Tuesday, December 30, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA AMDANGANYA RAIS KIKWETE, ADAIWA KUPANGIA MATUMIZI FEDHA ZA WAKULIMA WA KAHAWA KINYUME NA TARATIBU ZA USHIRIKA

Rais Jakaya Kikwete.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MALALAMIKO yaliyotolewa juu ya shilingi bilioni 2 ambazo baadhi ya vyama vya ushirika (AMCOS) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, vilikopeshwa na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) na kuleta gumzo kuwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hussein Ngaga, hakuzipeleka kwenye vyama hivyo badala yake alidaiwa kuziingiza kwenye akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo tumebaini kwamba, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti husika za vyama hivyo huku akitoa masharti kwa uongozi wa AMCOS hizo kuwa, hawana ruhusa ya kuzifanyia matumizi ya kukopeshana mpaka idhini itoke kwake.

Aidha mkurugenzi huyo analalamikiwa kuwa viongozi hao wa vyama vya ushirika, alikuwa akiwapangia matumizi ya fedha hizo baada ya yeye kujiridhisha kwanza wameandaa mpango kazi wa mahesabu husika na kiasi cha kahawa walichonacho ambayo itaingizwa kiwandani, ndipo alikuwa akiwaruhusu kwenda kutoa fedha benki huku akihakikisha hundi walizoandika zina kiwango halisi anachokifahamu.

Na wakati mwingine analalamikiwa kuwa, alikuwa hawapatii fedha kwa kiwango walichoomba katika mahesabu hayo ambayo walikuwa wakimpelekea ofisini kwake kwa ajili ya kuyakagua na kujiridhisha, badala yake alikuwa anapunguza kwa kiwango anachokitaka yeye.

Tumebaini pia baada ya mauzo ya kahawa kufanyika mnadani Moshi, hivi sasa mkurugenzi Ngaga amekuwa akikwepa kutoa Fomu ya mauzo ya kahawa kwa dola (Account Sale) kwa wanaushirika hao, licha ya wao kumfuata mara kwa mara wakimtaka awapatie.

Katika fomu hiyo huonyesha kahawa ambazo zimeuzwa kwa dola na ubadilishaji wa fedha za mauzo ya kahawa kutoka kiwango cha dola kuwa shilingi, hivyo inadaiwa huenda zimeuzwa kwa bei ya juu huku wanaAMCOS hao wakimlalamikia kuwalipa bei ndogo, ndio maana hataki kutoa fomu hizo na kuweka mchakato huo wa mauzo kuwa bayana ili wakulima waweze kufahamu juu ya mauzo ya kahawa yao ulivyofanyika.

Hali hiyo imeelezwa na wakulima hao kuwa huenda anaficha ukweli halisi usiweze kujulikana juu ya mwenendo mzima wa mauzo ya kahawa yao ulivyofanyika huko mnadani kwa kila mkulima (vikundi).

Sunday, December 28, 2014

TAMISEMI MKURUGENZI WENU WA MBINGA ANA MATATIZO CHUKUENI HATUA SASA KABLA KIDONDA HAKIJAWA SUGU

Hawa Ghasia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MAPYA yanaendelea kuibuka katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, ambapo baadhi ya Wafanyakazi wenye mikataba ya ajira ya muda wamemlalamikia Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, kwamba amekuwa ni mtu wa kuwatolea lugha zenye kukatisha tamaa ya kufanya kazi na kutowalipa mishahara yao kwa wakati. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti huku wakiomba majina yao yasitajwe kwa kuhofia usalama wa kazi zao wakidai kufukuzwa kazi, walisema Mkurugenzi huyo amekuwa akiwatolea lugha zenye ukali hasa pale wanapokuwa wakidai madai yao ya msingi, kama vile fedha za malipo ya kazi walizofanya.

Wengine walifafanua kuwa hata mishahara yao ambayo inabidi walipwe tarehe husika za mwisho wa mwezi, kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa na serikali, Ngaga amekuwa hafanyi hivyo badala yake amekuwa akiwalipa kwa kuchelewesha.

KWA MABOMU HAYA YA SONGEA, TUNAPASWA KUJIULIZA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VIPO WAPI?

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.
Na Kassian Nyandindi,

MATUKIO ya mabomu mjini Songea hapa mkoani Ruvuma, umekuwa sasa ni mchezo mchafu ambao unahatarisha usalama wa raia, hivyo kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua madhubuti juu ya kudhibiti hali hii.

Tunasema kuna kila sababu sasa ya kufanya hivyo, kutokana na kile tunachoweza kusema kwamba tumechoka kusikia kauli za viongozi wa ngazi ya juu hususani hapa mkoani, wakisema kwamba watahakikisha hali hii itadhibitiwa kwa kuwakamata wahusika ili matukio kama haya yasiweze kuendelea kutokea.

Ni muhimu sasa kuona namna gani tunashirikisha jamii kwa karibu zaidi, ili waweze kutoa ushirikiano wa kutosha ambao baadaye utaweza kuleta tija katika kukomesha genge la watu hawa, ambao wanahusika kutengeneza mabomu haya.

Hili ni tukio la tatu sasa kutokea hapa songea, mara ya kwanza askari polisi walirushiwa bomu, mara ya pili lilitegwa karibu na kituo cha kurusha matangazo (TBC) mjini Songea na leo askari hawa hawa wanarushiwa tena, tunapenda kuhoji vyombo vya ulinzi na usalama vipo wapi au vimeenda likizo? 

Tunahoji hivyo sio kwa nia mbaya, kwa sababu mara kwa mara tumekuwa tukiwanukuu baadhi ya vigogo wakisisitiza na kuahidi kukomesha hali hii isiweze kuendelea kutokea, lakini inashangaza kuona matukio haya yanajirudia na kuwafanya watu waishi kwa wasiwasi.

Saturday, December 27, 2014

JESHI LA POLISI NCHINI LAUNDA TIMU KUCHUNGUZA TUKIO LA BOMU SONGEA

Askari aliyejeruhiwa na bomu mjini Songea mkoa wa Ruvuma, WP Mariamu Lukindo akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa huo iliyopo mjini hapa.
Na Mwandishi wetu,
Songea.

TIMU ya makachero kutoka makao makuu ya Jeshi la polisi nchini, wakishirikiana na wa mkoa wa Ruvuma, kwa ajili ya kufanya uchunguzi kuhusiana na matukio ya mabomu yanayoendelea kujitokeza mara kwa mara mkoani humo.

Makachero hao wanatoka Jijini Dar es salaam, kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la mtu mmoja aliyelipukiwa na bomu maeneo ya majengo mjini songea  na kujeruhi askari polisi wawili, wakati akijiandaa kuwarushia  askari waliokuwa doria na kisha bomu hilo kumuua mwenyewe.

Hayo yalisemwa na kaimu mkurugenzi wa makosa ya jinai nchini, Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi Diwani Athumani aliyewasili mjini  Songea kwa helkopta kwa ajili ya tukio hilo ambalo mtu ambaye hajatambulika,   amelipukiwa na bomu hilo na kufariki dunia  papo hapo wakati akijaribu kuwarushia askari waliokuwa doria na kujeruhi askari wawili.

Aliwataja askari waliojeruhiwa kuwa ni PC Mselemu na WP Mariamu Lukindo  ambaye bado amelazwa katika hospitali ya mkoa iliyopo mjini Songea.

WAENDESHA PIKIPIKI TUNDURU WACHOMA MOTO VIBANDA NA KULETA FUJO KITUO KIKUU CHA POLISI


Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, ACP Mihayo Msikhela.
Na Waandishi wetu,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida waendesha pikipiki maarufu kwa jina la yeboyebo, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma walifanya maandamano makubwa kwa lengo la kupinga vitendo vya unyanyasaji ambavyo wanafanyiwa na askari polisi wa wilaya hiyo, ikiwemo kuwakamata hovyo bila kufuata taratibu.

Madereva hao waliandamana na kufanya fujo katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Tunduru, pia waandamanaji hao walichoma moto vibanda vinne ambavyo hutumiwa na kampuni ya State business center na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.

Kwa nyakati tofauti madereva hao walisema wamechukua maamuzi hayo magumu, baada ya kuchoshwa na vitendo viovu ikiwemo kuombwa rushwa mara kwa mara, ambavyo hufanyiwa na askari hao hasa wa kitengo cha usalama barabarani.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUUMWA NA NYOKA MWENYE SUMU KALI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

BINTI wa miaka mitano Mwanahamis Omary, mkazi wa kijiji cha Kalulu wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu kali.

Akizungumzia tukio hilo baba wa mtoto huyo Omary Bakari alisema mkasa huo ulimpata mtoto huyo, wakati akiwa anavuka mto Kalulu kuelekea shambani na kwamba wakati anakumbwa na tatizo hilo alikuwa amefuatana na mama yake mzazi Zainabu Ally.

Baada ya tukio hilo mama yake huyo alipiga kelele za kuomba msaada wa kumpeleka mtoto wao katika zahanati ya kijiji hicho  kwa matibabu zaidi, lakini ilishindikana kwani mtoto huyo alifariki dunia wakiwa njiani kuelekea katika zahanati hiyo.

Hata hivyo nyoka huyo hakuweza kutambuliwa ni wa aina gani, wakati anamuuma mtoto huyo.

UVCCM RUVUMA YAITAKA JAMII KUFARIJI WAGONJWA



Steven Augustino na Abbas Mlanya,
Tunduru.

UMOJA wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoani Ruvuma, umewataka wadau mbalimbali kujenga tabia ya kuwatembelea wagonjwa ambao wamelazwa hospitalini, kwa lengo la kuwafariji na kuwapatia zawadi hasa katika kipindi cha sikukuu za kitaifa.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa umoja huo mkoani hapa, Alex Nchimbi wakati alipowatembelea wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya wilaya ya Tunduru.

Aidha Nchimbi ambaye aliongozana na viongozi wenzake wa chama cha mapinduzi wilayani humo, wakiwemo wakiwemo katibu wa CCM wilaya Mohammed Lawa, Abdakah Zubery Mmala (Mwenyekiti wa UVCCM wilaya), Jumma Khatibu (Katibu UVCCM wilaya) wakiwemo pia makada na wakereketwa wa chama hicho.

Monday, December 22, 2014

SAKATA LA ESCROW: RAIS KIKWETE AZUNGUMZA NA WAZEE

Na Mwandishi wetu,
Dar.

RAIS Jakaya Kikwete hatimaye leo ametengua nafasi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kupitia hotuba aliyotoa kuzungumzia kashfa ya upotevu wa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.

Hatua hiyo imechukuliwa na Rais Kikwete mbele ya wazee wa Dar es Salaam, aliokuwa akiongea nao na matangazo kurushwa moja kwa moja kupitia televisheni ya taifa na vyombo vingine.

Uchunguzi uliofanywa na kamati ya hesabu za umma ya Tanzania (PAC) ilidai kuwa Profesa Tibaijuka ni mmoja wa watu walionufaika kinyume cha sheria, kwa kujipatia fedha zilizotoka katika akauti hiyo iliyofunguliwa kutunza fedha kusubiri ufumbuzi wa mgogoro wa kibiashara kati ya kampuni ya kusambaza umeme TANESCO na kampuni binafsi ya kuzalisha umeme ya IPTL.

Siku chache zilizopita Profesa Tibaijuka aliitisha mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar Es Salaam, kubainisha kuwa hakuwa akikusudia kujiuzulu kutokana na tuhuma zilizokuwa zikimkabili.

Aidha Rais Kikwete hakutangaza kuwachukulia hatua watumishi wengine waliodaiwa kuhusika na tuhuma hiyo, kwa maelezo kuwa uchunguzi zaidi unatakiwa kwa kila mtuhumiwa.

Kumekuwa na ubishi mkubwa kujadili endapo fedha ambazo ni mabilioni zilizochukuliwa zilikuwa za umma au la. 

Hata hivyo Rais Kikwete alisema maelezo aliyopewa na wataalamu yanaonyesha hazikuwa mali ya TANESCO.

KAYOMBO ALALAMIKIWA NA WAPIGA KURA WAKE KWA KUMTETEA MKURUGENZI MTENDAJI NA MKUU WA WILAYA YA MBINGA, WASEMA MWAROBAINI WAKE UCHAGUZI MKUU MWAKANI

Gaudence Kayombo.
Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya Wakazi wa mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamemtaka Mbunge wa jimbo la Mbinga, Gaudence Kayombo kufuta kauli zake anapokuwa akihutubia wananchi katika majukwaa ya kisiasa na kujenga hoja za kuwatetea Mkurugenzi mtendaji Hussein Ngaga na Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga kwamba ni viongozi wazuri na wameleta maendeleo makubwa wilayani humo.

Sambamba na hilo wananchi hao ambao ni wapiga kura wake, wamesema kuwa kauli za Kayombo kuwatetea viongozi hao ni sawa na kujichimbia kaburi kwa kupoteza nafasi aliyonayo, katika uchaguzi mkuu ujao ambao unatarajiwa kufanyika mwakani kwa nafasi ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

Walifafanua kuwa wanamshangaa Mbunge huyo amekuwa akiwasafisha viongozi hao wawili kwamba wanafanya vizuri, wakati maendeleo mengi yaliyofanywa wilayani humo yamefanywa na viongozi wenzao waliowatangulia na sio wao ambao wamefika hapa wilayani wanamuda mfupi na hakuna jambo jipya la maendeleo walilobuni na  kuweza kujivunia   kwa wananchi wakati mengi yaliyopo wanayoyaendeleza ni yale ambayo yalifanyiwa ubunifu na viongozi wenzao waliowatangulia.

Hayo yalisemwa jana na wakazi wa mji wa Mbinga kwa nyakati tofauti, mara baada ya Mbunge Kayombo kumaliza kuhutubia katika viwanja vya soko kuu mjini hapa, kwenye mkutano wa hadhara ambao uliandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani humo kwa ajili ya kushukuru wapiga kura wake kukipatia viti vingi vya nafasi ya Wenyeviti wa vitongoji, katika chaguzi za serikali za mitaa zilizofanyika hivi karibuni. 

Saturday, December 20, 2014

WAPOTEZA MAISHA KWA MAMBO YA KIMAPENZI NA USHIRIKINA



Steven Augustino na Abbas Mlanya,
Ruvuma.

WATU wawili wamefariki dunia mkoani Ruvuma, katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Tunduru na Namtumbo mkoani humo, ambapo la kwanza linasababishwa na wivu wa kimapenzi na lingine linahusishwa na mambo ya ushirikina.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio lililotokea wilayani Tunduru, walisema kuwa marahemu aliyetambuliwa kwa jina la Yusuph Jafari ambaye amehamia wilayani humo, akitokea wilaya ya Masasi alikuwa kinara wa kutembea na wake za watu na baadaye kuuawa na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, ASP Mihayo Msikhela alisema kuwa tukio la kwanza lilitokea  Disemba 16 mwaka huu katika kitongoji cha Naunditi kijiji cha Majimaji, kilichopo kata ya Muhuwesi wilayani humo.

MKURUGENZI MTENDAJI MBINGA AMDANGANYA RAIS KIKWETE, ADAIWA KUCHOTA FEDHA ZA WAKULIMA WA KAHAWA NA KUZIPANGIA MATUMIZI KINYUME NA TARATIBU ZA USHIRIKA

Rais Jakaya Kikwete.

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SHILINGI bilioni 2 ambazo baadhi ya vyama vya ushirika wa kahawa wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, vilikopeshwa hivi karibuni na shirika la hifadhi ya jamii (NSSF) zimezua malalamiko kwamba, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Hussein Ngaga hakuzipeleka kwenye vyama hivyo badala yake anadaiwa kuziingiza kwenye akaunti ya halmashauri ya wilaya hiyo na kuanza kukopesha vikundi husika.

Imeelezwa kuwa kitendo kilichofanywa na mkurugenzi huyo, ni ukiukwaji wa sheria na taratibu za ushirika, hivyo alitakiwa fedha hizo azifikishe kwanza kwenye ushirika kwa kufuata mgawo husika na sio yeye kuzipangia matumizi na kwamba kwa kufanya hivyo, amemdanganya Rais Jakaya Kikwete kwa kauli yake aliyoitoa hivi karibuni mbele yake kwamba fedha hizo watakabidhiwa walengwa wa vyama vya ushirika.

Rais Kikwete mnamo Julai 19 mwaka huu, alikabidhi mfano wa hundi kwa viongozi wa vyama vya ushirika ambavyo vilikopeshwa fedha hizo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi wilayani humo, kwa vyama vinne ambavyo vilipewa mkopo huo na shirika hilo.

Friday, December 19, 2014

WAANDIKISHAJI NA WASIMAMIZI UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA WILAYANI MBINGA WALALAMIKIA POSHO ZAO

Waziri wa TAMISEMI Hawa Ghasia (kulia) pamoja na Katibu mkuu TAMISEMI Jumanne Sagini. (kushoto)
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

KASORO za uchaguzi zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni hapa nchini, pia hali ya hewa imechafuka wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma kufuatia baadhi ya Waandikishaji na Wasimamizi wa uchaguzi huo, kumlalamikia Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, kwamba malipo ya posho walizolipwa katika zoezi hilo amewalipa kidogo, tofauti na maeneo mengine nje ya wilaya hiyo.
Aidha kufuatia hali hiyo Waandikishaji na Wasimamizi hao wamemuomba Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Hawa Ghasia, kuingilia kati na kuweza kulifanyia kazi jambo hilo ili waweze kupata haki yao ya msingi kwa kazi waliyofanya.
Malalamiko hayo yalitolewa kwa nyakati tofauti walipokuwa wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kwa kuomba majina yao yasitajwe gazetini ambapo walisema kuwa hata wakati wanafanyiwa semina na kupewa miongozo juu ya utekelezaji wa zoezi hilo, hawakulipwa posho badala yake waliambiwa kwamba watalipwa mara baada ya uchaguzi kufanyika.

Thursday, December 18, 2014

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA: WACHOMEWA NYUMBA MOTO KUTOKANA NA MALUMBANO YA KISIASA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

UCHAGUZI wa Serikali za Mitaa ambao umefanyika hivi karibuni Disemba 14 mwaka huu, umeacha makovu wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma kwa baadhi ya viongozi na wakereketwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuchomewa moto nyumba zao na watu wasiojulikana, na kusababisha hasara kubwa ya kuunguliwa mali zilizomo ndani ya nyumba hizo pamoja na kukosa makazi. 

Taarifa za tukio hilo zinaeleza kuwa Diwani wa kata ya Ngapa Rashid Issaya na mwanachama wake Hassan Liugu nyumba zao zilichomwa moto, baada ya kuzuka malumbano ya kisiasa na kuwasababishia hasara kubwa ya kuungua nyumba zao pamoja na mali zilizokuwemo ndani yake.

Sambamba na tukio hilo, mfuasi mmoja wa Chama Cha Wananchi (CUF) Yashua Kawisa (21) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mbesa wilayani humo, naye amejeruhiwa vibaya kwa kukatwa mapanga, wakati akiwa katika kampeni za uchaguzi huo.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUKANYAGWA NA LORI



Na Steven Augustino,
Tunduru.

KIJANA mwenye umri wa miaka 15 aliyefahamika  kwa jina la Khasim Mohammed, mkazi wa kijiji cha Mtangashari wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma amefariki dunia baada ya kupata ajali katika gari, ambalo alikuwa ameomba msaada ili aweze kusafiri.

Mihayo Msikhela kamanda wa polisi wa mkoa huo, alisema kuwa marahemu huyo alifariki dunia papo hapo baada ya kuanguka katika gari hilo.

Alisema ajali hiyo ilitokana na gari lenye namba za usajiri T699 BCX mali ya kampuni ya China Civil Engineering Construction Co.Ltd (CCECC) inayojenga kipande cha barabara kilometa 58.7 kutoka Tunduru mjini hadi Matemanga. 

Tuesday, December 16, 2014

MADIWANI MBINGA KUMSHTAKI MKURUGENZI KWA WAZIRI MKUU

Waziri mkuu, Mizengo Pinda.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

BAADHI ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wanampango wa kwenda kumuona Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda kwa lengo la kufikisha kilio chao juu ya mgogoro ambao unaendelea kati ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo na Afisa elimu wa msingi wa wilaya hiyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, Madiwani hao walisema kuwa wamechoshwa na mambo ambayo yanafanywa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Mbinga, Hussein Ngaga kwa kuendekeza migogoro na mambo yasiyokuwa na tija katika jamii.

Aidha walifafanua kuwa Ngaga ameshindwa kuiongoza wilaya hiyo, kutokana na kuendekeza migogoro na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali na kuchukua hatua ya kumsimamisha kazi kinyume na taratibu za utumishi wa umma wakati hana makosa.

SAFARI YA MWISHO YA MARAHEMU MENAS ANDOYA MBUNDA, ASKOFU NDIMBO AWATAKA WAKRISTO KUTENDA MEMA KATIKA MAISHA YAO

Mzee Asteri Ndunguru, upande wa kulia akisoma taarifa fupi ya marahemu Menas Mbunda Andoya nyumbani kwa marahemu mjini hapa.

Mwili wa marahemu Menas Mbunda Andoya ukiombewa katika kanisa la Mtakatifu Killian lililopo mjini Mbinga.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma naye alishiriki katika ibada ya mazishi hayo, kwenye kanisa la Mtakatifu Killian Mbinga mjini.

Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.

WAKRISTO wametakiwa kuacha matendo ya kumpuuza mwenyezi Mungu, badala yake wametakiwa kutenda mema katika maisha yao ya kikristo kwani hakuna binadamu aliyefunga mkataba na Mungu juu ya kuishi.

Hayo yalisemwa na Askofu mkuu wa jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo alipokuwa akihutubia katika misa takatifu ya mazishi ya marahemu Menas Andoya kwenye kanisa la mtakatifu Kiliani lililopo mjini hapa.

“Miili yetu ni hekalu la bwana na maskani ya mpito hapa duniani, inatupasa kufanya kila jitihada kwa mambo ambayo yanampendeza Mungu, hakuna binadamu asiyekuwa na utashi juu ya kifo”, alisema Ndimbo.

Monday, December 15, 2014

KABROTHER KUINGIA SOKONI NA MKUKI KWA NGURUWE

Msanii Gidion Kabrother akisisitiza jambo, wakati alipokuwa akizungumza na Mkurugenzi wa mtandao huu, Kassian Nyandindi Mbinga mjini mkoa wa Ruvuma.

Hii ni moja kati ya Filamu yake ambayo aliitoa mara ya mwisho, ikitamba kwa jina la Ni Shida, ambayo ipo sokoni.
Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma.

MUIGIZAJI wa filamu nchini, Gidion Simon maarufu kwa jina la Kabrother anatarajia kutoa filamu yake mpya yenye picha kali, ambayo itatamba hivi karibuni kwa jina la Mkuki kwa Nguruwe hivyo wadau mbalimbali amewataka kukaa mkao wa kula na kuipokea albamu hiyo, kwa kuendelea kumuunga mkono kwa kazi zake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kabrother anasema filamu hiyo inazalishwa na kusambazwa na kampuni ya Pamoja Film, iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Anafafanua kuwa filamu hiyo imebeba maudhui mazuri yenye kulenga kuelimisha jamii, ikiwemo inakemea vitendo vinavyofanywa na baadhi ya wafanyakazi mahospitalini wenye tabia ya kutibu wagonjwa, kwa kutumia madawa ambayo yamepitwa muda wake wa matumizi na kusababisha madhara kwa mtumiaji.

“Ndugu mwandishi katika matumizi ya madawa haya feki ni hatari sana, hata mkurugenzi husika mwenye hospitali hujikuta siku ya mwisho hata ndugu yake akiathirika na madawa hayo kwa sababu tu ya uzembe huu na kusababisha nguvu kazi ya taifa hili kupotea”, anasema Kabrother.

Pia filamu hiyo inaiasa jamii hasa kwa wale wenye kipato, kuacha tabia au matendo ya kuumiza wenzao kwa namna moja au nyingine kutokana tu, na hali ya uchumi mzuri walionao.

DEREVA ALIYEFANYA MAUAJI TUNDURU ASAKWA



Na Steven Augustino,
Tunduru.

POLISI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanamsaka dereva aliyekuwa akiendesha pikipiki aina ya SUNLG yenye namba za usajiri T 115 CZE ili aweze kujibu mashitaka ya mauaji aliyoyafanya baada ya kumgonga mwendesha baiskeli.

Dereva huyo ambaye jina lake halijafahamika anadaiwa kufanya mauaji hayo, Disemba 13 mwaka huu majira ya saa 5:00 asubuhi katika kijiji cha Tuleane kilichopo Tarafa ya Mlingoti – Namasakata mjini hapa.

Imeelezwa na Kamanda wa polisi wa mkoa huo, Mihayo Msikhela kuwa mauaji hayo aliyafanya kwa kumgonga na pikipiki Rashid Tawakali (50) wa kijiji cha Nakayaya wilayani humo na kumsababishia kifo papo hapo.

ILE NYOTA ILIYONG'ARA MBINGA KIMAENDELEO IMEZIMIKA, KATIBU MKUU UMOJA WA VIJANA TAIFA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI


Menas Mbunda Andoya wakati wa uhai wake akiwa na mkewe na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hivi karibuni wakati wa uzinduzi wa mradi wake wa kuzalisha umeme, maporomoko ya maji katika kijiji cha Lifakara, kata ya Mbangamao wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.



Na Kassian Nyandindi,
Ruvuma. 

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana Taifa kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Sixtus Mapunda, ametoa salamu za pole kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla, kwa kuondokewa na mwanaharakati ambaye ni mpiganaji katika mchango wa kukuza maendeleo wilayani humo, Marahemu Menas Mbunda Andoya.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Katibu huyo alisema kuwa amepokea taarifa ya kifo cha mwanaharakati huyo, kwa masikitiko makubwa na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo, kuungana pamoja katika kipindi hiki cha majonzi.

Mapunda alifafanua kuwa katika kipindi hiki kigumu, wananchi hawana budi kumuombea kwa Mungu Marahemu huyo, kwani sote tupo safarini na hapa duniani tunapita.

Marahemu Andoya alikuwa mpiganaji hasa katika shughuli nyingi za kimaendeleo wilayani Mbinga, ambapo ameacha kazi muhimu ambayo alikuwa akiitekeleza na yenye kufikia hatua ya mwisho juu ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maporomoko ya maji ambao unafahamika kwa jina maarufu, Andoya Hydro Electric Power (AHEPO) uliopo katika kijiji cha Lifakara kata ya Mbangamao wilayani humo. 

Lengo la mradi huo ukishakamilika taratibu husika, utaunganishwa katika mfumo wa gridi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tawi la Mbinga. 

Sunday, December 14, 2014

WANANCHI WENYE HASIRA KALI WAFANYA MAUAJI NYASA



Na  Steven Augustino,
Nyasa.

WANANCHI wenye hasira kali ambao ni wakazi wa kitongoji cha Libonde kata ya Tingi wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamefanya mauaji ya watu watatu katika tukio ambalo linadaiwa kuwa chanzo chake ni kulipiza kisasi.

ASP Mihayo Msikhela ambaye ni Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 4 mwaka huu, baada ya wananchi hao kuwatia katika mtego na kufanikiwa kuwanasa.

Katika tukio hilo Kamanda Msikhela aliwataja watu waliouawa kuwa ni Herman Ndunguru (25), Kwinibeti Komba (52) na Peter Kapinga (42).

Pamoja na mambo mengine alisema, kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi limejipanga kuwasaka wahusika wote wa tukio hilo, na kuhakikisha wanatiwa mikononi mwa dola ili sheria iweze kufuata mkondo wake.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa watuhumiwa hao, ambapo inadaiwa kuwa chanzo cha tukio la mauaji hayo kilisababishwa na kifo cha binti mmoja muuza baa ambaye hakumtaja jina lake kilichotokea mwezi Novemba mwaka huu kijijini hapo.

Saturday, December 13, 2014

MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA MBINGA, KWA HAYA UNAYOYAFANYA NINGEKUWA MIMI NIMEKUWEKA MADARAKANI NINGEKUFUKUZA KAZI MAPEMA ASUBUHI

Rais Jakaya Kikwete, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

SIRI juu ya mipango ambayo inaendelea kusukwa chini kwa chini, katika kuhakikisha kwamba Afisa elimu msingi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Mathias Mkali anachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani, kufuatia mgogoro uliotengenezwa na Mkurugenzi wake wa Halmashauri ya wilaya hiyo Hussein Ngaga, zimeanza kuvuja ambapo mtandao huu umeelezwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vimeeleza na kudai kwamba licha ya kuwepo kwa mipango ya kufikishwa Mahakamani Afisa elimu huyo, huenda kama itashindikana katika hilo atachukuliwa hata hatua ya kuhamishwa, ilimradi adhma ya mkurugenzi huyo iweze kutimia kama alivyopanga.

Serikali licha ya kuunda tume na kuja kuchunguza tatizo hili linaloendelea sasa kukera wananchi wa Mbinga, imeonekana tume hiyo kumezwa na vigogo wa halmashauri hiyo wakitaka ilinde maslahi yao binafsi, ikiwemo hudaiwa kushiriki kwa namna moja au nyingine katika kupanga mipango hiyo.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa, kumekuwa na vikao ambavyo vimekuwa vikifanyika mara kwa mara katika Ikulu ndogo ya Rais wilayani hapa, kati ya vigogo wa wilaya hiyo na wajumbe husika wa tume hiyo hasa nyakati za usiku na mapema alfajiri.

TUME YATILIWA MASHAKA, BAADHI YA VIGOGO MBINGA WADAIWA KUTENGENEZA MBINU CHAFU KUHARIBU UKWELI ULIOPO

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.

TUME ya watu wawili ambayo imeundwa na serikali, kwa ajili ya kuja kuchunguza mgogoro uliopo kati ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Hussein Ngaga na Afisa elimu msingi wa wilaya hiyo, Mathias Mkali imetiliwa shaka huku ikinyoshewa kidole na kudaiwa kutotenda haki kutokana na tume hiyo kuonekana ikiegemea upande wa mkurugenzi huyo.

Baadhi ya wadau wa elimu wakiwemo na watendaji wa serikali, ambao wameteuliwa kwa ajili ya kuhojiwa walisema hayo mjini hapa, wakati walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wetu mara baada ya kufanyiwa mahojiano na tume hiyo.

“Mambo tunayoulizwa ndani ya tume mengi yanaonesha ni yale yale ambayo yametengenezwa na mkurugenzi, sisi tunapotaka kutoa hoja zetu za msingi tunabanwa sana na kunyimwa uhuru wa kujieleza kweli hapa kuna haki? au tume hii imekuja kwa ajili ya kumbeba mtu”, ? walihoji.

Walisema wanashangazwa kuona wakati mwingine tume imekuwa ikihoji kwa kutumia lugha za vitisho, zenye kuonyesha kubeba kundi la upande mmoja na kwamba chumba cha mahojiano kilichopo katika jengo la ukumbi mdogo wa halmashauri ya wilaya hiyo, wahojiwa wamekuwa hawapewi uhuru wa kutosha wakati wa kujieleza jambo ambalo linajenga kukosa imani nao.

Aidha walieleza kuwa wanashangazwa kumuona Afisa utumishi wa wilaya ya Mbinga, Emmanuel Kapinga, kuwepo ndani ya chumba cha mahojiano na tume hiyo ambapo wakati wa mahojiano muda mwingi amekuwa mtu wa kupinga na kuwa mkali pale mhojiwa anapokuwa akitoa maelezo yenye ukweli juu ya jambo husika linaloulizwa kutoka kwa mjumbe wa tume.