Sunday, June 5, 2016

HALMASHAURI KUKAMILISHA UJENZI SKIMU YA UMWAGILIAJI SANGAMABUNI

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

HALMASHAURI ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imesema kwamba, itaendelea kufanya kazi ya kukamilisha ujenzi wa mfereji mkuu unaoleta maji shambani katika skimu ya umwagiliaji Sangamabuni, iliyopo kijiji cha Mabuni kata ya Litumbandyosi wilayani humo ili wakulima waweze kunufaika na kilimo cha zao la mpunga kupitia umwagiliaji wanaoufanya katika mradi huo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Venance Mwamengo alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea kuona kazi ya kilimo cha zao la mpunga, kinachofanywa na kikundi cha Sangamabuni kijijini humo.

“Hivi sasa tuna tatizo kubwa la ukosefu wa fedha katika halmashauri yetu ili tuweze kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo ya wananchi, lakini tunawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu mara tupatapo pesa tutaikamilisha ujenzi wake haraka iwezekanavyo”, alisema Mwamengo.


Mradi wa  Sangamabuni ulianza kutekelezwa  na wanakikundi wenyewe mwaka 2011, ambapo hivi sasa wapo 122 wakiwemo wanawake 61 na wanaume 61 hivyo wanashindwa kufikia malengo ya uzalishaji kutokana na mfereji mkuu unaotumika kupeleka maji shambani kutokamilika ujenzi wake.

Kwa mujibu wa Mwamengo alifafanua kuwa jitihada zilizooneshwa na wakulima wa kikundi hicho, kuna kila sababu kwa serikali kuendelea kuunga mkono ili waweze kuondokana na umaskini na kutumia fursa iliyopo kujiletea maendeleo.

Hata hivyo aliwataka nao wataalamu wa ugani wilayani Mbinga, kuendelea kuwa bega kwa bega na wakulima wanaozalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kwa kuwaelimisha mbinu bora za kilimo cha kisasa, ili waweze kuzalisha mazao mengi yenye ubora na hatimaye kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
 



No comments: