Wednesday, June 8, 2016

WALIMU SHULE SEKONDARI KITURA WALIA NA JENGO LA UTAWALA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JENGO la utawala ambalo hutumika na Walimu wa shule ya sekondari Kitura katika kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, lina hali mbaya ambapo wakati wowote huenda likabomoka na kuleta madhara kwa watumiaji.

Miundo mbinu ya jengo hilo ambayo ni chakavu na imetengeneza nyufa, hivi sasa baadhi ya kuta zake zimeanza kubomoka na kuhatarisha usalama wa walimu wanaofundisha katika shule hiyo.

Wakizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea shuleni hapo huku wakiomba majina yao yasitajwe gazetini, walimu hao walisema kuwa hata mazingira ya shule yao yamekuwa magumu ambapo vyoo vya wanafunzi na nyumba za walimu zilizopo hazikidhi mahitaji husika.


Kadhalika walieleza kuwa kuna kila sababu kwa uongozi husika kuchukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo, ili isiweze kuleta madhara makubwa hapo baadaye na kuwafanya walimu wakate tamaa ya kuendelea kufundisha katika shule hiyo.

Diwani wa kata ya Kitura Alex Ngui alipoulizwa juu ya tatizo hilo, alikiri kuwepo kwa matatizo hayo na kufafanua kuwa hivi sasa wameweka mikakati ya kuhamasisha wananchi wake kufyatua tofari ambazo zitasaidia kuanza kazi ya ujenzi wa jengo hilo la utawala katika shule ya sekondari Kitura, pamoja na vyoo na nyumba za walimu.

Alisema wananchi walikuwa wanashindwa kuanza kuchangia nguvu zao ikiwemo ufyatuaji wa tofari za udongo, kutokana na mvua za masika ambazo zilikuwa zikinyesha mara kwa mara hivyo walikuwa wakisubiri ziishe ndipo waanze kufanya kazi hiyo.

Ngui alifafanua kuwa kupitia vikao vyake vya kata ambavyo amekuwa akivifanya, wamejiwekea malengo pia ya kuushirikisha uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo uweze kusaidia vifaa vya kiwandani mara baada ya wananchi kuchangia nguvu zao, kama vile mchanga, mbao na ufyatuaji wa tofari za udongo.

Hata hivyo alisema kuwa, pia wameweza kuibua mradi wa madaraja mawili kutoka kijiji cha Mahilo kwenda makao makuu ya kata hiyo ambapo utekelezaji wake utaanza katika bajeti ya maendeleo ya wilaya ya Mbinga, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 madaraja hayo ujenzi wake utakuwa umekamilika.

No comments: