Sunday, December 14, 2014

WANANCHI WENYE HASIRA KALI WAFANYA MAUAJI NYASA



Na  Steven Augustino,
Nyasa.

WANANCHI wenye hasira kali ambao ni wakazi wa kitongoji cha Libonde kata ya Tingi wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma, wamefanya mauaji ya watu watatu katika tukio ambalo linadaiwa kuwa chanzo chake ni kulipiza kisasi.

ASP Mihayo Msikhela ambaye ni Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, alisema kuwa tukio hilo lilitokea Disemba 4 mwaka huu, baada ya wananchi hao kuwatia katika mtego na kufanikiwa kuwanasa.

Katika tukio hilo Kamanda Msikhela aliwataja watu waliouawa kuwa ni Herman Ndunguru (25), Kwinibeti Komba (52) na Peter Kapinga (42).

Pamoja na mambo mengine alisema, kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi limejipanga kuwasaka wahusika wote wa tukio hilo, na kuhakikisha wanatiwa mikononi mwa dola ili sheria iweze kufuata mkondo wake.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa watuhumiwa hao, ambapo inadaiwa kuwa chanzo cha tukio la mauaji hayo kilisababishwa na kifo cha binti mmoja muuza baa ambaye hakumtaja jina lake kilichotokea mwezi Novemba mwaka huu kijijini hapo.


Baada ya tukio hilo wanafamilia kwa kushirikiana na wananchi wa kitongoji hicho walifanya, ufuatiliaji na kubaini kuwa kati ya marehemu hao kulikuwa na mtu ambaye alionekana akiwa na marehemu binti huyo hadi nyakati za usiku wakati anakwenda kulala.

Alisema wakati wakiwa katika utafiti wa ufuatiliaji wa jambo hilo, ghafla mtu huyo alitoweka kijijini hapo na kutokomea kusikojulikana ambapo katika ufuatiliaji wao pia walibaini kuwa mtuhumiwa huyo, alikuwa amekimbilia katika machimbo yaliyopo nchi jirani ya Msumbiji.

Kamanda Msikhela aliendelea kufafanua kuwa baada ya wananchi hao kubaini hayo walituma watu kwenda kumfuata na kumrejesha hapa nchini, ambapo baada ya kufika walimbana na kumhoji juu ya tukio la kifo cha mwanamke huyo ambaye pia alifanyiwa unyama na unyanyasaji wa kijinsia, tuhuma ambazo alikiri na kuwataja wenzake wawili kuwa ndio alioshirikiana nao katika mauaji hayo hali ambayo iliwatia hasira.

Hata hivyo katika tukio hilo alifafanua kuwa, wananchi hao waliwashambulia kwa kuwapiga kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi yakiwemo mapanga, mawe, mikuki na mishale na kusababisha vifo papo hapo.

No comments: