Saturday, December 27, 2014

WAENDESHA PIKIPIKI TUNDURU WACHOMA MOTO VIBANDA NA KULETA FUJO KITUO KIKUU CHA POLISI


Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, ACP Mihayo Msikhela.
Na Waandishi wetu,
Tunduru.

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida waendesha pikipiki maarufu kwa jina la yeboyebo, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma walifanya maandamano makubwa kwa lengo la kupinga vitendo vya unyanyasaji ambavyo wanafanyiwa na askari polisi wa wilaya hiyo, ikiwemo kuwakamata hovyo bila kufuata taratibu.

Madereva hao waliandamana na kufanya fujo katika kituo kikuu cha polisi cha wilaya ya Tunduru, pia waandamanaji hao walichoma moto vibanda vinne ambavyo hutumiwa na kampuni ya State business center na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha.

Kwa nyakati tofauti madereva hao walisema wamechukua maamuzi hayo magumu, baada ya kuchoshwa na vitendo viovu ikiwemo kuombwa rushwa mara kwa mara, ambavyo hufanyiwa na askari hao hasa wa kitengo cha usalama barabarani.


Walisema askari hao wamekuwa wakikaa katika maeneo ya vizuizi barabarani, ambavyo hutumiwa na kampuni hiyo kwa ajili ya kukusanyia ushuru wa halmashauri ya wilaya hiyo ambapo huwakamata madereva hao kwa kutumia kamba zilizopo katika vizuizi hivyo na kuwaamrisha kwa nguvu wawapatie fedha huku wakati mwingine wakiwa hawana makosa.

Akizungumzia tukio hilo Meneja wa kampuni ya State Bussiness center Sajidi Mchucha alisema kuwa, katika tukio hilo waendesha pikipiki hao walichoma moto na kuteketeza kabisa vibanda vyake vilivyojengwa katika maeneo ya barabara ziendazo na kuingia mjini humo.

Mchucha aliyataja maeneo hayo kuwa ni Mlingoti, Biasi, Tuleane na Mkapunda hali ambayo imewatia hasara ya zaidi ya shilingi milioni 5 kwa kampuni yake pamoja na kuteketeza vitabu vya kutunzia kumbukumbu za ofisi yake wakati anapofanya kazi ya kukusanya ushuru.

Alisema katika tukio hilo pia kijana wake wa kukusanya ushuru katika kituo cha Tuleane Yazidu Nanyanga, amenusurika kuuawa baada ya madereva hao wa pikipiki kummwagia mafuta ya petroli kwa nia ya kutaka kumchoma moto.

Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo alisema tayari mlalamikaji amekwisha fungua kesi yenye namba TDR/IR/1058/2014 ambapo Jeshi la polisi linaitumia kufanya uchunguzi ikiwemo kuwakamata waliohusika katika tukio hilo.

No comments: