kimekuwa kikitumika ndege kutua, kipindi cha kiangazi wakati wa mavuno ya zao hilo na kwamba pia kumejengwa majengo ya ofisi na nyumba za kuishi wafanyakazi wa shamba hilo.

Kadhalika sehemu ya shamba hilo kumezalishwa kwa wingi zao la alizeti, ngano na mboga mboga pamoja na miti ya asili.

Naye diwani wa kata ya Mbalatse, Edson Msigwa alisema kuwa malalamiko hayo ya wananchi ni ya kweli kwa kile alichodai kuwa mwekezaji huyo alipewa ekari 70 tu kwa muda kwa lengo afanye majaribio ya kupanda mbegu za zao la shairi, lakini anashangaa kuona amezalisha ekari zaidi ya 3,000 na kujimilikisha maeneo hayo bila wananchi kujua.

Msigwa alisema kuwa kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko huo, tayari hatua zimechukuliwa kwa kwenda halmashauri ya wilaya ya Makete kuutaka uongozi husika kuona namna ya kumaliza tatizo hilo, kabla machafuko hayajatokea kama ilivyo kwa maeneo mengine ya nje ya mkoa wa Njombe.

“Wananchi wa kata yangu wapo tayari kufunga safari kwenda kuonana na Waziri mwenye dhamana, ili waweze kupata haki zao za msingi juu ya madai haya ya ardhi yao kutokana na hivi sasa wanakosa maeneo ya kuzalisha chakula”, alisema Msigwa.

Pamoja na mambo mengine Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Egnatio Mtawa alipohojiwa na waandishi wa habari alikiri kuwepo kwa mgogoro huo na kuongeza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa tume imeundwa kuchunguza kwa undani juu ya jambo hilo, ambapo baadaye tume itatoa taarifa baada ya kumaliza kazi yake.

Meneja wa shamba la kampuni hiyo, Steven Maina alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya malalamiko hayo ya wananchi, alikanusha na kusema kuwa hakuna mwananchi yeyote aliyewahi kwenda ofisini kwake na kutoa malalamiko kama hayo huku akiongeza kuwa kama kuna mtu anataka kufahamu juu ya umiliki wa shamba hilo, awasiliane na uongozi wa kampuni hiyo na sio vinginevyo.

No comments: